NHC YAFANYA MAZUNGUMZO NA SHIRIKA LA MAKAZI AFRIKA

Shirika la Nyumba la Taifa limeendelea kukutana na wadau mbalimbali muhimu katika maendeleo ya sekta ya nyumba wanaoshiriki katika Kongamano la 11 la Miji Duniani linaloeendelea katika Jiji la Katowice nchini Poland. 

Leo tarehe 28 Juni 2022, NHC ikiongozwa na Balozi wa Tanzania nchi Kenya ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Makazi Duniani ( UN Habitat) lenye Makao Makuu Jijini Nairobi,  imekutana na kufanya mazungumzo na Shirika la Makazi Afrika (Shelter Afrique) ili kuona uwezekano wa Shirika hilo wa kugharamia ujenzi wa nyumba za gharama nafuu nchini Tanzania. 

Akitoa maelezo ya NHC kwa Ujumbe wa Shirika la Makazi Afrika, Mkurugenzi wa Fedha wa NHC Bw. Adolph Kasegenya amesema kuwa Uongozi Mpya wa Shirika umekuja na maono ya kuwezesha ujenzi wa miradi ya nyumba za gharama nafuu kwa watu wa kipato cha kati na chini ili kutoa fursa kwa Watanzania kumiliki nyumba.

Mkurugenzi wa Fedha wa Shirika la Nyumba la Taifa, Adolph Kasegenya akijadiliana jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Makazi Afrika Bw. Kingsley Muwowo huku Balozi wa Tanzania nchini Kenya Dr John Stephen Simbachawene akishuhudia mazungumzo yaliyofanyika leo Jijini Katowice, Poland.

Amesema changamoto iliyopo ni kupata fedha za kugharamia miradi hiyo na hivyo kuhitaji mazungumzo na Shirika hilo ya kupata mikopo yenye riba na masharti nafuu ili kuwezesha nyumba zitakazojengwa kuwa nafuu.

Akasema kuwa Shirika lina mtaji wa nyumba zake unaofikia shilingi trilioni 5.4, mtaji ambao unaliwezesha Shirika hilo kuweza kukopesheka. Akaeleza ujumbe wa Shirika hilo kuwa NHC ilishaanzisha mazungumzo na Shirika hilo ya kuwezesha ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na kwamba umefika wakati sasa kukamilisha mazungumzo hayo. 

Kaimu Mtendaji Mkuu wa  Shirika hilo la Makazi Afrika Bw. Kingsley Muwowo amesema kuwa Shirika hilo linaliamini Shirika la Nyumba la Taifa(NHC) kwa kuwa mlipaji mzuri wa mikopo yake na kwamba hivi sasa hakuna deni lolote inalodaiwa na taasisi hiyo. Akasema kuwa kwa kuwa NHC ina ardhi na soko la uhakika la nyumba za gharama nafuu, Shelter Afrique iko tayari kukamilisha mazungumzo na NHC kabla ya mwezi Septemba 2022 ili kuwezesha azma ya NHC ya kujenga nyumba hizo.

Naye, Balozi wa Tanzania nchini Kenya Dr. John Stephen Simbachawene ameushukuru ujumbe huo kwa kuonyesha nia ya kuisaidia Tanzania upatikanaji wa nyumba bora za gharama nafuu na ameualika ujumbe huo kutembelea Tanzania ili kukutana na NHC na kuona wenyewe miradi inayohitaji kupatiwa msukumo wa haraka. Ujumbe huo umeukubali mwaliko huo na utaliarifu Shirika la Nyumba laTaifa juu ya ujio wao. 

Kongamano la Miji Duniani linaloendelea Jijini Katowice Poland linahusisha washiriki wapatao 25,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani na kwa sehemu kubwa unajadili changamoto za miji na namna ya kuondoa changamoto hizo ili kuwa na miji bora na salama kwa vizazi vijavyo. Imeelezwa katika Kongamano hilo  kuwa ifikapo mwaka 2050 asilimia 70 ya watu duniani itakuwa ikiishi mijini hivyo kuna umuhimu wa kuwa  na  mipango madhubuti ya kukabiliana na changamoto za ukuaji wa miji na idadi kubwa ya watu. 

Wageni mbalimbali wakipata maelezo katika Banda la Tanzania. Mabalozi wote wawili walikuwepo.

Tanzania katika Kongamano hilo ina washiriki kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, NHC, DART, TARURA, LATRA na Chuo cha Usafirishaji, ambapo miradi mbalimbali na vivutio vilivyopo nchini Tanzania vinaonyeshwa katika Banda la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo Filamu maarufu ya the Royal Tour.

Balozi wa Tanzania nchini Kenya Dr John Stephen Simbachawene akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Makazi Afrika Bw. Kingsley Muwowo ( wa pili kushoto) na ujumbe wa NHC baada ya mazungumzo yaliyofanyika leo Jijini Katowice, Poland.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *