MCHECHU: SEKTA YA NYUMBA NI MGODI ULIOLALA INAHITAJI KUCHIMBULIWA

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu akiwasilisha mpango wa uendelezaji wa sekta ya nyumba nchini unaoenda kutekelezwa na NHC kwa Menejimenti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwenye ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Nehemiah Kyando Mchechu amesema sekta ya nyumba ni mgodi wenye thamani na mapato makubwa kwa taifa na jamii kama itapewa uzito utakaostahili.

Ameyasema hayo wakati akiwasilisha mpango wa uendelezaji wa sekta ya nyumba nchini unaoenda kutekelezwa na NHC kwa Menejimenti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwenye ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.

Mchechu amesema sekta ya nyumba ni mgodi uliolala na wenye fedha nyingi na ina manufaa makubwa katika kuchangia ukuaji wa uchumi na maisha ya Watanzania. 

Amemuhakikishia Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha kuwa Shirika lina hali njema kiuchumi na kwamba linachangia kodi zote ikiwamo kodi ya ongezeko la thamani hivyo kuchangia pato la taifa na uchumi kwa ujumla,

Katika maelezo yake Mkurugenzi Mkuu alielezea miradi ya ujenzi itakayotekelezwa kuwa ni pamoja na  mradi wa nyumba 5,000 utakaotekelezwa kwa awamu tatu tofauti.

Kuhusu Sera ya  Ubia amesema sera hiyo itashirikisha sekta binafsi ili kuongeza kasi ya kuwapatia Watanzania nyumba nyingi na bora.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu alielezea Menejimenti hiyo kuwa ili kuweza kusukuma mbele ajenda ya nyumba, Shirika linahitaji rasilimali watu makini ambayo italiwezesha Shirika kupata tija na kujibu matarajiyo ya watanzania kwa haraka.

Akizungumza baada ya mawasilisho ya mpango huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba amempongeza Bw. Mchechu kwa kuwa na mipango mizuri yenye upeo mpana kuhusu sekta ya nyumba.

“Tuna matumaini makubwa ya kuona NHC inakuwa na kuweza kutimiza ndoto ya kuwezesha makazi bora kwa Watanzania, sisi kama Wizara tutaaiwezesha NHC iweze kufanya vizuri zaidi kuliko ilivyo sasa, waelimisheni Watanzania kwamba jukumu lenu ni kujenga na kuuza nyumba,”amesema.

Amepongeza uamuzi huo wa Shirika kwa kuweza kuwasilisha mpango wao kwa kuwa imewezesha kuwapo fursa nzuri zaidi ya kulifahamu Shirika la Nyumba la Taifa na sekta ya nyumba na kwa ujumla kwani sekta hiyo ikilelewa vyema inaweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa taifa.

Amesema wizara yake italiunga mkono Shirika la Nyumba la Taifa katika kufanikisha ndoto zake za kuwapàtia watanzania makazi bora.  

Menejimenti ya Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Watendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa wakifuatilia wasilisho lililotolewa na  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *