
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amewahakikishia Wadau wa Sekta ya Kilimo kuwa kipaumbele cha Serikali ni kuimarisha Sekta ya Kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa mvua.
Waziri Bashe ameyazungumza hayo mkoani Morogoro wakati anafungua mkutano wa Wadau wa kilimo cha umwagiliaji ulioandaliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji leo Juni 15, 2022.
Waziri Bashe amesema katika bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2022/2023. Serikali imetenga shilingi bilioni 364 katika kujenda na kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji maji mashamba madogo na makubwa; Huku kukiwa na ongezeko la bilioni 50 ambazo zimetengwa ili kuendeleza umwagiliaji.
Aidha Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itatangaza hekta elfu 10 kwa ajili ya Kilimo cha Umwagiliaji.
Waziri Bashe ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa na utashi wa kisiasa katika Sekta ya Kilimo; Serikali imedhamiria kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji.

“Serikali imetenga hekta elfu 20 kwa ajili ya mashamba ya Vijana ambayo yatajengwa miundombinu ya umwagiliaji ili kupunguza tatizo la ajira nchini”.
“Serikali imefungua milango kwa Wadau wote wa Sekta ya Kilimo kupeleka mawazo yatakayochochea matokeo chanya ili kuinua Sekta ya Kilimo nchini.” Amesema Waziri Bashe.