SERIKALI INAENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZILIZOPO KATIKA VIWANDA VYA KATANI-DKT. ASHATU

Dkt. Kijaji Serikali inaendelea kutatua changamoto zilizopo katika viwanda vya Katani

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt .Ashatu Kijaji (Mb.) amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazovikabili viwanda vya kuchakata katani ili kuliendeleza zao hilo la kimkakati katika kukuza biashara, kuongeza ajira na kuongeza pato la taifa.

Waziri Kijaji ameyasema hayo alipofanya ziara na kuongea na wafanyakazia wa Kiwanda cha 21st Century Holdings LTD kinachojihusisha na uchakataji wa kamba zinazotokana na mkonge kilichopo chang’ombe jijini Dar es salaam, Juni 17, 2022

Akiongea na wafanyakazi hao Dkt. Kijaji amesema katika kutatua changamoto hizo Serikali imeondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye mazao yote yanayotokana na zao Mkonge ikiwa ni lalamiko lao kubwa la wenye viwanda vinavyozalisha bidhaa za katani.

Pia Amesema Serikali inaendelea kushughulikia changamoto nyingine ili kuviwezesha viwanda hivyo kushiriki kikamilifu katika soko la ushindani ndani ya nchi, kikanda na kimataifa.

Aidha, Dkt. Kijaji amewahakikishia wafanyakazi wa kiwanda hicho kuwa kiwanda hicho hakitafungwa kwa kuwa Serikali inashughulikia changamoto zinazokikabili kiwanda hicho pamoja na zinazowakabili wafanyakazi hao ikiwemo upatikanaji wa maslahi na haki zao za msingi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *