WAZIRI BASHE KUWACHUKULIA HATUA KALI WASIOKATA VIBALI

Serikali imesema itawachukulia hatua ikiwemo kutaifisha mali kwa wafanyabiashara wa mazao wanaosafirisha kwenda nje ya nchi ambao hawajakata vibali vinavyotolewa na Wizara ya Kilimo bila malipo yoyote.
Waziri wa Kilimo HUSSEIN BASHE amesema, licha ya Serikali kuwataka wasafirishaji wa bidhaa za mazao kwenda nje kukata vibali vya usafirishaji mazao hayo, baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wameendelea kutumia njia za panya kufanya shughuli hiyo.
Akizungumza Jijini Dodoma BASHE amesema, licha ya kuwataka wafanyabiashara hao kufuata taratibu wamekuwa wakiendelea na utaratibu huo jambo ambalo limesababisha malori zaidi ya arobaini kukwama mpakani kwa kukosa vibali hivyo.
Amesema kwa kuwa lengo la Serikali ni kuona wakulima wakinufaika na nguvu kazi zao wataruhusu magari hayo kwa mara ya mwisho na jambo hilo halitaruhusiwa tena.
“Tunatoa vibali vya usafirishaji mazao kwenda nje ya nchi bila gharama yoyote, lakini hii ni mara ya pili wasafirishaji hawa wanaenda hadi mpakani bila vibali na hivyo kusababisha msururu wa magari usio na tija yoyote,” alisema Bashe.
Akibainisha zaidi Waziri huyo wa Kilimo amesema, kwa sasa wataruhusu magari hayo kupita, ila hii itakuwa kwa mara ya mwisho na mfanyabiashara yeyote atakayerudia kitendo hicho cha ukiukwaji wa sheria magari na mazao yao yatakamatwa na kutaifishwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *