NAIBU WAZIRI MAVUNDE APONGEZA MKOA WA MBEYA KWA KUTENGA MASHAMBA MAKUBWA KWA AJILI YA KILIMO CHA SOYA

Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Anthony Mavunde ameupongeza mkoa wa Mbeya chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa Cde Juma Homera kwa kuchukua hatua ya uamzishwaji wa mashamba makubwa(block farms) maalum kwa ajili ya kilimo cha maharage ya soya.

Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Wilayani Chunya alipotembelea na kukagua mashamba hayo na kufanya mikutano ya wananchi katika kata za Nkung’ungu na Lupa zilizopo tarafa ya Kipembawe,Chunya.

Ziara hiyo inatokana na maazimio ya kikao baina ya Wizara ya Kilimo na Kampuni ya Longping High Tech ya China ambayo ina lengo la kufanya uwekezaji wa zaidi ya bilioni 500 kwa ajili ya kilimo cha Soya na mahindi ya njano katika mikoa ya nyanda za juu kusini ambapo hitaji la msingi la awali ni upatikanaji wa ardhi ya kutosha kwa wakulima kulima mazao hayo.

“Uwekezaji huu ni matokeo ya kazi nzuri anayoifanya Mh Rais Samia Suluhu Hassan katika kuitangaza nchi yetu ya Tanzania huko duniani.

Niwapongeze sana Mkoa wa Mbeya chini ya uongozi wa RC Homera kwa utayari wenu wa kutenga ekari 100,000 za kilimo cha Soya ili kuchangamkia fursa hii iliyoletwa na Kampuni ya Longping High Tech ambao pamoja na huduma nyingine za kitaalamu pia wataleta mbegu bora,teknolojia bora na watakuwa soko la mazao ya wakulima.

Mkakati wa Wizara ni kuwa na mashamba makubwa 10,000 kama haya ifikapo mwaka 2030 katika kuelekea kuikuza sekta ya kilimo asilimia 10 ifikapo mwaka 2030,hii ni fursa kubwa ya vijana wengi kushiriki kwenye kilimo ili malengo haya ya nchi yaweze kutimia”Alisema Mavunde

Akitoa maelezo ya awali,Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Cde Juma Homera ameipongeza wizara ya kilimo katika jitahada zake za kutengeneza fursa za kilimo biashara na kuahidi kuendelea kuandaa mashamba makubwa zaidi katika mkoa wa Mbeya ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kukuza uchumi wa mkoa wa Mbeya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *