
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amemuambia Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa – NHC, Nehemiah Kyando Mchechu kuwa Mkoa wa Dodoma kupitia Kamati yake ya Ujenzi umetenga maeneo mazuri kwa ajili ya ujenzi wa majengo makubwa ya biashara na makazi ambayo yatabadilisha mwonekano wa sasa wa Jiji hilo.
Mtaka amesema kuwa imani kubwa aliyonayo ya utendaji kazi wa Mkurugenzi Mkuu wa NHC ni wazi kuwa Jiji la Dodoma linakwenda kubadilika kabla ya kipindi cha kwanza cha awamu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwani majengo makubwa ambayo yatajengwa katika kipindi hiki yatasaidia kulifanya jiji la Dodoma kuwa la kisasa zaidi.
Mtaka ameyasema hayo leo (tarehe 30/06/2022) kufuatia mwaliko wake wa kukutana na Mkurugenzi Mkuu Mchechu ili kuendelea kubadilisha naye uzoefu kwa ajili ya uendelezaji wa jiji la Dodoma.
Amesema kitendo cha Serikali kuhamishia Makao Makuu yake Dodoma ni dhahiri kuwa jiji la Dodoma linahitaji kubadilika kwa kuwa na majengo makubwa ya kisasa ambayo yatasaidia kukuza uchumi wa nchi na kuonesha uhalisia wa jiji.
“Mchechu nina imani kubwa sana na wewe katika masuala ya ubunifu na uendelezaji miji, nikuombe sasa ufikirie kulibadilisha jiji hili kwa kutujengea majengo makubwa ya kisasa ambayo yatalipa hadhi jiji letu kwa kuwa sasa limekuwa na wageni wengi wakubwa wa Kimataifa ambao wanafika hapa,” amesema Mtaka
Ameongeza kusema kuwa mkoa wa Dodoma umetenga maeneo mengi mazuri ambayo ameyataja na kuwa Kamati yake ya Ujenzi ya Jiji imeyatenga kwa ajili ujenzi wa majengo makubwa ya biashara na makazi ambayo yataendana na hadhi ya Makao Makuu ya nchi.
“Kuna maeneo yapo hapa katikati ya jiji ambayo hayo ninawaombeni mjenge majengo ya kisasa yenye hadhi ya Jiji hili yaende juu yawe mazuri na ya kuvutia yakiwa na umaliziaji bora, NHC tumieni fursa hiyo, tunawaamini sana mnafanya mambo mema kwa nchi,” amesema Mtaka.

Kwa upande wake Mchechu amemshukuru Mkuu wa Mkoa huyo kwa imani aliyonayo kwake na Shirika kwa ujumla na kusema kwamba katika mpango unaoanza kutekelezwa wa ujenzi wa majengo ya kisasa Jiji la Dodoma litajengwa asilimia 20 ya nyumba zote 5,000 huku Jiji la Dar es Salaam kukijengwa nyumba asilimia 50 na mikoa mingine ikijengewa asilimia 30 iliyobaki.
Bw. Mchechu amesema kwa sasa Shirika linakimbizana kuhakikisha linakamilisha miradi minane ya majengo ya Serikali kwa viwango na hadhi iliyotarajiwa na pengine kuwa zaidi ya walivyotarajia wadau wa mawizara..