OR-TAMISEMI yatoa siku 20 kwa Waganga Wakuu wa mikoa.

NA OR-TAMISEMI.

NAIBU Katibu Mkuu (Afya) Ofisi ya Rais-Talawa za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt.Grace Magembe amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa kuhakikisha ujenzi wa miundombinu unaotekelezwa katika vituo vya kutolea huduma za afya uwe umekamilika ifikapo Juni 30,2022 huku ubora ukiwa umezingatiwa.

Dkt. Magembe amebainisha kuwa, bado usimamizi na ufuatiliaji katika baadhi ya mikoa na halmashauri unasuasua, hivyo Sekretarieti za Mikoa zina wajibu wa kusimamia utekelezaji huo na kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.

Pia amewataka kushirikiana na Waganga Wakuu wa Halmashauri katika kuhakikisha ujenzi huo unakamilika sio zaidi ya tarehe 30 Juni, 2022.

Dkt. Grace ametoa rai hiyo Juni 10,2022 katika Kikao kazi cha Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Waganga Wakuu wa Mikoa pamoja na Makatibu Afya wa Mikoa jijini Dodoma.

Amesema, ni muhimu sana kuimarisha usimamizi katika utekelezaji huo kwa kuwa Serikali inatarajia kusambambaza vifaa tiba vitakavyotumika katika majengo hayo ambayo asilimia kubwa bado yapo katika hatua ya utekelezaji.

Dkt. Grace amesema, anatarjia vifaa hivyo vitakapofika majengo hayo yawe yamekamilika tayari kwa kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

“Tunatarajia kuanza kusambaza vifaa katika vituo ambavyo vinajengwa ni muhimu sana mkasimamie hii miradi imalizike kwa wakati ili sasa vifaa vitapokuja vikute tayari ujenzi umekamilika sio vifaa vinaletwa vinakaa nje kusubiri majengo yaishe hatutakubali vifaa viharibiwe,”amesema Dkt.Grace.

Kwa upande mwingine, Dkt. Magembe amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa kuziandikia barua halmashauri ambazo zilifanya mabadiliko ya miradi au matumizi ya fedha ya ujenzi wa miundombinu ya Afya bila kutoa taarifa katika ngazi ya Mikoa ziwasilishe sababu ya kufanya mabadiliko hayo ili OR-TAMISEMI iwe na taarifa kamili ya mabadiliko, lakini pia kuondoa hoja za ukaguzi.

Aidha, amewataka Waganga Wakuu na Makatibu Afya wa Mikoa kuhakikisha wanafanya usimamizi shirikishi katika mikoa yao hususan katika ukaguzi wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba pamoja na kusimamia utolewaji wa huduma bora katika kila kituo cha kutolea huduma za Afya zoezi litakalopelekea kuboreshaji wa huduma za Afya katika maeneo yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *