MCHECHU AIKARIBISHA SEKTA BINAFSI KUJENGA TANZANIA MPYA

MKUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Nehemia Mchechu ameiarika Sekta Binafsi kushiriki kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi ili kujenga Tanzania mpya.
Akizungumza jana katika makao makuu ya Shirika la Nyumba Zanzibar (NHZ) muda mfupi baada ya kufanya ziara ya kutembelea makao makuu ya shirika hilo yaliyopo Mji Mkongwe ambayo lengo lake ni kuimarisha ushirikiano wa mashirika hayo mawili, Mchechu alisema moja ya vipaumbele ya shirika hilo kuanzia Julai, 2022 ni kushirikiana na Sekta Binafsi lengo likiwa kupata wawekezaji muhimu 200 wenye mitaji isiyopungua Shilingi Bilioni 2 kila mmoja.
Vipaumbele vingine alivyovitaja ni kuangalia rasilimali za shirika ili zitumike kujiendesha kibiashara na kuongeza idadi ya nyumba kupitia sera ya ubia. Alisema rasilimali nyumba zitatumika vema kupangisha na kuuza ili kuongeza kipato na kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba mpya ili kuendelea kutimiza lengo la NHC la kuwa kiongozi katika usimamizi na endelezaji wa miliki nnchini.
Mkurugenzi Mkuu huyo alisema ili kufikia malengo hayo na kutekeleza vipambele vilivyopo sasa kwa ufanisi, NHC litafanya mabadiliko ya watendaji wake kwa kupanga watu sahihi katika nafasi sahihi ili kuwezesha Shirika hilo kufikia matarajio ya Watanzania, Serikali na wadau wa sekta ya nyumba.
“Tutafanya mabadiliko ya ndani kwa kupanga watu sahihi kwenye nafasi sahihi ili kuweza kufanya Shirika lifanye vizuri katika nyanja mbalimbali na kuweza kufanya mabadiliko ili mambo yaendelee kwa kasi, tuweze kukimbia kwa kasi inayotakiwa na Serikali,” alisema Mchechu.
Amebainisha kuwa rasilimali watu ni suala muhimu ili kubadili au kuleta matokeo chanya ndani ya Shirika.
Aidha, Mchechu alisema ili kuweza kuungwa mkono na wadau mbalimbali muhimu, Shirika limekuwa likikutana na wadau wa Sekta Binafsi ili kuwaeleza Mpango Mkakati wa Shirika na Mipango mingine ya kuendeleza sekta ya nyumba
Akimkaribisha Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Mkurugenzi Mkuu wa ZHC, Mwanaisha Ali Said alilishukuru NHC kwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa watendaji wa ZHC na akaahidi kuwa watafika tena kutembelea NHC ili kuweza kupata mafunzo mbalimbali kutoka kwa wakuu wa vitengo na kujua jinsi ya kuendesha Shirika ili kuweza kufikia malengo makubwa zaidi.
“Tunafurahi umerudi tena NHC kwani utatusaidia na tutakuja kuwatembelea huko Bara ili kuweza kupeana ushauri wa namna ya kwenda mbele na kuweza kujifunza kupitia mambo makubwa ambayo NHC imeyafanya na hasa jambo letu tunalofanya sasa la kuendeleza eneo la Mji Mkongwe wa Zanzibar ili kukuza utalii,” alisema Mwanaisha.
Kwa upande wake Mchechu aliahidi kuwa NHC itaendelea kushirikiana na ZHC katika kuwaletea wananchi maendeleo na kusaidia kuleta wawekezaji.
Sanjari na hilo, alilishauri Shirika la Nyumba Zanzibar kujenga nyumba za gharama nafuu na kati na kuruhusu wasiokuwa raia kumiliki nyumba ili kuweza kuongeza mtaji nchini na pia kuongeza masoko.
“Juhudi za Mhe. Rais za kufungua nchi mwelekeo mkubwa itakuwa kuhusisha sekta binafsi hivyo nawashauri Shirika la Nyumba la Zanzibar kukaribisha wawekezaji ili kuweza kuendeleza Shirika na kuongezea kipato. katika kipindi cha miaka mitano ya Mhe Rais Samia, NHC imekusudia kujenga nyumba 5,000 za gharama nafuu na kati,” amesema Mchechu
Alisema kuwa katika kusaidia suala la makazi hasa baada ya Serikali kuhamia Dodoma, Shirika litaendelea kujenga nyumba katika jiji la Dodoma na hivi sasa Shirika litauza nyumba 50 eneo la Medeli Jijini Dodoma ili kupata fedha za kujenga nyumba zingine 100 katika eneo hilo.
Bw. Mchechu alipata fursa ya kutembelea baadhi ya nyumba kongwe za Shirika hilo zinazokarabatiwa katika eneo la Mnadani Mjini Unguja ikiwa ni kazi ya kwanza ya ujenzi kufanywa na Shirika hilo tangu kuanzishwa kwake rasmi mwaka 2014 kwa sheria ya Baraza la Wawakilishi Na. 6.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Nehemia Mchechu alifanya ziara hii ya kikazi kwenye Shirika hili la Nyumba Zanzibar baada ya kukamilisha mwaliko aliyopewa wa kuhudhuria uzinduzi wa Taasisi ya Mwanamke(Mwanamke Initiatives Foundation-MIF) uliofanywa jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *