BASHUNGWA AAGIZA KITUO CHA HUDUMA KWA WATEJA TAMISEMI KUONGEZEWA UWEZO

Na OR TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe kukiongezea uwezo Kituo cha huduma kwa mteja kwa kuongeza vitendea kazi na mafunzo kwa watoa huduma ili kupanua wigo utoaji wa huduma bora kwa wananchi wengi.

Ametoa agizo hilo leo Juni 21, 2022 jijini Dodoma wakati alipotembelea Kituo cha huduma kwa mteja cha Ofisi ya Rais TAMISEMI na kuungana na watoa huduma kuongea na wateja ambao ni wananchi ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2022.

Bashungwa amesema dhamira ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI ni kutumia kituo hicho kuwapunguzuia tabu wanannchi ya kusafiri kutoka mikoani kuja Dodoma kutatuliwa shida zao ambazo wanaweza kusikilizwa na zikatatuliwa wakiwa huko huko walipo ili kuondokana na gharama na usumbufu.

Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa Watumishi wote kutimiza wajibu wao katika kazi zao kama wanavyofanya Watumishi wanaotoa huduma katika kituo cha huduma kwa wateja kwa kutimiza wajibu wao katikka kituo hicho.

Vile Vile, Amegiza kupewa taarifa ya utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kuhusu uanzishwaji wa Kituo cha kutolea huduma kwa mteja kwa kila Mkoa ili kurahisisha utoaji wa Huduma bora kwa wananchi kuanzia ngazi ya kijiji, kata, Tarafa , Wilaya na Mkoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *