TAARIFA YA HALI YA UCHUMI WA TAIFA KWA MWAKA 2021 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2022/23

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT.
MWIGULU LAMECK NCHEMBA MADELU (MB), AKIWASILISHA
BUNGENI TAARIFA YA HALI YA UCHUMI WA TAIFA KWA MWAKA
2021 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2022/23
DODOMA JUNI, 2022
1
UTANGULIZI

 1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako
  Tukufu lipokee na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa
  Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23.
  Pamoja na hotuba hii, nawasilisha vitabu vya Taarifa ya Hali ya
  Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa
  Taifa wa Mwaka 2022/23. Taarifa hizo ndiyo msingi wa bajeti ya
  Serikali kwa mwaka 2022/23 nitakayowasilisha katika Bunge hili
  Tukufu leo alasiri.
 2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda nitumie fursa hii
  kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema, na
  kutuwezesha kukutana kwa mara nyingine katika Bunge hili baada ya
  majadiliano ya bajeti za mafungu mbalimbali. Mkutano huu wa Saba
  wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muhimu
  katika kujadili namna ya kuharakisha maendeleo ya nchi yetu.
 3. Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine tena, nitumie fursa
  hii kutoa pole kwako Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge
  wote, Chama cha Mapinduzi na Watanzania wote kufuatia kifo cha
  aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu wa Bunge la Jamhuri ya
  Muungano wa Tanzania, Marehemu Irene Alex Ndyamkama.
  Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi,
  Amina.
 4. Mheshimiwa Spika, kwa moyo mkunjufu, napenda kutoa
  pongezi zangu za dhati kwako Mheshimiwa Spika kwa kuchaguliwa
  kwa kishindo kuwa Spika wa saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
  wa Tanzania. Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa ujumla wana
  imani kubwa sana na wewe na hawana shaka na uzoefu, weledi na
  umahiri wako katika kusimamia na kuongoza shughuli za Bunge.
  Aidha, napenda kuchukua fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa
  Mussa Azzan Zungu (Mb) kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa
  2
  Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Niungane na
  Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wenzangu kuwaombea kwa
  Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa nguvu, ujasiri na afya njema ili
  muweze kuendelea kutekeleza majukumu yenu ya kuliongoza Bunge
  letu.
 5. Mheshimiwa Spika, Kwa namna ya kipekee, nitoe pongezi
  zangu za dhati, kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa
  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake thabiti na
  utumishi uliotukuka kwa watanzania unaolenga kuleta mapinduzi
  makubwa ya kiuchumi na kijamii. Mheshimiwa Rais ameonesha
  dhamira yake ya dhati ya kulitumikia Taifa kwa uaminifu ambapo
  ameendelea kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali
  zinazolenga kuleta maendeleo kwa Watanzania ikiwemo: kuendelea
  kutekeleza miradi mikubwa ya kielelezo na miradi mingine ya
  kuchochea uchumi na kuimarisha huduma za jamii; kuendeleza
  mapambano dhidi ya rushwa; na kuimarisha ushirikiano wa kikanda
  na kimataifa.
 6. Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amekuwa akiendelea
  kutuongoza kwa vitendo kwa kuchukua hatua mbalimbali za
  kuchochea ukuaji wa uchumi hususan sekta ya utalii ambayo
  iliathirika zaidi na UVIKO-19 ikiwemo kushiriki kwenye filamu
  ijulikanayo kwa jina la The Royal Tour kama Mwongoza Utalii Namba
  Moja Nchini. Mheshimiwa Rais amekuwa chachu na kinara wa utalii
  kupitia filamu hiyo inayolenga kukuza sekta ya utalii ambayo
  inatarajiwa kuzalisha takriban ajira milioni 1.3 na fedha za kigeni dola
  za Marekani bilioni 2.6. Filamu hiyo iliyozinduliwa kwa Mara ya
  Kwanza Jijini New York tarehe 18 Aprili 2022 na baadaye tarehe 21
  Aprili 2022 Jijini Los Angeles. Ndugu Watanzania wenzangu, hii ni
  hatua kubwa sana kwa Taifa letu kwa kuwa filamu hii inapatikana
  kupitia chaneli za Apple TV Plus na Amazon Prime za nchini Marekani
  ambazo zinakadiriwa kuwa na watazamaji zaidi ya milioni 200
  3
  duniani. Ama kwa Hakika Mama Anaupiga Mwingi; na hivyo
  tuna kila sababu ya kuunga mkono jitihada hizi na kwenda
  pamoja na Mama.
 7. Mheshimiwa Spika, kipekee natoa shukrani zangu za dhati
  kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
  Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kumsaidia kazi
  katika nafasi ya Waziri wa Fedha na Mipango. Kwa imani hii
  aliyoionesha kwangu napenda kuwahakikishia Mheshimiwa Rais,
  Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla kuwa
  nitaendelea kutekeleza majukumu yangu kwa bidii kubwa, weledi,
  uaminifu, uadilifu na uzalendo wa kiwango cha hali ya juu ili
  kuhakikisha matamanio ya Mheshimiwa Rais na Watanzania wote ya
  kuwa na maendeleo na ustawi wa kiwango cha juu yanafikiwa.
 8. Mheshimiwa Spika, Sote tunafahamu kuwa, nchi yetu na
  dunia kwa ujumla inaendelea kushuhudia athari za UVIKO-19 ambazo
  zimesababisha kushuka kwa shughuli za kiuchumi duniani, ikiwemo
  uzalishaji, biashara za ndani na kimataifa, utalii na usafirishaji wa
  bidhaa. Katika mwaka 2021, uchumi wa Taifa letu na wa dunia kwa
  ujumla ulianza kuimarika baada ya kupitia katika kipindi cha
  kukabiliana na athari za UVIKO–19. Aidha, wakati Serikali ikiendelea
  na jitihada za kuimarisha uchumi, mwezi Februari 2022 kuliibuka vita
  kati ya mataifa ya Urusi na Ukraine ambayo imesababisha Urusi
  kuwekewa vikwazo na hivyo kusababisha kupanda kwa bei za bidhaa
  mbalimbali katika soko la dunia zikiwemo mafuta na gesi. Sanjari na
  kupanda kwa bei hizo, kumekuwa na uhaba wa baadhi ya bidhaa
  katika soko la Dunia ikiwemo, mbolea, ngano na mafuta ya kula.
  Serikali imeendelea kuchukua hatua katika kukabiliana na athari hizo
  ikiwemo kupokea Mkopo wa Masharti nafuu wa shilingi trilioni 1.3
  zilizoelekezwa katika sekta ya afya, elimu, maji na utalii ili kuchochea
  uchumi na kukabiliana na UVIKO-19; kuongeza bajeti ya kilimo,
  mifugo, uvuvi, nishati na miundombinu ya wafanyabiashara wadogo
  4
  maarufu kama machinga ili kuchochea uzalishaji wa ndani na
  kupunguza nakisi ya urari wa biashara; na kuangalia namna bora ya
  uagizaji mafuta itakayoleta unafuu wa bei kwa wananchi. Aidha,
  nichukue fursa hii kulihakikishia Bunge lako Tukufu na Watanzania
  wote kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili
  kukabiliana na athari hizo kwa lengo la kuleta unafuu wa maisha kwa
  Wananchi.
 9. Mheshimiwa Spika, Nipende kuwashukuru wadau wote
  walioshiriki katika mchakato huu nikianza na Bunge lako Tukufu chini
  ya uongozi wako Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika wa
  Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, napenda
  kumshukuru Mheshimiwa Sillo Daniel Baran (Mb), Mwenyekiti wa
  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na wajumbe wote wa Kamati
  kwa ushauri wao mahiri wakati wa uandaaji wa taarifa nilizowasilisha
  mbele ya Bunge lako Tukufu.
 10. Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa
  Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23
  imeandaliwa kwa kuzingatia mwenendo wa viashiria vya uchumi
  jumla na sekta mbalimbali kwa mwaka husika ikilinganishwa na
  mwaka 2020. Aidha, maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa
  wa Mwaka 2022/23 yamezingatia vipaumbele vya Serikali
  vilivyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa
  Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26, Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi
  Mkuu wa Mwaka 2020 na Hotuba ya Mheshimiwa Samia Suluhu
  Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati
  akilihutubia rasmi Bunge hili la 12 la Jamhuri ya Muungano wa
  Tanzania tarehe 22 Aprili, 2021. Aidha, Mpango umezingatia Sera na
  Mikakati mbalimbali ya kisekta, kikanda na kimataifa zikiwemo Dira
  ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) 2050; Dira ya
  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 2050; Ajenda 2063
  ya Maendeleo ya Afrika; na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.
  5
 11. Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza Mpango wa mwaka
  2022/23, msukumo mkubwa utawekwa katika sekta za uzalishaji
  ambazo ni kilimo, mifugo, uvuvi na nishati kwa kuwa sekta hizi
  huchochea uzalishaji kwa matumizi ya ndani na mauzo nje ya nchi,
  hupunguza nakisi ya urari wa biashara, mfumuko wa bei na huzalisha
  ajira zinazowagusa wananchi wengi. Sambamba na vipaumbele
  hivyo, Serikali itaendelea na utekelezaji wa miradi mingine ya
  maendeleo ikiwemo miradi ya kielelezo ya ujenzi wa Reli kwa
  Kiwango cha Kimataifa (SGR), ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme wa
  Maji la Julius Nyerere – MW 2,115, uboreshaji wa Shirika la Ndege
  Tanzania (ATCL) pamoja na miradi ya elimu, afya, maji, usafiri wa
  anga na majini, bandari, maliasili na utalii, mapinduzi ya TEHAMA,
  miundombinu ya barabara na madaraja na kuboresha mazingira ya
  biashara na uwekezaji ili kukuza ustawi wa sekta binafsi nchini.
  MWENENDO WA HALI YA UCHUMI KWA MWAKA 2021
  Uchumi wa Dunia
 12. Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa
  (IMF) ya Aprili 2022 inaonesha kuwa, uchumi wa dunia uliimarika na
  kufikia wastani wa asilimia 6.1 mwaka 2021 ikilinganishwa na ukuaji
  hasi wa asilimia 3.1 mwaka 2020. Kuimarika kwa uchumi wa dunia
  kumetokana na hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa
  na nchi mbalimbali katika kuimarisha uchumi, ikiwemo utekelezaji wa
  sera za fedha na bajeti zinazochochea shughuli za uchumi
  zilizoathirika na kuendelea kuimarishwa kwa huduma za afya ikiwemo
  uhamasishaji na usambazaji wa chanjo kwa lengo la kupunguza
  athari za UVIKO-19. Hata hivyo, uchumi wa dunia unatarajiwa
  kupungua na kufikia ukuaji wa asilimia 3.6 mwaka 2022. Hii
  inatokana na uwepo wa vita kati ya nchi ya Urusi na Ukraine ambayo
  imesababisha kuongezeka kwa bei za vyakula na nishati hivyo,
  6
  kudhoofisha zaidi matarajio ya kurejea kwa shughuli za kiuchumi
  zilizokuwa zimeathiriwa na UVIKO-19. Ikumbukwe kuwa Urusi ni nchi
  ya pili kwa hifadhi/uzalishaji wa bidhaa za petroli duniani ambapo
  inachangia wastani wa asilimia 12 katika mafuta yote yanayozalishwa
  dunia ikitanguliwa na Marekani yenye mchango wa asilimia 20.
  Aidha, Urusi ndiyo mzalishaji mkubwa wa nishati ya gesi na mafuta
  inayotumika katika shughuli za kiuchumi barani Ulaya. Vilevile, kufikia
  mwaka 2023 na kuendelea uchumi wa dunia unatarajiwa kupungua
  zaidi na kufikia ukuaji wa wastani wa asilimia 3.3 kwa kipindi cha
  muda wa kati iwapo vita kati ya Urusi na Ukraine vitaendelea pamoja
  na kuendelea kuzidisha vikwazo vya kiuchumi kwa nchi ya Urusi.
  Uchumi wa Afrika na Kikanda
 13. Mheshimiwa Spika, mwaka 2021, nchi za Kusini mwa
  Jangwa la Sahara zilikuwa na ukuaji wa uchumi wa wastani wa
  asilimia 4.5, ikilinganishwa na ukuaji hasi wa asilimia 1.7 mwaka
 14. Hii ilitokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa
  ili kuimarisha ukuaji wa uchumi ikiwemo kuboresha huduma za afya
  pamoja na kuimarika kwa bei za bidhaa zinazouzwa nje ya ukanda
  huo baada ya kuondolewa kwa vikwazo vilivyowekwa ili kudhibiti
  kuenea kwa ugonjwa wa UVIKO-19. Ukuaji wa uchumi katika ukanda
  wa Kusini mwa Jangwa la Sahara unatarajiwa kupungua na kufikia
  wastani wa asilimia 3.8 mwaka 2022 na utaongezeka kufika wastani
  wa asilimia 4.0 mwaka 2023.
 15. Mheshimiwa Spika, mwaka 2021, ukuaji wa Pato la nchi za
  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ulikuwa asilimia 4.2
  ikilinganishwa na ukuaji hasi wa asilimia 4.3 mwaka 2020. Aidha,
  ukuaji wa Pato la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ulikuwa asilimia
  5.9 mwaka 2021 ikilinganishwa na ukuaji hasi wa asilimia 1.1 mwaka
 16. Ukuaji chanya wa uchumi katika nchi wanachama wa jumuiya
  hizo ulitokana na kulegezwa kwa masharti yaliyowekwa kwa ajili ya
  7
  kudhibiti maambukizi ya UVIKO–19 pamoja na hatua mbalimbali za
  sera na kibajeti zilizochukuliwa kwa ajili ya kuchochea shughuli za
  kiuchumi katika sekta zilizoathirika na ugonjwa huo.
  Uchumi wa Taifa
  Pato la Taifa
 17. Mheshimiwa Spika, Ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa kipindi
  cha mwaka, 2021 ulikuwa asilimia 4.9 ikilinganishwa na ukuaji wa
  asilimia 4.8 mwaka 2020. Kuongezeka kwa kiwango cha ukuaji wa
  uchumi kumetokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea
  kuchukuliwa na Serikali ikiwemo utekelezaji wa Mpango wa
  Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO–19
  na uwekezaji wa kimkakati hususan katika miundombinu ya nishati,
  maji, afya, elimu, ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege.
  Shughuli za kiuchumi zilizokuwa na ukuaji mkubwa katika kipindi cha
  mwaka 2021 ni pamoja na Sanaa na Burudani (asilimia 19.4),
  Umeme (asilimia 10.0), Uchimbaji Madini na Mawe (asilimia 9.6) na
  Habari na Mawasiliano (asilimia 9.1).
 18. Mheshimiwa Spika, Pato Ghafi la Taifa lilikuwa shilingi trilioni
  161.5 mwaka 2021, ikilinganishwa na shilingi trilioni 151.2 mwaka
 19. Aidha, mwaka 2021, Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa na watu
  milioni 57.7, ikilinganishwa na watu milioni 55.9 mwaka 2020. Kwa
  mantiki hii, Wastani wa Pato kwa Mtu lilikadiriwa kufikia shilingi
  2,798,224.23, sawa na dola za Marekani 1,211.77 mwaka 2021
  ikilinganishwa na shilingi 2,701,039.25, sawa na dola za Marekani
  1,171.51 mwaka 2020.
  Mwenendo wa Bei
 20. Mheshimiwa Spika, Mfumuko wa Bei umeendelea kuwa
  ndani ya lengo la wigo wa asilimia 3 hadi 5. Mwaka 2021, mfumuko
  8
  wa bei uliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 3.7 kwa mwaka
  ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.3 katika kipindi cha mwaka
 21. Aidha, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 3.8 Aprili
  2022 ikilinganishwa na asilimia 3.3 Aprili 2021. Kuongezeka kwa
  mfumuko wa bei kulichangiwa na sababu zilizo nje ya udhibiti wa
  Serikali zikiwemo kuvurugika kwa mnyororo wa uzalishaji na
  usambazaji wa bidhaa na huduma katika soko la dunia kutokana na
  athari za vita baina ya Urusi na Ukraine.
  Utekelezaji wa Sera ya Fedha 2021/22
 22. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/22, malengo ya sera
  ya fedha yalikuwa ni kama ifuatavyo:
  (i) Ukuaji wa fedha taslimu (M0) wa wastani wa asilimia 9.9;
  (ii) Ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) wa
  asilimia 10.0;
  (iii) Ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi wa wastani wa asilimia
  10.6; na
  (iv) Kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosha kuagiza bidhaa na
  huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua miezi
  minne.
 23. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania
  imeendelea kutekeleza sera ya fedha yenye lengo la kuongeza
  ukwasi katika uchumi, ili kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta
  binafsi na kusaidia kuimarisha shughuli mbalimbali za kiuchumi
  zilizokuwa zimeathiriwa na janga la UVIKO-19, hali iliyosaidiwa na
  mfumuko mdogo wa bei ulioendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia
  3 hadi 5. Ili kufanikisha jukumu hili, Benki Kuu ya Tanzania imekuwa
  ikitumia nyenzo mbalimbali za sera ya fedha kwa ajili ya kuongeza
  ukwasi katika sekta ya benki, ikiwemo kutoa mikopo ya muda mfupi
  kwa mabenki, kununua fedha za kigeni kwenye soko la jumla, na
  9
  kuingia mikataba ya kubadilishana fedha za kigeni na mabenki
  (foreign exchange swap). Vilevile, Benki Kuu ilichukua hatua za ziada
  za kisera kwa ajili ya kuchochea ongezeko la mikopo nafuu kwa sekta
  binafsi, hususan shughuli za kilimo. Aidha, kufuatia athari za vita vya
  Ukraine ambayo imeongeza changamoto ya kuvurugika kwa
  minyororo ya ugavi na kusababisha kuongezeka kwa bei ya mafuta
  katika soko la dunia, pamoja na bei ya vyakula kama ngano na
  mafuta ya kula, imesababisha kuongeza kwa mfumuko wa bei ya
  bidhaa hizo nchini na kuhatarisha kupanda zaidi kwa mfumuko wa
  bei. Hali hii imeilazimu Benki Kuu kuanza kupunguza kiasi cha ukwasi
  inachoongeza kwenye uchumi ili kuanza kudhibiti hatari ya kuanza
  kuongezeka kwa kasi ya mfumuko wa bei nchini.
  Ujazi wa Fedha na Karadha
 24. Mheshimiwa Spika, sambamba na utekelezaji wa sera ya
  fedha inayolenga kuongeza ukwasi, ujazi wa fedha umeendelea
  kukua kwa kasi ya kuridhisha. Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Aprili
  2022, wastani wa fedha taslimu uliongezeka kwa asilimia 13.8
  ikilinganishwa na asilimia 2.7 katika kipindi kama hicho mwaka
  uliotangulia, na lengo la wastani wa asilimia 9.9 kwa mwaka
  2021/22. Vilevile, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ulikua
  kwa wastani wa asilimia 13.1, ikilinganishwa ukuaji wa asilimia 6.8 na
  lengo asilimia 10. Ongezeko hili la ukwasi kwenye uchumi limesaidia
  shughuli mbalimbali za uchumi zilizokuwa zimeathirika na UVIKO-19
  kuanza kufunguka kwa ujumla na kuongeza mchango kwenye Pato la
  Taifa.
  Mwenendo wa Mikopo kwa Sekta Binafsi
 25. Mheshimiwa Spika, mikopo kwa sekta binafsi imeendelea
  kukua kwa kasi ya kuridhisha kutokana na sera wezeshi za fedha na
  bajeti, pamoja na hatua zinazoendelea kutekelezwa na serikali
  10
  kuboresha mazingira ya biashara, na utekelezaji wa hatua za kisera
  zilizochukuliwa na Serikali kupitia Benki Kuu zenye lengo la
  kuchochea ukuaji wa mikopo na kushusha viwango vya riba za
  mikopo. Mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa wastani wa asilimia 8.4
  katika kipindi cha Julai 2021 hadi Aprili 2022 ikilinganishwa na ukuaji
  wa wastani wa asilimia 4.3 katika kipindi kama hicho mwaka
  2020/21, na lengo la ukuaji wa asilimia 10.6 kwa mwaka 2021/22.
  Miezi ya hivi karibuni kasi ya ukuaji wa mikopo imeongezeka na
  kufikia asilimia 13.4 kwa mwaka ulioishia Aprili 2022. Sehemu kubwa
  ya mikopo ilielekezwa katika shughuli binafsi ambazo zilipata asilimia
  39.3 ya mikopo yote, ikifuatiwa na shughuli za biashara asilimia 16.7,
  uzalishaji viwandani asilimia 10.1 na kilimo asilimia 7.9. Ni matarajio
  ya serikali kuwa lengo la wastani wa asilimia 10.6 kwa mwaka
  2021/22 litafikiwa kufuatia hatua za kisera na maboresho ya
  mazingira ya biashara yanayoendelea kutekelezwa nchini.
  Mwenendo wa viwango vya riba
 26. Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa sera ya fedha
  yamesaidia kudumisha kiwango cha kutosha cha ukwasi katika sekta
  ya benki, na kupelekea utulivu wa riba za masoko ya fedha ya muda
  mfupi katika viwango vya chini. Mathalani, riba ya siku moja katika
  soko la fedha baina ya mabenki (overnight interbank cash market
  interest rate) ilipungua hadi kufikia wastani wa asilimia 3.42 katika
  kipindi cha Julai 2021 hadi Aprili 2022, kutoka wastani wa asilimia
  3.60 katika kipindi kama hicho mwaka 2020/21. Vilevile, riba ya
  dhamana za muda mfupi (Overall Treasury bills rate) ilipungua hadi
  wastani wa asilimia 4.17 kutoka wastani wa asilimia 4.62 katika
  kipindi kama hicho mwaka 2021.
 27. Mheshimiwa Spika, wastani wa riba za mikopo ya benki kwa
  sekta binafsi kwa ujumla ulipungua japo kwa kasi ndogo hadi
  asilimia 16.44 katika kipindi cha Julai 2021 hadi Aprili 2022,
  11
  ikilinganishwa na wastani wa asilimia 16.59 katika kipindi kama hicho
  mwaka 2020/21. Aidha, wastani wa riba za amana kwa ujumla
  ulikuwa asilimia 6.85 katika, ikilinganishwa na wastani wa asilimia
  6.70. Ni matarajio yetu kuwa hatua za kisera zinazoendelea
  kuchukuliwa na Serikali kupitia Benki Kuu zitasaidia kuendelea
  kupungua kwa riba za mikopo nchini na kusaidia kukuza uchumi wa
  nchi na mazingira bora zaidi ya kufanya biashara.
  Sekta ya Nje
 28. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka kinachoishia
  Aprili 2022, thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ilifikia dola
  za Marekani bilioni 10.62 kutoka dola za Marekani bilioni 8.56 katika
  kipindi kama hicho mwaka 2021. Ongezeko hili kubwa lilitokana na
  kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa zisizo asilia pamoja na mapato
  yatokanayo na shuguli za utalii ikiwa ni matokeo ya hatua
  zilizochukuliwa na mataifa mengine duniani kufungua mipaka yao
  kuruhusu safari za kimataifa kutokana na kupungua kwa maambukizi
  ya UVIKO-19. Aidha, katika kipindi hicho, thamani ya bidhaa na
  huduma zilizoagizwa kutoka nje ilifikia dola za Marekani bilioni 13.29,
  ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 9.27 katika kipindi kama
  hicho mwaka 2021. Ongezeko hilo linatokana na kuongezeka kwa
  uagizaji wa bidhaa za walaji hususan petroli na dawa ambapo
  thamani ya petroli iliongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na
  ongezeko la bei katika Soko la Dunia pamoja na kiwango
  kilichoagizwa katika kipindi hicho.
 29. Mheshimiwa Spika, Thamani ya mauzo ya bidhaa iliongezeka
  kufikia dola za Marekani bilioni 7.03 katika kipindi cha mwaka
  kinachoishia Aprili 2022 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni
  6.36 katika kipindi kama hicho mwaka 2021. Ongezeko hilo lilitokana
  na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa asilia na zisizo asilia ikiwemo,
  bidhaa za maua na mbogamboga, saruji, bidhaa za plastiki, vipodozi
  12
  pamoja na nafaka hususan mchele na mahindi. Aidha, thamani ya
  bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ziliongezeka kutoka dola za Marekani
  bilioni 8.06 katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2021 hadi dola
  za Marekani bilioni 11.09 Aprili 2022. Hali hiyo ilitokana na
  kuongezeka kwa uagizaji wa malighafi, bidhaa za viwandani,
  mitambo na bidhaa za petroli.
 30. Mheshimiwa Spika, mapato yatokanayo na huduma
  yaliongezeka na kufikia dola za Marekani bilioni 3.59 kwa mwaka
  unaoishia Aprili 2022, ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 2.20
  katika kipindi kama hicho mwaka 2021, ongezeko hili lilichangiwa na
  idadi kubwa ya watalii waliongia nchini katika kipindi husika. Aidha,
  katika kipindi husika malipo ya huduma yaliongezeka kutoka dola za
  Marekani bilioni 1.22 na kufikia dola za Marekani bilioni 2.20.
  Ongezeko hili lilichangiwa na ongezeko la gharama za mizigo
  sambamba na ongezeko la gharama za uagizaji wa mafuta.
  Akiba ya Fedha za Kigeni
 31. Mheshimiwa Spika, akiba ya fedha za kigeni imeendelea
  kuwa ya kuridhisha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na
  huduma kutoka nje ya nchi. Hadi kufikia Aprili 2022, akiba ya fedha
  za kigeni ilikuwa dola za Marekani bilioni 5.46 ambayo inatosheleza
  uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha
  takriban miezi 4.8. Mahitaji ya nchi kisheria ni kuwa na kiasi cha
  fedha za kigeni kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma
  kutoka nje ya nchi kwa muda usiopungua miezi 4.0. Aidha, kiwango
  kilichopo kinakidhi pia lengo la kuwa na miezi isiyopungua 4.5 kwa
  nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
  Mwenendo wa Thamani ya Shilingi
 32. Mheshimiwa Spika, thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya
  13
  dola ya Marekani imeendelea kuwa tulivu, ambapo dola moja ya
  Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,308.87 katika soko la
  jumla kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Aprili 2022, ikilinganishwa na
  wastani wa shilingi 2,309.48 katika kipindi cha Julai 2020 hadi Aprili
 33. Hii ni sawa na kuongezeka kwa thamani ya shilingi
  (appreciation) kwa wastani wa asilimia 0.03. Hali hii imechangiwa
  kwa kiasi kikubwa na kuwepo kwa akiba ya kutosha ya fedha za
  kigeni, utulivu wa mfumuko wa bei nchini, mwendelezo wa nakisi
  ndogo katika urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji
  mali nchi za nje, pamoja na utekelezaji wa sera thabiti za fedha na
  bajeti.
  Mwenendo wa sekta ya kibenki
 34. Mheshimiwa Spika, sekta ya kibenki nchini imeendelea
  kubaki imara, stahimilivu na yenye kutengeneza faida ikiwa na mtaji
  na ukwasi wa kutosha. Hadi kufikia mwezi Aprili 2022, rasilimali za
  benki zilifikia kiasi cha Shilingi bilioni 40,198.2, sawa na ongezeko la
  asilimia 12.9 ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana. Aidha,
  amana za benki ziliongezeka hadi kufikia kiasi cha Shilingi bilioni
  28,603.3, sawa na ongezeko la asilimia 11.8, ikilinganishwa na kipindi
  kama hiki mwaka 2020/21. Vilevile, hali ya mitaji ya mabenki na
  ukwasi vimeendelea kuimarika hadi kufikia faida ya mtaji ya asilimia
  18.4 Aprili 2022, ikilinganishwa na faida ya asilimia 10.3 kipindi kama
  hiki mwaka 2020/21.
 35. Mheshimiwa Spika, benki zimeendelea kuongeza utoaji wa
  huduma za kibenki kwa wananchi wengi zaidi kwa kutumia mifumo
  ya kielektroniki yenye gharama nafuu. Kwa upande mwingine, Benki
  Kuu imeendelea kuimarisha usimamizi wa benki na taasisi za fedha
  nchini kwa kutekeleza sera wezeshi na kutoa kanuni na miongozo
  mbalimbali ili kulinda uimara wa sekta hiyo. Vilevile, benki
  zimeelekezwa kutekeleza mipango ya kuongeza mitaji juu ya kiwango
  14
  kinachotakiwa kisheria, ili kuongeza uwezo kwenye utoaji wa mikopo
  kwa sekta binafsi na huduma nyingine za benki.
 36. Mheshimiwa Spika, sekta ya benki inatarajiwa kubaki salama
  na tulivu, sambamba na sera zinazotekelezwa na hatua
  zinazochukuliwa na Serikali pamoja na Benki Kuu ya Tanzania katika
  kuboresha mazingira ya biashara na ufanisi katika utoaji wa huduma
  za fedha nchini. Aidha, Benki Kuu imeendelea kuimarisha jitihada za
  kupunguza kiwango cha mikopo chechefu ambapo, hadi kufikia
  mwezi Aprili 2022 kiwango cha mikopo chechefu kilipungua kufikia
  asilimia 8.23 ikilinganishwa na asilimia 9.77 mwezi Aprili 2021. Benki
  Kuu ya Tanzania inaendelea kufuatilia kwa karibu mikakati ya
  mabenki katika kupunguza mikopo chechefu hadi kufikia kiwango
  kisichozidi asilimia 5.
  Deni la Serikali
 37. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2022, deni la Serikali lilikuwa
  shilingi trilioni 69.44 ikilinganishwa na shilingi trilioni 60.72 kipindi
  kama hicho mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 14.4. Kati ya
  kiasi hicho, deni la nje lilikuwa shilingi trilioni 47.07 na deni la ndani
  lilikuwa shilingi trilioni 22.37. Ongezeko la deni la Serikali lilitokana na
  kupokelewa kwa mikopo mipya kutoka vyanzo vyenye masharti nafuu
  na ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha,
  ongezeko la deni lilitokana na kutolewa kwa hatifungani maalumu
  yenye thamani ya shilingi trilioni 2.18 kwa ajili ya deni la Mfuko wa
  Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) lililotokana na
  michango ya watumishi wa kabla ya mwaka 1999. Taarifa ya tathmini
  ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba 2021 inaonesha kuwa deni
  la Serikali bado ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na
  mrefu kwa kuzingatia ukomo wa viashiria vyote vinavyokubalika
  kimataifa.
  15
  MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO
  WA TAIFA WA MWAKA 2021/22
 38. Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu Serikali imekuwa
  ikitekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22
  ambao ni Mpango wa Kwanza katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu
  wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 wenye
  dhima ya Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya
  Watu. Kutokana na usimamizi thabiti wa Serikali chini ya Mheshimiwa
  Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
  utekelezaji wa Mpango umekuwa na mafanikio makubwa katika
  nyanja zote ikiwemo kiuchumi, miundombinu, kijamii na uwekezaji.
  Mafanikio yaliyopatikana katika sekta mbalimbali ni pamoja na:
  (i) Miundombinu ya Reli: Kuendelea na ujenzi wa Reli ya Kati
  ya Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway – SGR)
  ambapo kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300)
  utekelezaji umefikia asilimia 96.54 na kipande cha Morogoro –
  Makutupora (km 422) asilimia 85.02; kusainiwa kwa mkataba
  wa ujenzi wa kipande cha Makutupora – Tabora (km 368);
  kuendelea na ununuzi wa mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa njia
  ya reli kwa kipande cha Tabora – Isaka (km 165); kuendelea na
  ununuzi wa injini, mabehewa na vifaa vya matengenezo ya njia
  ya reli; na kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa awali
  kwa ajili ya ujenzi wa njia za reli za Tabora – Kigoma (km 411),
  Uvinza – Musongati – Gitega (km 282) na Kaliua – Mpanda –
  Karema (km 321) kwa kiwango cha Standard Gauge. Mafanikio
  mengine ni: Kukamilika kwa ukarabati wa njia ya reli ya Tanga
  – Moshi – Arusha (km 470); kukamilika kwa ukarabati wa
  mabehewa ya mizigo 200 yanayotumika kutoa huduma ya
  usafiri kwa njia ya reli ya Meter Gauge iliyopo; kukamilika kwa
  uundaji wa vichwa vya injini saba (7) vya sogeza; na
  kupokelewa kwa vichwa vya treni vitatu (3), mabehewa 44 ya
  16
  mizigo na mtambo wa kupima ubora wa njia ya reli.
  (ii) Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere – MW
  2,115: Kuendelea na ujenzi wa tuta kuu la bwawa ambapo
  utekelezaji umefikia asilimia 62.01, njia za kupitisha maji ya
  kufua umeme asilimia 74.16, nyumba ya mitambo ya kufua
  umeme asilimia 44.22, kingo za bwawa asilimia 42.82 na kituo
  cha kupokea na kusafirisha umeme kV 400 asilimia 75.44. Kwa
  ujumla utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 60.22.
  (iii) Uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania: Kupokelewa
  kwa ndege tatu (3) ambapo ndege moja (1) ni aina ya Dash 8
  Q400 na mbili (2) ni aina ya Airbus A220 300; kufanyika kwa
  malipo ya awali ya ununuzi wa ndege tano (5) mpya ambapo
  ndege moja (1) aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, ndege mbili
  (2) aina ya Boeing 737-9, ndege moja (1) aina ya De Havilland
  Dash 8-Q400 na ndege moja (1) ya mizigo aina ya Boeing 767-
  300F; kuendelea na ukarabati wa karakana ya matengenezo ya
  ndege ya KIMAFA katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa
  Kilimanjaro (KIA); kuanzisha safari katika vituo vitatu (3) vipya
  vya nje ya nchi vya Lubumbashi, Nairobi na Ndola; kurejesha
  safari za ndani na nje kwa abiria; kuanzisha safari za mizigo za
  kwenda Guangzhou; na kutolewa kwa mafunzo kwa marubani
  102 na wahudumu 108 wa ndani ya ndege.
  (iv) Miradi ya Umeme: kuendelea na ujenzi wa mradi wa kufua
  umeme wa Rusumo – MW 80 ambapo utekelezaji umefikia
  asilimia 91.6; kuendelea na utekelezaji wa mradi wa Kinyerezi I
  Extension MW 185 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 88;
  kukamilika kwa ujenzi wa vituo vya kupooza umeme vya
  Singida na Dodoma katika mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme
  wa Msongo wa kV 400 Iringa – Singida – Shinyanga (Backbone
  Transmission Investment Project – BTIP II); kuendelea na
  17
  ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 Singida –
  Arusha – Namanga ambapo utekelezaji umefikia asilimia 96.1;
  kuendelea na ujenzi wa njia ya usafirishaji wa umeme wa kV
  400 kutoka Rufiji – Chalinze – Kinyerezi – Dodoma ambapo
  utekelezaji umefikia asilimia 37; kuendelea na ujenzi wa mradi
  wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 220 (Rusumo
  – Nyakanazi) ambapo ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme
  umefikia asilimia 61 na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha
  Nyakanazi umefikia asilimia 95; na kuunganishwa umeme kwa
  jumla ya vijiji 8,688 kati ya vijiji 12,345 sawa na asilimia 70.4
  ya vijiji vyote Tanzania Bara.
  (v) Ujenzi na Ukarabati wa Viwanja vya Ndege: kusainiwa
  kwa mkataba kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha
  Kimataifa cha Msalato awamu ya kwanza itakayohusisha ujenzi
  wa njia ya kuruka na kutua ndege pamoja na jengo la abiria;
  kukamilika kwa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Geita;
  kukamilika kwa upanuzi wa njia ya kutua na kuruka ndege na
  kufungwa kwa mfumo wa kuongoza ndege katika Kiwanja cha
  Ndege cha Dodoma; kukamilika kwa usanifu na kuendelea na
  maandalizi ya ujenzi wa jengo la abiria katika Kiwanja cha
  Ndege cha Mwanza; kuendelea na ujenzi na ukarabati wa
  viwanja vya ndege vya Songea (asilimia 96), Mtwara (asilimia
  89), Iringa (asilimia 44.65), Songwe (asilimia 95) na Musoma
  (asilimia 10); kuendelea na maandalizi ya ujenzi na upanuzi wa
  viwanja vya ndege vya Shinyanga, Kigoma, Tabora na
  Sumbawanga vitakavyogharimu Euro milioni 50 sawa na shilingi
  bilioni 136.85.
  (vi) Uendelezaji wa Bandari: Bandari ya Dar es Salaam:
  Kuboreshwa kwa gati namba 1 – 7; na kukamilika kwa ujenzi
  wa gati maalumu la kuhudumia meli za magari (RoRo) na yadi
  ya kuhudumia makasha. Bandari ya Mtwara: kukamilika kwa
  18
  ujenzi wa gati moja lenye urefu wa mita 300; na kuendelea na
  ujenzi wa uzio na sakafu ngumu katika eneo la mita za mraba
  75,807. Bandari ya Tanga: kukamilika kwa uongezaji wa kina
  kwenye lango la kuingia meli kutoka mita nne (4) hadi mita 13
  pamoja na kuweka vifaa vya kuongoza meli.
  Bandari za Maziwa Makuu: Ziwa Victoria: Kukamilika kwa
  ujenzi wa magati ya Nyamirembe, Magarine, Lushamba, Ntama
  na Mwigobero pamoja na gati mbili (2) za majahazi katika
  bandari ya Mwigobero. Ziwa Tanganyika: kukamilika kwa
  ujenzi wa magati ya Kagunga, Sibwesa na Kabwe (Nkasi);
  kukamilika kwa ujenzi wa bandari ya Lagosa pamoja na
  upanuzi wa bandari ya Kasanga; na kuendelea na ujenzi wa
  Bandari za Karema, Kibirizi, Kigoma na Ujiji. Ziwa Nyasa:
  kukamilika kwa ujenzi wa sakafu ngumu katika bandari ya
  Kiwira na Itungi; na kukamilika kwa ujenzi wa gati na
  miundombinu yake katika bandari ya Ndumbi.
  (vii) Kuboresha Huduma za Usafiri na Usafirishaji wa Abiria
  na Mizigo katika Maziwa Makuu
  Kukamilika kwa ukarabati wa meli mbili (2) za New Butiama
  Hapa Kazi Tu na New Victoria Hapa Kazi Tu; kuendelea na
  ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa kazi Tu yenye uwezo
  wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo ambao umefikia
  asilimia 66; na kukamilika kwa ujenzi wa chelezo cha kujengea
  na kukarabati meli katika Bandari ya Mwanza chenye uwezo wa
  kubeba meli au chombo chenye uzito kuanzia tani moja (1)
  hadi tani 4,000.
  (viii) Barabara na Madaraja Makubwa: Kujengwa kwa mtandao
  wa barabara kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilomita
  216.26; na kukarabatiwa kwa kiwango cha changarawe jumla
  ya kilomita 1,124.3 za barabara za mikoa. Kwa upande wa
  19
  barabara zinazosimamiwa na TARURA, jumla ya kilometa
  232.94 za lami, kilomita 8,181.65 za changarawe, madaraja
  405 na makalvati 206 yamejengwa. Miradi iliyokamilika ni
  pamoja na: ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami sehemu
  za Tabora – Nyahua (km 85), Nyahua – Chaya (km 85.4) na
  Manyoni – Itigi – Chaya (km 89.35); barabara za Mbeya –
  Lwanjilo (km 36) na Lwanjilo – Chunya (km 36), sehemu ya
  Chunya – Makongolosi (km 39); na barabara za Mtwara –
  Mnivata (km 50). Barabara zinazoendelea ni pamoja na ujenzi
  sehemu ya Lusitu – Mawengi (km 50) ambapo utekelezaji
  umefikia asilimia 83.79, Kidatu – Ifakara (km 68) asilimia 54.5,
  Makutano – Sanzate (km 50) asilimia 94.1, Mto wa Mbu –
  Loliondo sehemu ya Waso – Sale Jct (km 50) asilimia 98, na
  Moronga – Makete (km 53.5) umefikia asilimia 86. Aidha,
  Serikali imeanza ujenzi wa barabara ya mzunguko katika jiji la
  Dodoma (Dodoma outer ring road) yenye urefu wa kilometa
  (112.3) na kuendelea na maandalizi ya upanuzi wa barabara
  kutoka Dodoma kwenda Singida (km 50), Dodoma – Iringa (km
  50), Dodoma – Arusha (km 50) na Dodoma – Morogoro (km
  70).
  Kwa upande wa madaraja hatua zilizofikiwa ni: kuzinduliwa na
  kuanza kutumika kwa daraja la Tanzanite Dar es Salaam;
  kuanza kutumika kwa daraja la Kiyegeya (Morogoro); na
  kuendelea na ujenzi wa madaraja ya Kitengule (Kagera)
  ambapo utekelezaji umefikia asilimia 90; Wami (Pwani) asilimia
  72.88; Msingi (Singida) asilimia 82; Lower Malagarasi asilimia
  65; na ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi umefikia asilimia
  40.2.
  (ix) Huduma za Afya: Kuendelea na ujenzi wa Hospitali za
  Halmashauri 127, ujenzi wa vituo vya afya 70, ukamilishaji wa
  maboma ya zahanati 564; kukamilika kwa ukarabati wa wodi
  20
  namba 18 katika jengo la Sewa Haji katika haspitali ya Taifa
  Muhimbili kwa ajili ya wodi za kulaza wagonjwa binafsi;
  kukamilika kwa ujenzi na ufungaji wa mtambo wa kuzalisha
  tiba hewa (Oxygen generating plant) katika hospitali ya Taifa
  Muhimbili – Mloganzila; kukamilika kwa ujenzi wa maabara
  maalumu na ufungaji wa mtambo wa kisasa (Angio-Suite)
  katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili – MOI; kukamilika kwa wodi
  ya watoto katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete; ukarabati
  wa jengo la wagonjwa mahututi (asilimia 70), chumba cha
  kufunga mashine ya MRI (asilimia 80) na kujengwa kwa kituo
  cha habari kwa magonjwa ya saratani (Patient Information
  Centre) katika Taasisi ya Saratani Ocean Road; ukarabati wa
  jengo la wagonjwa mahututi katika hospitali ya rufaa ya
  magonjwa ya kifua kikuu Kibong’oto; ukarabati wa chumba cha
  X-ray na Utra-sound katika hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili
  Mirembe; kujengwa kwa majengo ya kutolea huduma za afya
  ya Mama na Mtoto (Maternal and Newborn Wing) katika
  hospitali ya Rufaa Kanda ya Mashariki CCBRT; kuendelea na
  ujenzi wa wodi za wagonjwa wa saratani (asilimia 57) na kliniki
  ya wagonjwa wa macho (asilimia 65) katika hospitali ya rufaa
  kanda ya ziwa Bugando; kuendelea na ujenzi wa vyumba nane
  (8) vya upasuaji (asilimia 80) katika hospitali ya kanda ya
  kaskazini (KCMC); kuendelea na ujenzi wa jengo la ghorofa sita
  (6) la afya ya uzazi ambapo utekelezaji umefikia asilimia 93
  katika hospitali ya rufaa Mbeya; kuendelea na ujenzi wa jengo
  la kuhudumia wagonjwa wa UVIKO – 19 (asilimia 95) katika
  hospitali ya rufaa Shinyanga; kununuliwa na kusambazwa kwa
  chanjo za polio, surua, rubella, kifaduro, pepopunda, homa ya
  ini, homa ya uti wa mgongo na kichomi na chanjo dhidi ya
  UVIKO – 19.
  (x) Elimu: Kuendelea kutekeleza Sera ya elimumsingi bila ada ili
  kuongeza fursa za elimu nchini ambapo hadi Aprili 2022,
  21
  Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 244.5; kuchapishwa na
  kusambazwa kwa vitabu vya kiada 15,609,515 na kiongozi cha
  mwalimu 538,006 kwa masomo yote ya Darasa la VI na VII ili
  kuimarisha uwiano kati ya mwanafunzi na kitabu; kuendelea na
  ujenzi wa shule mpya 232 za Sekondari za kata katika kata
  zisizokuwa na shule za Sekondari; ujenzi wa shule 10 kati ya
  lengo la shule 26 maalumu za bweni za wasichana kwa
  masomo ya Sayansi; kutolewa kwa mafunzo kazini kwa walimu
  10,000 wa sekondari wa masomo ya hisabati na sayansi;
  kuwezesha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuchapisha na
  kusambaza miongozo ya masomo tisa (9); kukusanywa kwa
  mikopo ya shilingi bilioni 156.81 kutoka kwa wanufaika wa
  mikopo iliyoiva na kugharamia mikopo yenye thamani ya
  shilingi bilioni 569.0 kwa wanafunzi 177,777; na kuimarishwa
  kwa Tume ya Nguvu za Atomiki kwa kuendelea na ujenzi wa
  awamu ya pili wa maabara changamano.
  (xi) Maji Mijini na Vijijini: Upatikanaji wa huduma ya maji hadi
  Aprili 2022 umefikia wastani wa asilimia 74.5 vijijini kutoka
  asilimia 72.3 Juni, 2021 na mijini asilimia 86.5 kutoka asilimia
  86 katika kipindi kama hicho mwaka 2021. Baadhi ya miradi
  iliyotekelezwa na hatua zilizofikiwa ni: kuendelea kwa ujenzi wa
  mradi wa maji katika mji wa Kigoma (asilimia 95), Arusha
  (asilimia 80) na mradi wa Mugango – Kiabakari – Butiama
  (asilimia 42). Aidha, katika eneo linalohudumiwa na DAWASA
  (mikoa ya Dar es Salaam na Pwani) utekelezaji wa miradi
  umekamilika kwa zaidi ya asilimia 95. Vile vile, Serikali imeanza
  hatua za kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo la maji katika
  majiji ya Dodoma na Dar es Salaam kwa kutekeleza miradi ya
  Bwawa la Kidunda, bwawa la Farkwa na mradi mkubwa wa
  maji kutoka ziwa Victoria hadi Dodoma.
  (xii) Kilimo, Mifugo na Uvuvi
  22
  Kilimo: Kuzalishwa kwa mbegu bora tani 35,199.39 na miche
  32,301,995 ya mazao mbalimbali; kutolewa kwa pikipiki 7,000
  kwa Maafisa ugani kwa ajili ya kuimarisha huduma za ugani;
  kupatikana kwa mbolea tani 436,452; kuanzishwa kwa
  mashamba 67 yenye ukubwa wa hekta 205,432.45 ambayo kila
  moja lina ukubwa wa kuanzia hekta 20; kuhakikiwa na
  kutambuliwa kwa mashamba matano (5) ya NAFCO yenye
  ukubwa wa ekari 18,980; kukamilika kwa upembuzi yakinifu na
  usanifu wa kina katika skimu tatu (3) za umwagiliaji za
  Mkombozi (Iringa), Idudumo (Nzega) na Ilemba
  (Sumbawanga); kutolewa kwa mafunzo kwa maafisa ugani
  2,486 kuhusu kilimo bora cha alizeti na pamba katika mikoa ya
  Dodoma, Singida, Simiyu, Kilimanjaro, Kigoma na Manyara;
  kukamilika kwa ukarabati wa ghala lenye uwezo wa kuhifadhi
  tani 1,000 za mazao katika Wilaya ya Kiteto; kukamilika kwa
  ukarabati wa vihenge vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 38,000
  katika Mkoa wa Arusha na ghala la Mbugani – Dodoma lenye
  uwezo wa kuhifadhi tani 30,000 za nafaka; kutolewa kwa vibali
  681 kwa wafanyabiashara wa viuatilifu; kuendelea na ujenzi wa
  kiwanda cha mbolea cha FOMI Mkoani Dodoma chenye uwezo
  wa kuzalisha tani 600,000 kwa mwaka; NFRA na CPB
  zilifanikiwa kununua mahindi ya wakulima ambapo kiasi cha
  shilingi bilioni 114 zilitumika; na kufanyika kwa majaribio 88 ya
  kisayansi (bioefficacy field trials) kwa viuatilifu vipya.
  Mifugo: Kuendelea na tafiti na tathmini za teknolojia bora za
  ng’ombe chotara wa maziwa na uzalishaji wa nyama;
  kukamilika kwa ujenzi wa majosho 95 katika mamlaka
  mbalimbali za Serikali za Mitaa; kuanza kwa ujenzi wa majosho
  73 katika halmashauri 58; kuzalishwa na kusambazwa kwa dozi
  43,409,600 za chanjo dhidi ya magonjwa ya Mdondo, Homa ya
  Mapafu ya Ng’ombe na Mbuzi, Kimeta, Chambavu,
  23
  Mchanganyiko wa Kimeta na Chambavu na Kutupa Mimba;
  kuzalishwa kwa jumla ya dozi 50,261 za mbegu za mifugo na
  kusambazwa kwa dozi 31,380 katika mikoa 19 kwa ajili ya
  uhimilishaji; kununuliwa na kusambazwa kwa jumla ya pikipiki
  300 ili kurahisisha utoaji wa huduma za ugani kwa Mamlaka za
  Serikali za Mitaa; kuendelea na ujenzi na ukarabati wa
  miundombinu ya mifugo katika minada 18 nchini; kulimwa kwa
  hekta 800 za malisho ya mifugo katika ranchi za Kongwa, Ruvu
  na West Kilimanjaro; na kuzalishwa kwa jumla ya ndama 3,119
  katika Ranchi za Kikulula, Misenyi, Kongwa, Ruvu, Mkata, West
  kilimanjaro, Mzeri na Kalambo.
  Uvuvi: kusainiwa kwa Mkataba na Mkandarasi China Harbour
  Engineering Co. Ltd kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya uvuvi
  katika eneo la Kilwa Masoko, Lindi; kuendelea na maandalizi ya
  ununuzi wa meli mbili (2) za uvuvi kati ya nne (4)
  zilizopangwa; kukamilika kwa mpango biashara wa ufufuaji wa
  Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO); kujenga ofisi tano (5)
  katika Halmashauri tano (5) kwa ajili ya kuimarisha vikundi vya
  ulinzi shirikishi wa rasilimali za uvuvi; kufanyika kwa kaguzi
  1,863 za kuhakiki ubora na usalama wa samaki na mazao ya
  uvuvi kwenye viwanda vya kuchakata samaki, mialo, magari ya
  kusafirisha samaki, maghala ya kuhifadhi samaki na masoko ya
  samaki; kujenga na kuimarisha miundombinu ya mialo na
  masoko ikiwemo kukamilika kwa ujenzi wa baadhi ya mialo na
  kuendelea na ujenzi wa mialo pamoja na ujenzi wa soko la
  samaki la Mbamba Bay; kuvuliwa kwa tani 324,752.45 za
  samaki zenye thamani ya shilingi trilioni 2.18; kuuzwa nje kwa
  tani 34,841.72 za samaki na Samaki hai 169,089 wa mapambo
  wenye thamani ya shilingi bilioni 475.01; kujengwa kwa
  maabara ya utafiti wa uvuvi katika kituo cha TAFIRI – Dar es
  Salaam; na kufanyika kwa tafiti mbalimbali za mazao ya samaki
  ikiwemo tafiti kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na
  24
  ongezeko la tindikali baharini.
  (xiii) Uendelezaji wa Viwanda: Katika kutekeleza mkakati wa
  kuendeleza sekta ya viwanda kwa kuweka mazingira wezeshi,
  hatua iliyofikiwa ni pamoja na: kuendelea na majadiliano na
  wawekezaji watakaowekeza kwenye miradi ya msingi mitatu
  (3) katika eneo maalumu la uwekezaji Bagamoyo ambayo ni
  Bandari ya kisasa (Modern Seaport Component), sehemu ya
  kanda maalumu kwa ajili ya mizigo na usafirishaji (Logistics
  Park) na sehemu ya mji wa viwanda (Port side Industrial City);
  kukamilika kwa ujenzi wa mabwawa manne (4) ya kuvuna na
  kuhifadhi maji yenye uwezo wa kuhifadhi maji ya mita za ujazo
  1,750,000 na kuendelea na upanuzi wa mashamba ya miwa
  katika kiwanda cha Sukari Mbigiri ambapo utekelezaji wa mradi
  umefikia asilimia 75 kwa upande wa mashamba ya miwa na
  asilimia 45 kwa upande wa ujenzi wa kiwanda; kuendelea
  kuimarisha Sekta Ndogo za ngozi, nguo na mavazi, chuma na
  bidhaa za chuma, mbolea na kemikali za viwandani na
  uchakataji wa bidhaa zinazotokana na kilimo kama vile mafuta
  ya kula, korosho, matunda, maziwa na bidhaa za maziwa.
  Aidha, kupitia maonesho ya Dubai Expro Serikali ilifanikiwa
  kusaini mikataba 36 ya uwekezaji yenye thamani ya shilingi
  trilioni 17 pamoja na mikataba yenye thamani ya shilingi trilioni
  11.7 ilisainiwa wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais ya uzinduzi
  wa filamu ya Royal Tour.
  (xiv) Madini: kukamilika kwa ujenzi wa vituo vitatu (3) vya umahiri
  katika shughuli za uchimbaji madini vya Chunya, Songea na
  Mpanda; kuanzishwa kwa masoko mapya manne (4) ya madini
  na vituo vipya nane (8) vya ununuzi wa madini, hivyo kufanya
  jumla ya masoko ya madini kuwa 42 na vituo vya ununuzi wa
  madini kufikia 75; na kusainiwa kwa mikataba ya ubia kwa ajili
  ya uwekezaji wa kiasi cha takribani dola za Marekani milioni
  25
  1,672.57 kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
  na kampuni za Madini za: Nyanzaga (NMCL) kwa ajili ya
  uchimbaji mkubwa wa madini ya dhahabu na madini ambata ya
  shaba, chuma, nickel, zinc na lead kwenye eneo lenye ukubwa
  wa kilomita za mraba 23.36 Sengerema; Kampuni ya Jacana
  Resources Limited (Strandline Resources Limited) kwa ajili ya
  uchimbaji wa madini ya Heavy Mineral Sand (Beach Sands)
  Kigamboni kwenye eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba
  4.45; Kampuni ya Mahenge Resources Limited (Black Rock
  Mining Ltd) kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya graphite; na
  Kampuni ya Petra Diamond Ltd inayoendelea na uchimbaji wa
  madini ya Almasi katika mgodi wa Williamson Diamonds Limited
  eneo la Mwadui. Katika mikataba hiyo Serikali itamiliki asilimia
  16 ya hisa za kila kampuni.
  (xv) Habari, Mawasiliano na TEHAMA: kukamilika kwa ujenzi wa
  Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa kilomita 409 ambapo
  kilomita 72 zimeunganisha nchi ya Msumbiji kupitia mpaka wa
  Mtambaswala, kilomita 72 zimeunganisha watumiaji wa mwisho
  katika ofisi za Serikali za Msalato, Mtumba na Kikombo Dodoma
  na kilomita 265 zimeunganisha Manyoni – Kambi katoto
  (Chunya); kukamilika kwa ukarabati wa kilomita 105 za ujenzi
  wa mkongo Arusha – Namanga kupitia miundombinu ya
  TANESCO; kukamilika kwa uandaaji wa ramani za mipaka ya
  kiutawala katika Halmashauri 20; na kuendelea na uwekaji wa
  miundombinu ya anwani za makazi nchini.
  Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa kuongeza
  upanuzi na usikivu wa shirika la utangazaj TBC ambapo
  shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na: Kukamilika kwa ujenzi
  wa jengo la kituo cha kurushia matangazo ya masafa ya FM
  katika kituo cha Kisaki mkoani Morogoro; kukamilika kwa ujenzi
  na ufungaji wa mitambo ya kituo cha Redio ya Jamii Makao
  26
  Makuu Jijini Dodoma; kuendelea na ujenzi na ufungaji wa
  mitambo ya masafa ya FM katika mikoa mipya ya Njombe,
  Songwe na Simiyu, sambamba na wilaya za Kilwa, Serengeti
  pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba ambapo utekelezaji
  umefikia asilimia 40; kununuliwa na kufungwa kwa mitambo
  miwili (2) ya kurushia matangazo kwa njia ya Satelaiti (FLY
  AWAY) pamoja na mtambo wa kurusha mubashara matangazo
  ya redio kwa njia ya mtandao (LIVE U); na kukamilisha ujenzi
  wa jengo la Studio na ununuzi wa vifaa vya Chaneli ya
  Televisheni ya TBC 2 katika ofisi za Mikocheni Dar es Salaam.
  (xvi) Maliasili na Utalii: Kuanzishwa kwa mara ya kwanza kwa
  Programu ya Royal Tour iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya
  Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan
  ambayo imelitangaza Taifa na utalii katika Nyanja za kimataifa;
  kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka nje ya nchi kutoka
  watalii 620,867 mwaka 2020 hadi watalii 922,692 mwaka 2021,
  sawa na ongezeko la asilimia 48.6; Hifadhi ya Taifa Serengeti
  ilitangazwa na shirika la Mainland Aggregates Limited la nchini
  Marekani mwaka 2021 kuwa mshindi wa pili barani Afrika na
  wa 12 duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya watumiaji wa
  mtandao wa kijamii wa instagram; kampuni 11 za uwekezaji
  zilipatiwa maeneo ya kujenga huduma ya malazi ya hoteli za
  hadhi ya kitalii katika Hifadhi za Taifa Nyerere, Mikumi,
  Serengeti na Arusha; na Tanzania kuwa mwenyeji katika
  Onesho la Kwanza la Kimataifa la Utalii la Jumuiya ya Afrika
  Mashariki (East African Regional Tourism Expo – EARTE 2021);
  (xvii) Kukuza Biashara na Uwekezaji: wateja 13,836 walipatiwa
  huduma katika kituo cha Huduma za Uwekezaji Mahala Pamoja
  (OSC) ambapo jumla ya miradi 206 (73 wageni, 69 Watanzania
  64 ubia kati ya wageni na Watanzania) ilisajiliwa yenye thamani
  ya dola za Marekani milioni 769.5 na inatarajiwa kutoa ajira
  27
  kwa watanzania wapatao 37,451; kushiriki katika mikutano tisa
  (9) ya ndani ikiwemo Maonesho ya Utalii ya Kanda ya Afrika
  Mashariki (EA Regional Tourism Expo), Dubai Expo 2020,
  Jukwaa la Viwanda lililofanyika Zanzibar na maonyesho ya
  viwanda vidogo (SIDO Trade Fair) yaliyofanyika Kigoma; na
  kutolewa kwa mikopo kwa kampuni 31 zinazozalisha na
  kuchakata bidhaa zitokanazo na mazao ya mifugo na kilimo
  kupitia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kutumia
  Mpango wa SANVN (SIDO, AZANIA Bank, NEEC, VETA na
  NSSF).
  (xviii) Utawala Bora na Utawala wa Sheria: katika
  kuhakikisha kuwa utawala bora na utawala wa sheria
  unashamiri nchini, Serikali imeendelea kuimarisha Mifumo na
  Miundombinu ya Kitaasisi na utoaji haki, uwazi na uwajibikaji
  katika utumishi wa umma, shughuli za Mfuko wa Bunge pamoja
  na Mfuko wa Mahakama. Mafanikio yaliyopatikana ni:
  kulijengea Bunge uwezo kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi
  kwa Waheshimiwa Wabunge na Watumishi katika maeneo ya
  usimamizi wa bajeti, masuala ya kodi, utungaji wa sheria,
  kuendesha shughuli za Bunge kupitia Bunge mtandao,
  ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo, pamoja na
  ujumuishwaji wa masuala ya jinsia katika bajeti; na kununuliwa
  na kufungwa kwa vifaa vya kuhifadhi taarifa ili kuimarisha
  Mamlaka ya Serikali Mtandao. Aidha, kwa upande wa
  mahakama Serikali imekamilisha ujenzi wa vituo vitano (5)
  Jumuishi vya utoaji Haki katika Mikoa ya Dar es Salaam
  (Temeke na Kinondoni), Dodoma, Arusha na Morogoro;
  kuendelea na ujenzi wa makao Makuu ya Mahakama Dodoma,
  Mahakama za Mwanzo sita (6), Mahakama za Hakimu Mkazi
  tatu (3) na Mahakama za wilaya sita (6); kuendelea na ujenzi
  wa Mahakama za Wilaya 26, Mahakama za Mwanzo sita (6) na
  kituo kimoja (1) jumuishi cha utoaji haki katika Mkoa wa
  28
  Mwanza. Vilevile, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa
  haki za watoto, wasichana, wanawake na wanaume;
  mapambano dhidi ya rushwa; na kuendelea na ujenzi wa
  majengo 24 ya Wizara katika mji wa Serikali Dodoma ili
  kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kutokea makao
  makuu ya nchi Dodoma.
  UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO KWA USTAWI
  WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO–19
 39. Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu katika kipindi cha
  mwaka 2019, dunia ilikumbwa na mlipuko wa janga la UVIKO – 19
  ambapo kwa kiasi kikubwa uliathiri afya za jamii na uchumi wa nchi
  mbalimbali ikiwemo Tanzania. Katika kukabiliana na athari za mlipuko
  huo, Serikali iliandaa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na
  Mapambano dhidi ya UVIKO–19 (Tanzania COVID-19 Socio-economic
  Response and Recovery Plan – TCRP). Mpango huo ulizinduliwa rasmi
  tarehe 10 Oktoba, 2021 na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais
  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mpango huo unatekelezwa
  kwa kugharamiwa na mkopo nafuu usio na riba wenye thamani ya
  dola za Marekani milioni 567.25 sawa na shilingi trilioni 1.3 kutoka
  Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Kati ya fedha hizo, dola za
  Marekani milioni 467.3 sawa na shilingi bilioni 1,079.6 zilielekezwa
  Tanzania Bara na dola za Marekani milioni 100 sawa na shilingi bilioni
  231.0 zilielekezwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
 40. Mheshimiwa Spika, kupitia fedha hizo Serikali imeweza
  kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi hususan katika
  sekta ya elimu ambayo ilipokea shilingi bilioni 368.9, afya shilingi
  bilioni 466.9, utalii shilingi bilioni 90.2, maji shilingi bilioni 139.4 na
  Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) shilingi bilioni 5.5.
 41. Mheshimiwa Spika, katika sekta ya elimu, Serikali imeweza
  kupunguza msongamano wa wanafunzi kwa kukamilisha ujenzi wa
  29
  vyumba vya madarasa 12,000 katika shule za sekondari, madarasa
  3,000 ya vituo shikizi katika shule za msingi na mabweni 50 ya
  wanafunzi wenye mahitaji maalumu pamoja na ununuzi wa
  madawati, viti na meza. Aidha, ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi –
  VETA unaendelea katika wilaya 25 ikijumuisha upatikanaji wa vifaa
  vya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika vyuo 11.
 42. Mheshmiwa Spika, katika sekta ya afya, hatua iliyofikiwa ni
  kuanza kwa ujenzi na ukarabati wa majengo 26 ya wagonjwa
  mahututi (ICU), majengo 80 ya huduma za dharura – EMD na
  nyumba 150 (3 in 1) za watumishi katika ngazi ya msingi chini ya
  Ofisi ya Rais – TAMISEMI na ujenzi wa wodi 38 za wagonjwa mahtuti
 • ICU; wodi 20 za huduma za dharura – EMD; nyumba 26 za
  watumishi, uboreshaji wa hospitali za rufaa za mikoa saba (7),
  hospitali maalumu ya Mirembe; kituo cha magonjwa ya kuambukiza
  Kisopwa – Dar es Salaam na kituo cha mfano cha utoaji elimu ya afya
  kwa umma Njedengwa – Dodoma ziko katika hatua mbalimbali za
  ujenzi. Aidha, maandalizi ya ununuzi wa vifaa tiba vya UVIKO – 19
  yamekamilika ikiwemo ununuzi wa mashine 130 za Kidigitali za X –
  Ray, CT – Scan 31, MRI nne (4) na Portable Echo Cardiography saba
  (7) kwa ajili za Hospitali ya Taifa Muhimbili, Ocean Road, Taasisi ya
  Moyo ya Jakaya Kikwete, hospitali za kanda, Hospitali za Rufaa za
  Mikoa pamoja na hospitali ya Emilio Mzena Memorial na Lugalo.
 1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya Maji, Serikali
  imekamilisha taratibu za ununuzi wa seti 25 za mitambo ya kuchimba
  visima katika mikoa yote nchini, seti tano (5) za mitambo ya ujenzi
  wa mabwawa na seti nne (4) za vifaa vya uchunguzi wa maji chini ya
  ardhi. Aidha, utekelezaji wa miradi 218 ya kuboresha huduma za maji
  unaendelea katika maeneo ya mijini na vijijini yenye thamani ya
  shilingi bilioni 139.4, ambapo miradi 46 ni kwa maeneo ya mijini na
  miradi 172 kwa maeneo ya vijijini.
  30
 2. Mheshimiwa Spika, sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta
  zilizopata athari za moja kwa moja kutokana na UVIKO-19. Katika
  kuimarisha sekta hiyo, Serikali inaendelea na ukarabati na ujenzi wa
  miundombinu mbalimbali ikiwemo malango, barabara, njia ya
  watembea kwa miguu, Trails, campsite na bandas katika hifadhi zilizo
  chini ya TANAPA ikiwemo Nyerere National Park, Saadani National
  Park, Kilimanjaro (trails) pamoja na majengo ya kale na nyumba za
  kihistoria. Vilevile, Serikali imetoa mafunzo kwa waongoza watalii
  1,060 katika Hifadhi za Taifa Tarangire, Saadani, Serengeti,
  Ngorongoro na Manyara ili kuimarisha udhibiti wa ubora wa huduma
  za utalii katika kukabiliana na janga la UVIKO – 19.
 3. Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango wa Kukabiliana na Athari
  za Kijamii na Kiuchumi zitokanazo na UVIKO – 19, Serikali
  imewezesha kaya maskini 51,290 katika Halmashauri 35 kupitia
  Mfuko wa TASAF ambapo shilingi bilioni 5.5 zimetumika. Aidha,
  Serikali imewawezesha wajasiriamali vijana, wanawake, na wenye
  ulemavu jumla ya shilingi bilioni 5 kupitia Mpango wa biashara wa
  kuboresha miundombinu na mazingira ya wafanyabiashara wadogo
  katika Halmashauri za Jiji la Dodoma, Mwanza, Arusha, Tanga,
  Mbeya na Dar es Salaam pamoja na Halmashauri za Manispaa za
  Kinondoni, Temeke, Ubungo na Morogoro. Vilevile, Serikali
  imeendelea na hatua za upatikanaji wa mkandarasi kwa ajili ya
  ukarabati wa vyuo vinne (4) vyenye mazingira hatarishi vya watu
  wenye ulemavu katika mikoa minne (4) ya Tanzania Bara kwa
  gharama ya shilingi bilioni 3.5.
  MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2022/23
 4. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
  Mwaka 2022/23 ni wa pili katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa
  Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) wenye
  dhima ya Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa
  Maendeleo ya Watu. Mpango umeandaliwa kwa kuzingatia: Dira ya
  31
  Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa
  wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26; Ilani ya Chama cha Mapinduzi
  kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020; Mapendekezo ya
  Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23; na Sera na
  Mikakati mbalimbali ya kisekta, kikanda na kimataifa zikiwemo Dira
  ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) 2050, Dira ya
  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 2050, Agenda 2063
  ya Maendeleo ya Afrika na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.
  Malengo na Shabaha za Uchumi Jumla kwa Mwaka 2022/23
 5. Mheshimiwa Spika, Malengo na Shabaha za Ukuaji wa
  Uchumi katika kipindi cha mwaka 2022/23, ni kama ifuatavyo:
  (i) Ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 4.7 mwaka 2022
  na asilimia 5.3 mwaka 2023;
  (ii) Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha
  kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa
  asilimia kati ya 3.0 hadi 7.0 katika muda wa kati;
  (iii) Mapato ya ndani kufikia asilimia 14.9 ya Pato la Taifa mwaka
  2022/23;
  (iv) Mapato ya kodi kufikia asilimia 11.7 ya Pato la Taifa mwaka
  2022/23; na
  (v) Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi
  mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa
  kipindi kisichopungua miezi minne (4).
 6. Mheshimiwa Spika, Misingi itakayozingatiwa katika Mpango
  wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23 ni kama ifuatavyo:
  (i) Kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za
  maendeleo;
  (ii) Kuendelea kuhimili athari za majanga ya asili na yasiyo ya asili
  kama vile ukame, vita na magonjwa ya mlipuko;
  (iii) Kuendelea kuwa na utoshelevu wa chakula nchini; na
  32
  (iv) Uwepo wa amani, usalama, umoja, utulivu wa ndani na katika
  nchi jirani.
  Miradi ya Kipaumbele kwa Mwaka 2022/23
 7. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23, Serikali
  itaendelea kukamilisha miradi ya kielelezo na ile ya kimkakati
  inayoendelea. Miradi hiyo inatarajiwa kuwa na matokeo mapana na
  ya haraka katika uchumi, ikiwemo kuzalisha ajira, kipato na
  kuchangia zaidi kupunguza hali ya umaskini nchini. Miradi hiyo
  inajumuisha: Ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa
  (Standard Gauge Railway – SGR); Mradi wa Kufua Umeme wa Maji
  wa Julius Nyerere – MW 2,115; Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania
  (ATCL); Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) –
  Lindi; Kufua Umeme wa Maji wa Ruhudji (MW 358) na Rumakali (MW
  222) – Njombe; Daraja la JPM – Kigongo – Busisi (Mwanza); Ujenzi
  wa barabara na Madaraja Makubwa; kuendeleza Kanda Maalumu za
  Kiuchumi ikiwemo Eneo Maalumu la Uwekezaji Bagamoyo; na
  programu ya kuendeleza ujuzi adimu.
 8. Mheshimiwa Spika, miradi ya kipaumbele kwa mwaka
  2022/23 itakaendelea kuzingatia maeneo matano ya kipaumbele ya
  Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2021/22
  – 2025/26 kama ifuatavyo:
  (a) Kuchochea Uchumi Shindani na Shirikishi: Msisitizo
  utawekwa katika kuimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji
  ikijumuisha kuimarisha utulivu wa uchumi jumla. Miradi
  itakayotekelezwa ni pamoja na: uendelezaji wa miundombinu
  na huduma; ukarabati wa njia kuu za reli ikiwemo kukamilisha
  ukarabati wa njia ya reli kwa maeneo yaliyobaki kwa kipande
  cha Dar es Salaam hadi Isaka (km 970); ujenzi wa barabara za
  kufungua fursa za kiuchumi na zile za kuunganisha Tanzania na
  33
  nchi jirani ikiwemo Barabara ya Kidatu – Ifakara – Lupilo –
  Malinyi – Londo – Lumecha/Songea (km 499), Barabara ya
  Mbeya – Makongolosi – Manyoni (Mkiwa) (km 528), Barabara
  ya Itoni – Ludewa – Manda (km 211); barabara ya Handeni –
  Kibirashi – Kijungu – Kibaya – Njoro – Olboloti – Mrijo Chini –
  Dalai – Bicha – Chambalo – Chemba – Kwa Mtoro – Singida
  (km 460); barabara ya Mafinga – Mtwango – Nyololo –
  Mgololo; Kibaha – Mlandizi – Chalinze – Morogoro Express Way
  (km 158); barabara ya Igawa – Songwe – Tunduma (km 218)
  na mchepuo wa Mbeya (Uyole – Songwe (km 48.9); barabara
  ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti River – Lalago – Maswa
  (km 389); kukamilisha madaraja makubwa ya New Wami
  (Pwani), Kitengule (Kagera), Lower Malagarasi, Mkundi
  (Morogoro), Godegode (Dodoma) na Mtera (Iringa); ujenzi wa
  meli katika ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa; kuendelea
  kuboresha bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na
  Bandari Kavu ya Ruvu; ujenzi wa viwanja vya ndege vya
  Msalato, Shinyanga, Tabora, Kigoma na Lindi; kujenga njia ya
  kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 ya Rufiji – Chalinze –
  Dodoma; kujenga njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV
  400 ya Singida – Arusha – Namanga; kujenga njia ya
  kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 ya Iringa – Mbeya –
  Sumbawanga – Mpanda – Kigoma – Nyakanazi (North West
  Grid Extension); kusambaza umeme vijijini kupitia REA;
  uimarishaji wa Gridi ya Taifa ikijumuisha ujenzi wa vituo vipya
  57 vya kupoza umeme; ujenzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa
  Taifa; kuimarisha huduma za bima hususan bima za mazao na
  huduma za fedha ili kuimarisha shughuli za uwekezaji nchini;
  na kuimarisha mapinduzi ya kidigitali kwa kukuza teknolojia ya
  habari na mawasiliano.
  (b) Kuimarisha Uwezo wa Uzalishaji Viwandani na
  Huduma: miradi itajielekeza katika kuendelea kukuza sekta ya
  34
  kilimo kwa kutekeleza miradi ya kimkakati ya umwagiliaji,
  mbegu na maghala kwa lengo la kuongeza kasi ya ukuaji wa
  sekta ya kilimo kufikia wastani wa asilimia 10 na mchango wa
  shughuli za umwagiliaji kwenye kilimo kufikia asilimia 50 ifikapo
  mwaka 2030. Aidha, Serikali inalenga kuongeza eneo la
  umwagiliaji kufikia hekta 8,500,000 pamoja na kuongeza
  mauzo ya bidhaa za kilimo nje kutoka dola za Marekani bilioni
  1.2 hadi dola za Marekani bilioni 5 ifikapo mwaka 2030. Baadhi
  ya mikakati mahsusi itakayotekelezwa ni pamoja na kujenga
  skimu za umwagiliaji, kuanzisha Mfuko wa Kutengamaza Bei za
  Mazao (Price Stabilisation Fund) na mifuko ya kuendeleza
  mazao, kujenga maghala ya kuhifadhi mazao kwenye vijiji ili
  kukabiliana na changamoto ya upotevu wa mazao baada ya
  mavuno na kuanzisha Youth Agricultural Parks; kuongeza
  matumizi ya teknolojia bora katika uzalishaji, kuimarisha
  huduma za ugani; kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao
  ya kilimo; kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa mitaji katika
  sekta ya kilimo; kuimarisha afya ya mifugo; kuimarisha taasisi
  za utafiti wa kilimo za TARI na ASA; kuimarisha miundombinu
  ya masoko ya mifugo na mazao yake; kufufua Shirika la Uvuvi
  Tanzania – TAFICO na kuliwezesha kujiendesha kibiashara;
  ujenzi wa bandari ya uvuvi – Kilwa Masoko; kununua boti 250
  za kisasa aina ya fibre kwa ajili ya vyama vya ushirika vya
  wavuvi; na kujenga na kukarabati vituo vya ukuzaji viumbe
  maji.
  Kwa upande wa viwanda, miradi itakayotekelezwa ni pamoja
  na: kuendelea kuboresha Kituo cha Kuendeleza Teknolojia ya
  Magari Tanzania – TATC; kuendelea kufufua Kiwanda cha
  Mashine na Vipuri KMTC; kuimarisha Kiwanda cha Viuadudu;
  Uendelezaji wa Viwanda Vidogo – SIDO; kuendeleza Eneo la
  Kongano ya Viwanda – TAMCO; Maeneo Maalum ya Uwekezaji
  (SEZ/EPZ) ya Dodoma, Manyara na Bunda; na kuendelea
  35
  kuweka sera na mazingira wezeshi kwa uwekezaji wa sekta
  binafsi katika viwanda.
  Kwa upande wa eneo la madini na huduma, miradi
  itakayotekelezwa ni pamoja na: kuendelea kufungua masoko
  na vituo vya madini; kuendeleza wawekezaji wadogo wa sekta
  ya madini; kuendeleza utalii kanda ya kusini na kuimarisha
  utalii hususan kwa kuanzisha mazao mapya ya utalii wa fukwe,
  mikutano pamoja na kuimarisha utalii wa ndani; na kukabiliana
  na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori kwa lengo la
  kulinda urithi na maliasili za Taifa.
  (c) Kukuza Biashara na Uwekezaji: Kipaumbele kitakuwa
  katika kusimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kuboresha
  Mazingira ya Biashara ikiwemo kuimarisha mazingira ya kisera
  na kisheria kuhusu uwekezaji pamoja na mifumo ya uratibu na
  usimamizi wa masuala ya uwekezaji kitaifa; kuondoa utozaji
  kodi mara mbili; na kulinda biashara na uwekezaji wa sekta
  binafsi. Aidha, shughuli nyingine zitakazotekelezwa ni pamoja
  na: kutekeleza Programu za Kuboresha Mifumo ya Udhibiti wa
  Biashara; Kukuza Ushiriki wa Watanzania kwenye Miradi ya
  Kimkakati na Uwekezaji; Kukuza Uwezeshaji Wananchi
  Kiuchumi; Kukuza Sekta Binafsi; Uendelezaji wa Masoko ya
  Bidhaa; Udhibiti wa Ubora wa Bidhaa; na kuimarisha masoko,
  maonesho na makongamano ya uwekezaji ya kikanda na
  kimataifa.
  (d) Kuchochea Maendeleo ya Watu: Miradi itakayotekelezwa
  inalenga kuboresha maisha ya watu: Kwa upande wa sekta ya
  elimu shughuli zitakazo tekelezwa ni pamoja na: kuendelea
  kugharamia elimumsingi bila ada; kugharamia mikopo ya
  wanafunzi wa elimu ya juu; kuimarisha vyuo vya elimu ya juu,
  vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na vyuo vya
  36
  ualimu; kuboresha Elimu ya Sekondari; uboreshaji wa
  maktaba; kukamilisha maboma ya vyumba vya madarasa
  yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi; kuboresha mitaala ili
  iendane na mahitaji ya soko; kujenga shule mpya katika
  maeneo yenye mahitaji; na kugharamia uboreshaji wa lishe
  shuleni.
  Kwa upande wa eneo la afya, miradi itakayotekelezwa ni
  pamoja na: kuimarisha huduma za afya hususan ujenzi wa
  Hospitali za Rufaa za Kanda na za Mikoa, zahanati, vituo vya
  afya na hospitali za Halmashauri za Wilaya; kuimarisha
  upatikanaji wa chanjo, dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi
  kwa kuongeza bajeti, kutoa fedha na kuimarisha udhibiti;
  kuimarisha huduma za ustawi na maendeleo ya jamii, hususan
  haki za wazee, watoto na makundi maalumu; na kuendelea na
  hatua za uteelezaji wa ahadi ya utoaji wa bima za afya kwa
  wote;
  Kwa upande wa eneo la maji safi na usafi wa mazingira miradi
  itakayotekelezwa ni pamoja na: kuimarisha huduma za maji na
  usafi wa mazingira vijijini; ujenzi, ukarabati na upanuzi wa
  miradi ya maji katika miji mikuu ya mikoa, wilaya, miji midogo
  na miradi ya kitaifa; ujenzi wa bwawa la Farkwa kwa ajili ya
  kuimarisha huduma ya maji katika jiji la Dodoma; bwawa la
  Kidunda kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa maji jijini Dar es
  Salaam; na kutekeleza mradi wa kimkakati wa kutoa maji
  kutoka ziwa Victoria hadi jijini Dodoma.
  Kwa upande wa eneo la ardhi, miradi itakayotekelezwa ni
  pamoja na: kuendelea kupanga, kupima na kumilikisha ardhi
  nchi nzima; kuimarisha mipaka ya kimataifa; kuimarisha
  miundombinu ya upimaji na ramani; na kuendeleza upangaji
  wa matumizi ya ardhi nchini ili kuondoa migogoro katika
  37
  matumizi ya ardhi.
  (e) Kuendeleza Rasilimali Watu: Kuendelea na utekelezaji wa
  programu na miradi mbalimbali ya kukuza ujuzi nchini ili
  kuongeza ajira kwa vijana kwa kutoa mafunzo ya ufundi na
  stadi za kazi kupitia programu mbalimbali zikiwemo:
  kuimarisha programu ya taifa ya kukuza ujuzi nchini; kuboresha
  mfuko wa maendeleo ya vijana; kuendelea na ujenzi na
  ukarabati wa vituo vya ufundi kwa watu wenye ulemavu; na
  kutekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Kazi za Staha.
 9. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu miradi ya
  kipaumbele kwa mwaka 2022/23 yanapatikana katika Kitabu cha
  Mpango, Sura ya Nne.
  Vihatarishi vya Utekelezaji wa Mpango wa Mwaka 2022/23
 10. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango unaweza
  kuathiriwa na vihatarishi vya ndani na nje. Vihatarishi vya ndani ni
  pamoja na: ufinyu wa rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia
  utekelezaji wa miradi ya maendeleo; ushiriki mdogo wa sekta binafsi
  katika mipango ya maendeleo; uharibifu wa mazingira na mabadiliko
  ya tabianchi; na uhalifu wa kimtandao na rushwa. Vihatarishi vya nje
  ni pamoja na: majanga ya asili na magonjwa ya mlipuko; mitikisiko
  ya kiuchumi duniani; kubadilika kwa teknolojia; na kutopatikana kwa
  misaada na mikopo kwa wakati.
 11. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na vihatarishi vya
  utekelezaji wa Mpango, Serikali itachukua hatua mbalimbali
  ikijumuisha: Kuimarisha ukusanyaji na usimamizi wa kodi kwa
  kuhakikisha wafanyabiashara wanatoa risiti za kielektroniki
  wanapouza bidhaa na wanunuzi kudai risiti wanaponunua bidhaa;
  kuhamasisha ulipaji kodi katika sekta isiyo rasmi kwa kuijumuisha
  38
  kwenye mfumo rasmi wa ulipaji kodi; kuendelea kuimarisha na
  kuhamasisha wananchi kuhusu uelewa wa huduma za sekta ya fedha
  ikiwemo utoaji wa mikopo, uwekezaji, mitaji na bima; kuendelea
  kuweka mazingira ya kuvutia uwekezaji wa sekta Binafsi wa ndani na
  nje ili kupunguza gharama za uwekezaji; kusimamia miongozo na
  kanuni za usimamizi wa mazingira; kuendelea kuimarisha
  mapambano dhidi ya rushwa ikijumuisha kuchukua hatua za kisheria
  kwa wanaobainika kuhusika na vitendo vya rushwa; kuboresha
  mifumo ya kuzuia na kukabiliana na majanga; na kuweka mazingira
  wezeshi kwa wawekezaji hususan viwanda vinavyozalisha bidhaa kwa
  kutumia teknolojia na malighafi za ndani ili kupunguza uagizaji wa
  bidhaa kutoka nje.
  Ugharamiaji wa Mpango 2022/23
 12. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2022/23, inakadiriwa kuwa
  jumla ya shilingi bilioni 15,004.8 sawa na asilimia 36.2 ya Bajeti yote
  ya Serikali zitatumika kugharamia miradi ya maendeleo ikijumuisha
  miradi ya huduma za jamii. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni
  12,305.8 sawa na asilimia 82.0 ya bajeti ya maendeleo ni fedha za
  ndani na shilingi bilioni 2,699.1 sawa na asilimia 18.0 ya bajeti ya
  maendeleo ni fedha za nje. Katika kuongeza ushiriki wa sekta binafsi
  kama injini muhimu ya utekelezaji wa miradi, Serikali itahakikisha
  miradi yote inayovutia uwekezaji wa sekta binafsi inatekelezwa kwa
  utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) na
  Joint Venture kwa kutumia utaratibu wa Kampuni Maalumu (Special
  Purpose Vehicle).
