TAASISI ZA ELIMU NCHINI ZATAKIWA KUANGALIA UBORA WA MITAALA-MCHECHU

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemiah Kyando Mchechu akipokea tuzo kutoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma), Profesa Bonaventure Rutinwa ikiwa ni shukurani ya kutambua mchango wake kwa Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS).

Na Mwandishi Wetu

Taasisi za elimu nchini zimetakiwa kuangalia uhalisia wa mitàala ya elimu inayoendana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira kitaifa na kimataifa.

Mchechu ameyasema hayo alipokuwa akitoa kwenye mhadhara ulioandaliwa na Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mchechu amesema ipo haja ya vyuo vikuu kuwa na kanzidata ya wahitimu wake ili kuwa na umoja utakaosaidia kuondoa changamoto mbalimbali za kijamii ikiwemo kusaidia wanafunzi wenye uhitaji wa kupata ufadhili wa masomo na kupata ajira.

Amesema kuwa umoja huo utaimarisha mawasiliano na kupashana habari mbalimbali za kitaifa na kimataifa kwa lengo la kufungua milango ya ajira, ujuzi na fursa mbalimbali.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemiah Kyando Mchechu akijadili jambo na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma), Profesa Bonaventure Rutinwa anayeshuhudia kushoto ni Mkuu wa Shule Kuu ya Biashara, Dkt. Wineaster Anderson

Akizungumza katika Kongamano hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Taaluma, Profesa Bonaventure Rutinwa amesema kuwa amefurahishwa kuona shule kuu hiyo imeweza kuanzisha mfuko wa kusaidia wasio na uwezo na hivyo inaendana na falsafa ya Chuo Kikuu hicho ya kuwa Chuo Kikuu bora duniani.

Amesema kuwa moja ya matatizo makubwa yanayowakabili wanafunzi na hata kuwaletea msongo wa mawazo ni ukosefu wa fedha wa kugharamia masomo yao na kujikimu na amezitaka taasisi mbalimbali kuunga mkono juhudi za kuchangia ubora wa elimu Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemiah Kyando Mchechu katika picha ya pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma), Profesa Bonaventure Rutinwa anayeshuhudia kushoto ni Mkuu wa Shule Kuu ya Biashara, Dkt. Wineaster Anderson, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna na CEO wa Crush Human Capital, Kabeho Nsolo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *