
Mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa jana dhidi ya Tanzania Prisons , Timu ya KMC FC leo inaendelea na maandalizi kwa ajili ya mchezo mwingine wa kiporo dhidi ya Simba utakaopigwa siku ya Jumapili ya Juni 19 katika uwanja wa Benjamini Mkapa.
Jana KMC FC iliwakaribisha Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Uhuru mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya goli moja kwa moja ambalo lilifungwa na Matheo Anton.
Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni chini ya kocha Mkuu Thierry Hitimana inaendelea kujifua leo kuzisaka alama tatu nyingine kwenye mchezo huo muhimu ambapo KMC itakuwa ugenini.
“Leo tunaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Simba, tunakwenda kwenye mechi ngumu ambayo kila mmoja anataka matokeo, lakini tunawahakikishia mashabiki zetu kuwa tutaenda kupambana uwanjani kuzisaka alama tatu muhimu.”
“Jana hatujatimiza malengo ambayo tulihitaji kwa maana ya kupata alama tatu, lakini hiyo haitutoi kwenye mapambano , bado tunaendelea kujipanga zaidi kwa michezo inayokuja, tunafahamu kuwa mechi zilizobakia zote ni ngumu lakini tutahakikisha tunashinda.

Hata hivyo kwa upande wa Afya za wachezaji wote wako vizuri na wanahali nzuri ya kujiandaa kwenye mchezo huo dhidi ya Simba hivyo mashabiki na watanzania wote wazidi kuwasapoti kwa kuwa Ligi haijaisha na kwamba watahakikisha Timu inamaliza Ligi kwenye nafasi nzuri.
Hadi sasa KMC imecheza michezo 26 na kukusanya jumla ya alama 32 hivyo kupanda hadi nafasi ya tisa kutoka nafasi ya 10 iliyokuwa kabla ya mchezo wa jana na kwamba imebakiza mechi nne ambazo ni dhidi ya Simba, Mbeya kwanza, Biashara pamoja na Dodoma Jiji
Imetolewa leo Juni 15
Na Christina Mwagala
Afisa Habari na Mawasiliano KMC FC.