 13. Mheshimiwa Spika, katika kuongeza ukusanyaji wa mapato
  ya kugharamia Mpango, Serikali itaendelea kuweka mikakati ya
  kusimamia ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kutoka
  vyanzo mbalimbali vya ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali
  zikiwemo: Kuimarisha ukusanyaji na usimamizi wa kodi kwa
  39
  kuhakikisha wafanyabiashara wanatoa risiti za kielektroniki
  wanapouza bidhaa na wanunuzi kuchukua risiti wanaponunua
  bidhaa; kuendelea kutoa elimu kwa mlipakodi kupitia runinga, redio,
  mitandao ya kijamii na semina; kupanua wigo wa kodi kwa
  kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara katika mfumo rasmi wa
  ulipaji kodi kupitia kampeni ya Mlango kwa Mlango; kuendelea
  kutumia Mpango wa Usimamizi wa Viashiria Hatarishi (Compliance
  Risk Management Plan) ili kubaini na kutambua wakwepaji wa kodi;
  kuendelea kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa mipaka yote kwa
  kuongeza ushirikiano baina ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na
  vyombo vya ulinzi na usalama nchini ili kudhibiti bidhaa za magendo
  na kupunguza tatizo la ukwepaji wa kodi; na kuimarisha mazingira
  rafiki ya ulipaji kodi kwa hiari kwa kuboresha na kuhimiza matumizi
  sahihi ya mifumo ya TEHAMA ikiwa ni pamoja na kuboresha mifumo
  itakayosaidia na kurahisisha ulipaji kodi.
 14. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha Mfumo wa
  Kielektroniki wa Kufuatilia Mizigo inayokwenda nchi jirani (Eletronic
  Cargo Tracking System) ili kuimarisha uwezo wa usimamizi wa mizigo
  inayopita kwenda nchi jirani; kuhamasisha ulipaji kodi katika sekta
  isiyo rasmi kwa kuijumuisha kwenye mfumo rasmi wa ulipaji kodi;
  kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji
  wapya, kukuza biashara ndogo na za kati kwa ukuaji endelevu wa
  uchumi utakaowezesha kuongeza wigo wa kodi pamoja na
  kuendelea kusimamia Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa
  Ukusanyaji wa Mapato (Government Electronic Payment Gateway –
  GePG) ili kurahisisha ulipaji na kudhibiti upotevu wa mapato.
 15. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha
  mashirikiano na Washirika wa Maendeleo kwa kutekeleza Mwongozo
  wa Ushirikiano wa Maendeleo (Development Cooperation Framework
 • DCF) ili kuhakikisha kuwa fedha kutoka kwa Washirika wa
  Maendeleo zinaendelea kupatikana kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji
  40
  wa miradi na programu mbalimbali nchini. Aidha, Serikali kwa
  kushirikiana na washirika wa Maendeleo imeanza maandalizi ya
  kufanya tathmini na mapitio ya Mwongozo wa Ushirikiano
  itakayoiwezesha nchi kujipanga kimkakati ili kunufaika zaidi na fursa
  zilizopo kwa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Serikali, Sekta
  binafsi na Asasi Zisizo za Kiserikali katika masuala ya ushirikiano wa
  kimataifa.
  Vile vile, kwa kutambua uwepo wa pengo la rasilimali fedha
  zinazohitajika katika kufikia shabaha ya maendeleo ya Taifa, Serikali
  imeainisha vyanzo mbadala na bunifu vitakavyotumika kugharamia
  miradi ya maendeleo na hivyo kupunguza mzigo kwa bajeti ya
  Serikali. Vyanzo hivyo ni utekelezaji wa Mkakati wa Ugharamiaji wa
  Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano sanjari na
  Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa mwaka 2020/21-
  2029/30. Katika kufikia azma hiyo, Serikali itafanya maboresho ya
  sheria mbalimbali pamoja na kuweka miongozo itakayowezesha
  kunufaika na vyanzo mbadala na bunifu katika utekelezaji wa
  shughuli za maendeleo.
 1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ugharamiaji wa miradi
  ya maendeleo itakayotekelezwa kwa utaratibu wa Ubia baina ya
  Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Serikali imepanga kuwezesha
  Mamlaka za Serikali zenye miradi ya PPP iliyopo katika hatua
  mbalimbali za maandalizi ikiwemo Upembuzi Yakinifu na Ununuzi wa
  wabia kukamilisha miradi hiyo iweze kuanza utekelezaji. Katika
  mwaka 2022/23, Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta Binafsi
  katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa utaratibu
  wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP). Baadhi
  masuala yatakayotekelezwa ni pamoja na kuendelea kutafuta wabia
  wa miradi mitano (5) iliyofikia katika hatua za ununuzi (procurement
  stage) kwa kuitangaza katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Miradi
  hiyo ni: ujenzi wa viwanda vya dawa muhimu (Kibaha), vifaa tiba
  41
  vitokanavyo na pamba (Mwanza) na maji tiba (Mbeya); uendeshaji
  wa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es
  Salaam awamu ya kwanza; ujenzi wa hoteli ya nyota nne katika
  Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere; ujenzi wa kituo
  changamani cha biashara (commercial Complex) katika Kiwanja cha
  Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere; na ujenzi wa kiwanda cha
  kutengeneza simu za mkononi chini ya Mamlaka ya Mawasiliano
  Tanzania (TCRA) katika Mkoa wa Mwanza.
  Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji wa Taarifa za Utekelezaji
 2. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa mipango ya
  maendeleo inatekelezwa kama ilivyokusudiwa, suala la ufuatiliaji,
  tathmini na utoaji wa taarifa za utekelezaji limeendelea kupewa
  msukumo wa pekee katika shughuli za kila siku za Serikali. Katika
  kutekeleza hilo, mwaka 2021/22, Wizara ya Fedha na Mipango
  ilifanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi 225 katika sekta za Uchukuzi,
  Viwanda, Elimu, Afya, Ujenzi, Utawala Bora, Kilimo, Mifugo, Maji na
  Biashara inayotekelezwa na Serikali pamoja na Sekta Binafsi. Katika
  mwaka 2022/23, Serikali itaendelea kutumia mbinu na viashiria
  vilivyoainishwa katika Mkakati wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mpango
  wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 –
  2025/26 pamoja na Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini
  ya Miradi na Programu za Maendeleo kupima utekelezaji wa Mpango
  wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano na miradi ya maendeleo na
  kuchukua hatua za kutatua changamoto zitakazobainika katika
  utekelezaji. Vile vile, Serikali itaendelea kuzingatia miongozo
  mbalimbali ya ufuatiliaji na tathmini ya Mpango ikiwemo Sheria ya
  Ununuzi wa Umma, SURA 410, Sheria ya Bajeti, SURA 439 na Sheria
  ya Fedha za Umma, SURA 348. Pamoja na Sheria hizo, Serikali pia
  imeanza maandalizi ya Sera ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ili
  kutatua changamoto za uratibu wa shughuli za ufuatiliaji na tathmini
  Serikalini.
  42
 3. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha uwepo wa
  ushirikishwaji wa kutosha katika masuala ya ufuatiliaji na tathmini,
  Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kushirikiana
  na Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na
  Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za
  Mitaa pamoja na Sekta Binafsi katika kuratibu na kusimamia
  ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango.
 4. Mheshimiwa Spika, Serikali inazielekeza Wizara, Idara
  Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma,
  Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutafsiri
  malengo na viashiria vya utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa
  Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 katika
  Mipango na Bajeti za kisekta kwa mwaka 2022/23. Aidha, Wizara,
  Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya
  Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa
  zinaelekezwa kuzingatia maelekezo yaliyoainishwa katika Mwongozo
  wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi na Programu za
  Maendeleo wa Mwaka 2022 ikiwa ni pamoja na: kuandaa Mpango
  Kazi wa mwaka wa ufuatiliaji na tathmini, kutenga rasilimali fedha
  zitakazowezesha shughuli za ufuatiliaji na tathmini; kuimarisha
  mifumo ya ndani ya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo;
  kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo kwa
  kuzingatia mipango kazi iliyowekwa; kuendelea kuwajengea uwezo
  watumishi katika tasnia ya ufuatiliaji na tathmini; na kuwa na mfumo
  mmoja wa kielektroniki unaoratibu taarifa za utekelezaji, ufuatiliaji na
  tathmini katika kutekeleza mipango ya maendeleo.
 5. Mheshimiwa Spika, Serikali inazielekeza Wizara, Idara
  Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma,
  Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuaandaa
  43
  taarifa za ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi na programu
  za maendeleo na kuziwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango. Ofisi ya
  Rais – TAMISEMI itaratibu ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya
  maendeleo inayotekelezwa katika ngazi za Sekretarieti za Mikoa na
  Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuwasilisha taarifa husika Wizara ya
  Fedha na Mipango.
  MAJUMUISHO
 6. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, Mpango
  wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23 ni wa pili katika
  utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka
  Mitano 2021/22 – 2025/26 wenye dhima ya “Kujenga Uchumi
  Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”. Utekelezaji wa
  Mpango utaendelea kuimarisha viashiria vya uchumi jumla,
  kuboresha mazingira ya uwekezaji viwandani ikiwemo kuimarisha
  majadiliano na wawekezaji wa ndani na nje, kuimarisha mahusiano
  ya kisiasa, ulinzi na diplomasia ya uchumi na nchi nyingine,
  kuendelea kutekeleza kwa kasi miradi ya maendeleo, kuendeleza
  mashirikiano na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya
  maendeleo pamoja na kuchochea uwekezaji viwandani hususan kwa
  kutumia rasilimali watu na malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini
  ikiwemo mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, madini, misitu na gesi
  asilia.
 7. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na jitihada za
  kukabiliana na athari za majanga mbalimbali ya asili na yasiyo ya asili
  yakiwemo magonjwa, vita na mabadiliko ya tabianchi. Mathalani,
  tutaendelea kuimarisha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa
  Kukabiliana na Athari za UVIKO–19 pamoja na kuweka mipango
  madhubuti ya kupunguza athari zitokanazo na vita inayoendelea kati
  ya Urusi na Ukraine ikiwemo kudhibiti ongezeko la bei za bidhaa
  mbalimbali na kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi.
  44
 8. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji
  na utoaji wa huduma bora kwa wananchi zikiwemo huduma za afya,
  elimu, umeme na maji safi na salama mijini na vijijini, kuongeza kasi
  ya utekelezaji wa miradi ya kielelezo na ya kimkakati, kuimarisha
  miundombinu wezeshi ya uwekezaji na biashara kwa ajili ya masoko
  ya kimataifa hususan ya nchi jirani, kuimarisha sekta za uzalishaji ili
  kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi, kufungua fursa zaidi za
  ajira na maendeleo ya watu.
  HITIMISHO
 9. Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali ninaomba kutumia
  fursa hii kuwashukuru wadau wote wa maendeleo wakiwemo
  Waheshimiwa Wabunge, Sekta Binafsi, Taasisi za Elimu na Tafiti,
  Asasi za Kiraia, Taasisi za Dini, Washirika wa Maendeleo na Wananchi
  wote kwa namna walivyojitoa na kushiriki kikamilifu katika hatua
  mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuimarisha
  uchumi wa Taifa letu. Wadau hao wamekuwa na mchango mkubwa
  katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo. Kwa msingi
  huo, ninawaomba na kuwasihi wadau wote waendelee kushirikiana
  na Serikali yetu inayoongozwa na Rais shupavu, Mheshimiwa Samia
  Suluhu Hassan.
 10. Mheshimiwa Spika, hotuba hii isingeweza kukamilika bila
  jitihada kubwa zilizofanywa na watumishi wote wa Wizara ya Fedha
  na Mipango. Hivyo, kwa dhati ya nafsi yangu naomba nitoe shukrani
  za pekee kwa Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), Naibu Waziri wa
  Fedha na Mipango, Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa
  Wizara zote, Viongozi wote wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za
  Serikali za Mitaa, Wakuu wa Idara Zinazojitegemea, Wakala za
  Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma kwa ushirikiano wao katika
  maandalizi ya taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2021
  45
  na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23. Aidha,
  ninawashukuru watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango
  wakiongozwa na Katibu Mkuu Bw. Emmanuel Mpawe Tutuba kwa
  kujitoa usiku na mchana kukamilisha kwa wakati na kwa ubora
  Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa
  Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23.
 11. Mheshimiwa Spika, mwisho lakini si kwa umuhimu, napenda
  kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote kwa ujumla
  kwa kutenga muda wao kunisikiliza. Aidha, napenda kuwataarifu
  wadau wote kuwa, hotuba hii pamoja na vitabu vya Taarifa ya Hali
  ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa
  Taifa wa Mwaka 2022/23 vinapatikana katika tovuti ya Wizara ya
  Fedha na Mipango ambayo ni www.mof.go.tz.
 12. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa
  Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi wa
  Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
  Mwaka 2022/23.
 13. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *