DAWASA YAZUNGUMZA NA WANANCHI KIBESA, UHAKIKA WA MAJI JULAI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam DAWASA imewatoa hofu ya upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi wa Kibesa-Mpiji kata ya Mabwepande kufuatia utekelezaji wa mradi wa maji Kibesa kuelekea kukamilika mapema Julai mwaka huu.

Meneja wa Mkoa wa kihuduma DAWASA Mabwepande, Ndugu Haruna Taratibu ameeleza kuwa mradi wa maji Kibesa umekamilika kwa awamu ya kwanza na hivi karibuni mkandarasi ataruhusu maji kwa wananchi waanze kupata huduma huku wakiendelea kufikisha huduma kwa maeneo ikifanyika kwa awamu ya pili.

“Napenda kuwahakikishia wananchi wote wa Kibesa hadi Mpiji kuwa watapata huduma ya maji, kwa wale ambao tenki la maji Malolo litaweza kuwafikishia huduma watafikishiwa huduma kwa haraka sana, lakini wale ambao huduma haitafika kupitia tenki hilo basi suluhisho la kudumu linakuja kupitia tenki la maji mshikamano ambalo litakamilika mnamo mwezi wa nane mwaka huu.”ameeleza ndugu Haruna.

Kwa upande wake Meneja Mawasiliano ndugu, Everlasting Lyaro amewatoa wasiwasi watoa huduma binafsi kuwa Mamlaka haitawaondoa kutoa huduma kwa wateja hadi hapo itakapojiridhisha wananchi wote wameunganishiwa na huduma ya majisafi.

“Tunathamini mchago wa watoa huduma binafsi kwa kipindi chote ambacho Mamlaka ilikuwa haijafika, niwatoe hofu kuwa tutaendela kushirikiana hadi pale tutakapo jiridhisha kuwa huduma imemfikia kila mmoja”ameeleza Ndugu Lyaro.

Akizungumza na wananchi katika mkutano huo wa elimu kwa umma, Diwani wa kata ya Mbezi Ndugu Ismail Malata ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kazi inayofanyika kuhakikisha maji yanafika eneo la Kibesa pamoja na Mpiji.

“Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia watendaji wa DAWASA wametoa ushirikiano mkubwa sana na wameweza kufanya kazi kwa ukaribu mno na ofisi za Serikali ya Mtaa, ushirikiano huu umechochea kwa haraka utekelezaji wa mradi huo kwa haraka na wepesi.”ameeleza ndugu Marata

Diwani Marata amewataka wananchi kuongeza ushirikiano kwa DAWASA kwa kulipa huduma za maji Kwa wakati Ili huduma iwe endelevu na yenye kutosheleza wananchi wengi wa Kibesa na baadhi ya eneo la Mpiji

Festo William Mkazi wa Kibesa ameiomba DAWASA kuongeza kasi ya usambazaji Maji kwa Wananchi ili maeneo yote yafikiwe na huduma.

Mradi wa Maji Kibesa-Mpiji umetekelezwa na DAWASA kwa kutumia fedha za ndani kiasi cha Tsh Milioni 234 huku ikihusisha kazi mbalimbali ikiwemo kulaza mabomba ya inchi 8, 6, 2 na 1.5 kwa umbali wa Kilomita 8.2
Chanzo cha Maji ni tanki la Maji Malolo lenye ujazo wa lita Milioni sita

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *