SERIKALI YATANGAZA NEEMA KWA WAKULIMA WA ZABIBU MKOANI DODOMA KWA KUJENGA VITUO VITATU VYA UCHAKATAJI ZABIBU

Serikali kwa kupitia Wizara ya Kilimo imepanga kujenga vituo vitatu (Storage Facilities) vya kukusanya,kuchakata na kuhifadhi mvinyo ghafi wa zabibu mkoani Dodoma kwa lengo la kuokoa zabibu za wakulima zinazooza shambani kwa kukosa masoko kwa wakati.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde leo 10/06/2022 alipofungua kikao cha wadau wa zao la zabibu kilichofanyika katika ukumbi wa PSSSF Jijini Dodoma
Mhe. Mavunde amesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili wakulima wa zabibu ni kukosekana kwa soko la uhakika jambo ambalo hupelekea mkulima kuuza zabibu zake kwa bei ya hasara.

Vilevile, Mhe. Mavunde amewahakikishia wakulima wa zabibu kuwa wataweza kuuza mvinyo ghafi kwa utulivu baada ya kupatikana kwa vituo hivyo vya uhifadhi na yeye kama Naibu Waziri wa Kilimo atawasaidia kutafuta masoko ya mvinyo ghafi katika nchi mbalimbali za nje zikiwemo Burundi na Brazil.

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya imedhamiria kuwainua wakulima wakiwemo wa zabibu hivyo waendelee kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amekipa Kilimo kipaumbele cha juu.
Amefafanua kuwa katika kuhakikisha wakulima wa zabibu wanazalisha kwa tija na weledi serikali itapeleka wataalam na wakulima katika nchi zinazofanya vizuri kwenye kilimo cha zabibu ili wakulima watakaopata fursa ya kujifunza wakasaidie kufundisha wakulima wengine.

“Tutapeleka wataalam na wakulima kwenye nchi za Ufaransa, Italy na Afrika ya Kusini ili wakulima watakaopata elimu wasaidiae na maafisa ugani kutoa elimu kwa wakulima wengine”. Amesema Mhe. Mavunde.
Aidha Mhe. Mavunde amewataka wadau wa zabibu kujadili kwa uwazi muongozo wa uzalishaji,masoko na uchakataji wa zabibu ili yapatikane mawazo yenye nia ya kujenga na hatimaye kuleta maendeleo kwenye zao hilo.

Awali akitoa salamu za mkoa wa Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Mwanahamisi Mukunda amesema ana imani kubwa na uwezo wa Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe pamoja Naibu Waziri Mhe. Anthony Mavunde.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *