
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb), amewataka watanzania kuachana na kauli za baadhi ya watu ambao kwa makusudi wamekuwa wakipotosha jamii kuhusu kuhesabiwa na badala yake amewasihi kuungana na Serikali katika kuhamasishana kuhusu umuhimu wa sensa ya watu na makazi inayotarahiwa kufanyika Agosti 23, 2022.
Dkt. Tulia ameyasema hayo leo Juni 29, 2022 wakati akifungua Kongamano maalum la Viongozi wa dini la kuhamasisha Sensa ya watu na makazi lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Mkoani Dar es salaam.
Mhe. Spika amesisitiza kuwa, nchi zote duniani ikiwemo Tanzania zimekuwa na utaratibu wake wa kujua takwimu za watu wake kwa kupitia sensa ili kuweza kurahisisha namna bora ya utoaji huduma kwakuwa hicho ndicho kipimo kikuu.

“Leo tumeungana hapa na Viongozi wetu wa dini na hapa wametuhakikishia ya kwamba suala la sensa ya watu na makazi haijaanza leo na badala yake imekuwepo tangu enzi za mitume, hivyo basi ni Imani yangu kwamba hakutakuwa na mtu yeyote tena ambaye atapingana na zoezi hili muhimu kwa lengo la kuisaidia Serikali yetu inayoongozwa na Mama yetu Samia Suluhu Hassan kukamilisha ndoto zake” amesema Dkt. Tulia

