BALOZI SIMBACHAWENE AWATAKA WASHIRIKI WA KONGAMANO LA 11 LA MIJI DUNIANI KUELEZEA VIVUTIO VILIVYOPO TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Katowice, Poland

Balozi wa Tanzania nchini Kenya ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Makazi Duniani lenye Makao Makuu Jijini Nairobi Mheshimiwa Dr. John Stephen Simbachawene amewataka watanzania wanaoshiriki katika Kongamano la 11 la Miji Duniani linalofanyika katika Jiji la Ketowice, Poland kuvitangaza vivutio mbalimbali vilivyopo Tanzania ili kuvutia uwekezaji wa mitaji nchini Tanzania.

Balozi Simbachawene ameyasema hayo leo alipohudhuria ufunguzi rasmi wa Kongamano hilo kubwa la  Miji Duniani lenye washiriki wapatao 25, 000 kutoka sehemu mbalimbali Duniani.

Amewaambia washiriki kutoka Tanzania kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha ushiriki wa Tanzania katika Kongamano hilo na ana matarajio makubwa kuwa ushiriki huo utazidi kuifungua nchi yetu kupata fursa mbalimbali za Kimataifa. 

Awali, kabla ya ufunguzi wa Kongamano hilo, leo asubuhi Balozi huyo akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Dr. Abdallah Possi walihudhuria kikao cha Mawaziri na Wakuu wa Taasisi za Kimataifa za makazi na Miji Duniani kujadili namna bora ya kugharamia miradi mbalimbali inayosaidia kuwa na miji salama.

 Katika Kongamano hilo, Mabalozi hao wameshauri taasisi mbalimbali nchini Tanzania zinazojihusisha na masuala ya nyumba, uendelezaji miji, barabara na usafiri mijini kutumia fursa za mikopo inayotolewa na Benki mbalimbali ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB yenye wanachama 54 wa nchi za Afrika) na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu(IDB yenye wanachama wa nchi za Afrika 23) ili kupata mikopo yenye riba nafuu ya kugharamia ujenzi wa nyumba, barabara mijini na usafirishaji mijini. Benki hizo zilinadi kwenye Kikao hicho cha Mawaziri fursa za mikopo yenye riba na masharti nafuu zinazotolewa na Benki hizo.

Kongamano hilo limefunguliwa leo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Poland Bw. Mateusz Morawiecki ambaye amewataka washiriki wa kongamano hilo la 11 la Miji Duniani kujadili na kuja na mawazo na ubunifu utakaosaidia kuondoa changamoto za makazi duniani ili kuleta maisha bora ya wakaazi wa dunia. 

Kadhalika, Naibu Katibu Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Makazi Duniani(UN Habitat)  Bi. Maimunah Mohd Sharif amezitaka serikali zote duniani kufahamu na kuchukua hatua madhubuti katika kuboresha makazi ya watu duniani.

Amesema kuwa hadi kufikia mwaka 2020 asilimia 50 ya watu walikuwa wakiishi mijini na inatarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2050 asilimia 70 ya watu duniani watakuwa wanaishi mijini na kwamba hivi sana watu zaidi ya bilioni 1 duniani wanaishi katika maeneo yenye makazi holela na hatarishi. Hivyo, serikali zinapaswa kuona kuwa idadi kubwa ya watu mijini italeta changamoto mbalimbali ambazo zinapaswa kuwekewa utaratibu mapema wa kukabiliana nazo. 

Tanzania katika Kongamano hilo inaongozwa na Balozi John Stephen Simbachawene akiwa na taasisi mbalimbali ikiwemo Shirika la Nyumba la Taifa(NHC), DART, Taasisi kadhaa zilizopo chini ya TAMISEMI, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Halmashauri ya Jiji la Dodoma. 

Katika Banda la Tanzania miradi mbalimbali ya Shirika la Nyumba la Taifa(NHC)  inayohitaji kupata wawekezaji na miradi ya taasisi zingine inaonyeshwa na vivutio vya kitalii vinatangazwa kupitia filamu ya the Royal Tour.  Kongamano hilo litaendelea hadi Juni 30 ambapo litatoka na maazimio ya Dunia ya kuboresha Miji na  makazi.

Mkurugenzi Fedha wa Shirika la Nyumba la Taifa Bw. Adolph Kasegenya (Kulia) akiwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya Balozi Simbachawene na kushoto ni Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa, Muungano Saguya, kwenye Kongamano la 11 la Miji Duniani unaofanyika Ketowice, Poland leo. Balozi John Steven Simbachawene anaiwakilisha Tanzania kwenye Mkutano huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *