
Na Mwandishi Wetu, Ketowice, Poland
Imeelezwa kuwa changamoto ya ukuaji wa miji na kuwa na miji isiyozingatia ajenda ya dunia inasababishwa na wakuu wa nchi za Afrika kutoipa kipaumbele sekta ya makazi.
Hayo yamesemwa leo Juni 29, 2022 kwenye Kikao cha Mawaziri (African Ministers Caucas) kikichoshirikisha pia Mabalozi na Watendaji wa Taasisi na Mashirika yanayosimamia makazi wanaoshiriki katika Kongamano la 11 la Miji Duniani linaloeendelea katika Jiji la Katowice nchini Poland.
Wakijadili ajenda mpya ya Dunia ya uendelezaji Miji na Makazi, Wakuu hao wamesema kuna umuhimu wa kila nchi Barani Afrika kushiriki kikamilifu kusukuma mbele ajenda ya dunia ya kuwa na miji bora na salama. Hivyo, wametoa wito kwa serikali za nchi za kiafrika kutenga rasilimali fedha ya kutosha kugharamia maendeleo na ukuaji wa Miji na Makazi. Aidha, wameshauri kuwepo na sera endelevu zinazosimamia ukuaji wa miji na kwamba imebainika kwamba kwa sasa suala la ajenda ya maendeleo ya miji na makazi barani Afrika inasimamiwa tu na ngazi ya wizara hali inayopunguza kasi ya kutatua changamoto za miji na makazi.
Kikao hicho kilichohudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa( UN Habitat) lenye Makao Makuu Jijini Nairobi, Kenya Dr. John Stephen Simbachawene, kimependekeza kuwa suala la ajenda mpya ya makazi duniani ikajadiliwa na kusimamiwa na Wakuu wa nchi za husika. Kwa minajili hiyo, wamekubaliana suala hilo likajadiliwe kwenye kikao cha Wakuu wa Nchi za Kiafrika ili kuweka msisitizo kwa kuwaomba Wakuu wa nchi kuweka mamlaka zao kwenye usimamizi wa ajenda hiyo.

Kongamano la Miji Duniani linaloendelea Jijini Katowice Poland lina kauli mbiu “uboreshaji wa miji kwa makazi bora ya baadae” linahusisha washiriki wapatao 25,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani na kwa sehemu kubwa unajadili changamoto za miji na namna ya kuondoa changamoto hizo ili kuwa na miji bora na salama kwa vizazi vijavyo. Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 asilimia 70 ya watu duniani itakuwa ikiishi mijini hivyo kuna umuhimu wa kuwa na mipango madhubuti ya kukabiliana na changamoto za ukuaji wa miji na idadi kubwa ya watu.
Tanzania katika Kongamano hilo ina washiriki kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo Wizara ya TAMISEMI, Wiazara ya Ujenzi na Uchukuzi, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, NHC, DART, TARURA, LATRA na Chuo cha Usafirishaji ambapo miradi mbalimbali na vivutio vilivyopo nchini Tanzania vinaonyeshwa katika Banda la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo Filamu maarufu ya the Royal Tour.
