DKT.MAGEMBE AAGIZA UPATIKANAJI WA HATI KWENYE MAENEO YANAYOJENGWA MIUNDOMBINU YA SERIKALI

OR-TAMISEMI


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR-TAMISEMI) anayeshughukia afya Dkt. Grace Magembe amewaagiza Wakurugenzi wote nchini kuhakikisha maeneo yanaoyojengwa miundombinu ya Serikali yana hati ili kuepuka usumbufu wowote unaoweza kujitokeza.

Dkt. Magembe ametoa agizo tarehe 24 Juni 2022 alipofanya ziara kukagua utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za Afya katika Hospitali ya Wilaya Misenyi Mkoani Kagera.

“ Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya ya afya nchini ili wananchi waweze kupata huduma bora hivyo kukosekana kwa hati katika maeneo hayo ni hatari kubwa, nakuagiza Mkurugenzi hakikisha hati ya Hospitali ya Wilaya ya Misenyi inapatikana haraka iwezekanavyo ili eneo hilo liwe salama”Dkt. Magembe

Sambamba na hilo Dkt. Magembe amemtaka Mkurugenzi huyo kuhakikisha ujenzi wa miundombinu katika hospitali hiyo hasa ujenzi wa jengo la dharula unakamilika kwa wakati huku akizingatia ubora katika utekelezaji huo ili majengo hayo yaweze kudumu kwa muda mrefu lakini pia kuepusha gharama za ukarabati wa mara kwa mara.

Aidha amempongeza Mkurugenzi kwa kusimamia vizuri ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Missenyi na kumtaka kuhakikisha ujenzi wa majengo ya kutolea huduma za afya unazingatia mpangalio wa majengo ili majengo yanayotoa huduma zinazofanana yakae sehemu moja lakini pia kumpa urahisi mgonjwa na watumishi wakati wa utoaji wa huduma.

” Mkurugenzi ujenzi wa jengo la dharula ni mzuri, hongereni sana, kasi ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ni mzuri na kazi inaridhisha, muhimu andaeni na kuzingatia mpangilio wa majengo ( site plan) na pia mzingatie kupendezesha mazingira”amesisitiza Dkt.Magembe

Hii itaepusha msongamano,kituo kitapendeza na majengo yanayotoa huduma zinazofanana kukaa pamoja na hivyo kuwapa urahisi wagonjwa na watumishi”Dkt. Magembe

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Misenyi Bw. Waziri Kombo amemuhakikishia Dkt. Magembe kuwa hati hiyo itapatikana kwa wakati kwakuwa tayari mchakato wa upatikanaji wa hati hiyo ulishaanza na upo katika hatua za ukamilishaji.

Katika ziara yake Dkt. Magembe alitembelea na kukagua utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu na utolewaji wa huduma za Afya katika Hospitali ya Wilaya Misenyi, Kituo cha Afya cha Kakunyu pamoja na Zahanati ya Kashai iliyopo katika Manispaa ya Bukoba ambapo ameridhika na kasi utekelezaji na kuwataka Wakurugenzi wa Halmashauri hizo kuendelea kuzingatia ubora na kasi ya utekelezaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *