WAZIRI MKUU MAJALIWA AWAFUNDA MAMEYA, WENYEVITI WA HALMASHAURI

Na Angela Msimbira, OR-TAMISEMI

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewaagiza Waheshimiwa Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri kuhakikisha wanaongeza udhibiti wa matumizi ya mapato katika Halmashauri wanazoziongoza.

Akifungua mafunzo ya siku mbili leo tarehe 28 juni, 2022 ya Mameya na wenyeviti wa Halmashauri zote nchini Mhe. Majaliwa amesema kumekuwa na ubadhilifu mkubwa wa fedha za Serikali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, hivyo ni wajibu wa mameya na wenyeviti wa Halmashauri kudhibiti upotevu wa mapato katika Halmashauri

“Waheshimiwa Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri nawasihi kuwa makini katika kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi yake katika Halmashauri mnazoziongoza ili fedha zinazopatikana ziweze kutatua kero za wananchi” amesema Mhe. Majaliwa

Pia amewagiza viongozi hao kuhakikisha wanasimamia utawala bora na utawala wa kisheria kwenye maeneo wanayoyaongoza ili kusaidia utatuzi wa migogoro iliyopo na kuwashirikisha wale wanounga mkono katika shughuli za maendeleo.

Mhe. Majaliwa amewataka kuhakikisha wananchi wanapata taarifa ya utekelezaji wa mipango na bajeti inayotekelezwa kwenye Halmashauri wanazoziongoza kwa kutumia mikutano ya vijiji ili wajue jinsi wanavyoweza kunufaika na bajeti inayotekelezwa.

Amewataka kuwatumikia makundi ya jamii yaliyopo katika maeneo yao wakiwemo vijana, wazee na makundi maalum kwa kuwashirikisha na kuwahudumia ili kutoa fursa ya kushiriki katika kuleta maendeleo

Vilevile amewaagiza kuahikisha wanasimami utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia ubora na ukamilishaji kwa wakati ili miradi hiyo iweze kudumu kwa miaka

“Jikiteni katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani na fedha zinazotolewa na Serikali na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa kuwa nyie ndio wenye fursa ya kujua maeneo yatakayoibuliwa kuongeza vyanzo vya mapato” amesisitiza

Aidha amewataka Waheshimiwa Mameya na wenyeviti wa Halmashauri kuhakikisha wanasimamia matumizi ya fedha katika Halmashauri zao ili kuweza kujua matumizi sahihi ya fedha na kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mhe. Majaliwa pia wamewahimiza mameya na wenyeviti wa halmashauri kuhakikisha wanadhibiti matumizi ya fedha mbichi, kusimamia mali za halmashauri husani matumizi yasiyosahihi ya magari na kuhakikisha vikao vya kisheria vinafanyika.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa amesema mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kusimamia uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mameya wa Halmashauri za Majiji na Manispaa na Wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya na Miji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *