
Wizara ya Maji inaendelea na mageuzi mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kuwa huduma ya maji inaendelea na utekelezaji wa miradi mipya unafanyika kwa kasi kubwa ili wananchi waendelee kuboresha maisha yao kiuchumi na kijamii kupitia uwepo wa rasilimali maji za kutosha.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema hayo leo Juni 30, 2022 wakati akizindua Bodi ya Nne ya Maji ya Taifa jijini Dodoma.
Ameainisha jitihada zilizofanyika ni pamoja na kuanzisha mfumo wa kijiditali wa kukusanya na kuhifadhi takwimu za maji ambao unaitwa MajiApp, kuanzisha Design Manual ili kuhakikisha kuwa gharama za miradi inayoendana hazitofautiani sana, kuanzisha matumizi ya dira za kulipia kabla (prepay meters) ili kupunguza malalamiko ya wateja wa maji yanayohusu usomaji usio sahihi, kukijengea uwezo Chuo cha Maji ili kiweze kuzalisha Wataalam wa kutosha na kukwamua miradi chechefu 126 kati ya miradi 177 iliyokuwa ikisimamiwa na Halmashauri za Wilaya kabla ya kuanzishwa kwa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Waziri Aweso amesema kupitia taftishi iliyofanywa na Wizara ya Maji, ilionekana kuwa rasilimali za maji zinazofaa kwa matumizi mbalimbali nchini kwa mwaka zilizopo juu ya ardhi zinakadiriwa kufikia wastani wa mita za ujazo bilioni 105 na mita za ujazo bilioni 21zipochini ya ardhi na hivyo kufanya jumla ya rasilimali za maji nchini kufikia mita za ujazo bilioni126.
Amesema kiasi hicho cha rasilimali za maji kinaonesha kuwa kiwango cha maji kilichopo kwa kila mtu kwa mwaka ni takribani wastani wa mita za ujazo 2,250kwa kuzingatia makadirio ya idadi ya watu milioni 55.9 kwa mwaka 2019.

“Kiasi hiki cha maji kwa mtu kwa mwaka kimepungua kutoka wastani wa mita za ujazo 12,600 mwaka 1960 wakati nchi yetu ikiwa na idadi ya watu milioni 10. hadiwastani wa mita za ujazo 2,250 kwa mwaka 2019” Waziri Aweso amesema na kuongeza pamoja na jitihada zinazofanyika ziko changamoto ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi; kuongezeka kwa mahitaji ya maji kunakosababishwa na kuboreka kwa maisha, kuongezeka kwa viwanda na shughuli nyingine za kiuchumi, kuongezeka kwa idadi ya watu; uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibinadamu na matumizi ya maji yasiyo na ufanisi, hususani kwenye kilimo cha umwagiliaji, hivyo kuchangia katika kupunguza kiasi cha upatikanaji wa maji.
Waziri Aweso amesisitiza baada ya Sensa ya Watu na Makazi mwaka huu, takwimu za upatikanaji wa maji zirejewe ili kuendana na wakati, hivyo Bodi ya Nne ya Maji ya Taifa inategemewa kushauri na kuchochea zaidi juu ya kufanya tathmini ya rasilimali za maji juu na chini ya ardhi mara kwa mara ili kuwa na takwimu sahihi kwa nchi ambazo zitaisaidia katika ufanyaji wa maamuzi.

Akiongea katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) ameitaka bodi iliyozinduliwa kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na viongozi, pamoja na jamii ambako ndipokwenye rasilimali za maji zinazotakiwa kuendelezwa kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.
Mhandisi Mahundi amesema bozi izingatie miradi ya utoaji huduma za maji, uendelevu wake unategemea utunzaji wa vyanzo vya maji na usimamizi mathubuti wa rasilimali za maji kwa ujumla.
Wizara ya Maji imejipanga kuwafikishia huduma ya maji wananchi waliopo maeneo ya vijijini kwa asilimia 85 na wananchi wanaoishi maeneo ya mijini kwa asilimia 95 ifikapo mwaka 2025.
