DKT. KIRUSWA AAHIDI KUHARAKISHWA MCHAKATO WA UPATIKANAJI WA LESENI YA UCHIMBAJI MADINI YA MCHANGA WA BAHARINI

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ametoa ahidi kwa Kampuni ya Nyati Mineral Sands Limited ya kuharakishwa kwa mchakato wa upatikanaji wa Leseni ya Uchimbaji Mkubwa wa Madini ya Mchanga wa Baharini.

Dkt. Kiruswa ameyasema hayo leo Juni 14, 2022 baada ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa kampuni hiyo yenye ubia kati ya Kampuni ya Strandline Resources Limited kwa hisa za asilimia 84 na Serikali kwa hisa ya asilimia 16.

Disemba 13 ,2021 Kampuni ya Strandline Resources Limited yenye makazi yake nchini Australia iliingia ubia na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupelekea kuundwa kwa Kampuni moja ya Nyati Mineral Sands Limited ambayo ipo kwenye hatua za mwisho za upatikanaji wa Leseni ya Uchimbaji Mkubwa wa Madini ya Mchanga wa Baharini ambapo watachimba katika eneo la Pangani Tanga na Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Aidha, Dkt. Kiruswa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anataka kuona wawekezaji wanaandaliwa mazingira wezeshi na rafiki kwa ajili ya uwekezaji ili pande zote mbili zinufaike yani mwekezaji na serikali.

“Sisi kama wizara tutajitahidi tuone jinsi gani tutaweza kusaidia ili mchakato wa upatikanaji wa leseni kubwa ya uchimbaji wa Madini ya Mchanga wa Baharini kupatikana kwa wakati,” amesema Dkt. Kiruswa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Nyati Mineral Sands Limited anayeiwakilisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhandisi Heri Gombera amesema kuanzishwa kwa mgodi huo, kutawezesha kupatikana kwa ajira kwa watanzania na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *