MTANZANIA AMTWANGA MJERUMANI KWA TKO

Bondia Mtanzania anayeishi nchini Sweden Awadhi Tamim amemtwanga Bondia Shkelqim Ademaj wa Ujerumani kwa TKO katika pambano la raundi 10 lililofanyika Essen nchini Ujerumani.

Awadh Tamim ameshinda taji lililokuwa wazi la World Boxing Foundation (WBF International) mapema usiku wa kuamkia Jumapili ya tarehe 12 Juni 2022 mjini Essen Ujerumani, kwa kumpiga Shkelqim Ademaj kwa Technical Knock Out katika raundi ya kumi ambapo mpinzani wake alishindwa kuendelea na pambano hilo. Awadhi Tamim alianza kwa kumlambisha sakafu Ademaj katika raundi ya sita lakini baadae aliamka na kuruhusiwa kuendelea na pambano. Tamim aliongoza kwa pointi wakati wote wa pambano hilo hadi lilipovunjwa kutokana na Ademaj kushindwa kuendelea. Awadhi Tamim anasema huu ni ushindi muhimu zaidi kwake.

Hivi Karibuni Bondia huyo alikutana na kuzungumza na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango alipokuwa ziarani nchini Sweden ambapo alimueleza juhudi zake katika kuitangaza Tanzania kupitia mchezo huo wa masumbwi pia alimuahidi kuiwakilisha vema Tanzania katika pambano hilo la uzito wa juu lililofanyika Ujerumani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *