SHIRIKA LA MAKAZI DUNIANI LAFIKIRIA KUREJESHA OFISI ZAKE NCHINI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Katowice, Poland

Shirika la Makazi Duniani(UN- Habitat) lenye Makao Makuu Jijini Nairobi, Kenya limekubaliana na ombi la Balozi wa Tanzania nchini Kenya ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika hilo, Dr John Stephen Simbachawene la kurudisha Ofisi za Shirika hilo nchini Tanzania.

Balozi Simbachawene alitoa rai hiyo leo Juni 30, 2022 wakati wa kikao cha pamoja cha UNDP, UN- Habitat na Ujumbe wa Tanzania kilichofanyika leo katika Jiji la Katowice, Poland kunakofanyika Kongamano la 11 la Miji Duniani. 

Akijibu ombi hilo la Tanzania,   Mkurugenzi wa Shirika la Makazi Duniani Kanda ya Afrika, Bw. Oumar Sylla  alisema kuwa sera nzuri na uongozi bora wa Rais wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan unaipa moyo taasisi hiyo ya makazi duniani wa kuzirejesha Ofisi hizo nchini Tanzania.

Aidha, amebainisha kuwa Shirika hilo linatambua kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazokuwa na idadi kubwa ya watu duniani katika miaka ijayo, hivyo kuwa na umuhimu wa kuwa na Ofisi hiyo ili kuratibu na kusimamia changamoto zitakazokuwepo  za makazi, ukuaji wa miji na idadi kubwa ya watu. Amesema kuwa kinachotakiwa ili kuwa na Ofisi hiyo ni Tanzania kuhakikisha kuwa inaandaa mazingira yatakayowezesha kuanzishwa tena kwa Ofisi hiyo muhimu.

Naye, Mratibu Mwandamizi wa Miradi ya Uendelezaji wa Makazi wa Shirika hilo, Kanda ya Afrika Bw. Ishaku Maitumbi amesema kuwa Shirika hilo likishirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limesaidia baadhi ya  serikali za Mitaa nchini  Tanzania ambazo tayari zina mipango ya vipaumbele ya maendeleo na Mipango miji, katika kuzijengea uwezo na kuibua miradi mbalimbali.

Amesema kuwa jumla  ya Dola za Kimarekani milioni 30 zinatumika kugharamia miradi katika Halmashauri za Serikali za Mitaa nchini Tanzania zipatazo 15 zilizopo katika mikoa 6 ya Dodoma, Mara, Mwanza, Simiyu, Tanga na Mtwara.  Akabainisha kuwa vigezo vilivyotumika kutoa msaada kwa Halmashauri hizo ni kiwango cha umaskini na mahitaji yake, uwezo wa kutekeleza miradi katika mikoa husika na uwezekano wa miradi  iliyowekezwa kuwa endelevu. 

Kadhalika,  Mkuu wa Utafiti wa UNDP nchini Tanzania Bw. Godfrey Nyamrunda amesema kuwa miradi hiyo ina manufaa makubwa, hivyo  ameziomba Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa zinasimamia kikamilifu miradi inayosaidiwa na taasisi hizo mbili ili iweze kuwa na manufaa kwa nchi. 

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Dr. Abdallah Possi amesema kuwa ili miradi inayosaidiwa iweze kuwa na manufaa ni lazima wanaoisimamia wajengewe uwezo na uelewa hususan unaohusu miji na makazi. 

Wakizungumza katika kikao hicho, wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali nchini Tanzania wanaoshiriki katika Kongamano hilo wameyaomba mashirika hayo kuhakikisha kuwa miradi inayosaidiwa inashirikisha sekta binafsi na Waheshimiwa Wabunge, Madiwani na Mameya kwa kuwa wana umuhimu mkubwa wa kuifanya miradi hiyo kuungwa mkono.

Wameyaomba mashirika hayo kuisaidia sekta ya ardhi na nyumba kwa kuwa zina uwezo mkubwa wa kubadilisha nchi kuwa na miji bora na salama. 

Balozi John Stephen Simbachawene ameyashukuru  mashirika hayo ya Kimataifa kwa misaada wanayoipatia Tanzania na dhamira yao njema ya kuendelea kuisaidia Tanzania. 

Kongamano hilo lenye washiriki wapatao 25,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani linafungwa leo na linatarajiwa kufanyika tena katika Jiji la Cairo Misri mwaka 2024.

Ujumbe wa Tanzania ukiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa UNDP na UN- Habitat baada ya kikao chao kilichojadili miradi inayosaidiwa na mashirika hayo nchini

Mkurugenzi wa UN-  Habitat  Kanda ya Afrika Bw. Oumar Sylla akielezea mipango ya Shirika hilo ya kuisaidia Tanzania, wakati wa kikao cha pamoja na ujumbe wa Tanzania ulioshiriki katika Kongamano la 11 la Miji Duniani Jijini Katowice Poland

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *