
Na; Mwandishi wetu – Mvomero
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa, amewaasa wakulima nchini kutunza vyanzo vya maji kwa kutokufanya shughuli za kibinadamu hususan za kilimo ndani ya mita sitini (60) ili kunusuru kuharibika kwa kingo za mito unaopelekea uharibifu wa Miundombinu ya kilimo cha Umwagiliaji.
Bw. Mndolwa ameyasema hayo mapema jana alipokuwa akizungumza na wakulima wa skimu ya Umwagiliaji Msufini iliyopo Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro, inayotumia maji kutoka mto Mvomero kama chanzo cha maji ya kilimo cha Umwagiliaji, ambapo ameshuhudia uharibifu mkubwa uliofanyika kutokana na shughuli za kilimo sisizo rasmi.

Aliwashauri viongozi wa Serikali ya kijiji kushirikiana kulinda vyanzo hivyo vya maji kwa manufaa ya kila mwananchi na aliendelea kusema “Hatulindi vyanzo vya maji ya kunywa tuu, hata vya kilimo na kuzuia uharibifu unaofanywa na binadamu wenzetu, asili inaharibiwa na binadamu.”Alisisitiza
Bw. Mndolwa aliagiza wataalam kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wataalam kutoka Halmashauri kufanya mapitio ya mto na chanzo na kuona athari iliyotokana na mafuriko yaliyopita katika mto huu. Katika zoezi hilo wataalam watatakiwa kuja na mapendekezo ya nini kifanyike ili kurekebisha athari za mafuriko hali itakayopelekea skimu ya Msufini kuanza kufanya kazi.
Aliongeza kuwa, kitachaofanyika kwa sasa ni kutengeneza chanzo kinachopeleka maji katika skimu hiyo matengenezo ambayo yataridhisha pande zote ikiwa ni pamoja na serikali na watumiaji wa skimu hiyo.
“siwezi ruhusu mkandarasi aliyefanya kazi kwa kiwango cha chini upande mwingine aje tena hapa, sababu kuna mahali kaharibu na nitamfukuza, kama kaharibu kwingine na hapa ataharibu.”Alibainisha Mndolwa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Miundombinu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mhandisi Ntonda Kimasa alisema, kuwa mradi huo umetengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya kuboresha miundombinu yake, hivyo mara baada ya kukamilika mapendekezo ya timu kazi ya ukarabati wa miundombinu itaanza mara moja.

Awali, Bw. Mndolwa aliwakumbusha wakulima swala zima za kulipa Tozo na ada za matunzo ya skimu za Umwagiliaji baada ya kujengewa na kukarabatiwa kwa miundombinu hiyo.
Kwa upande mwingine aliwashauri wadau husika akitolea mfano wadau wa barabara, kilimo na wadau wengine wakae kwa pamoja ili yafanyike maamuzi sahihi na kuona namna ya kuunusuru mto mvomero kutokuacha njia yake ya asili na kupelekea kuvamia makazi ya watu.
Skimu ya kilimo cha Umwagiliaji Msufini, iliyopo Wilayani Mvumero Mkoani Morogoro pamoja na kuathiriwa na athari zitokanazo na mabadiliko ya Tabianchi, imeharibiwa vibaya na shughuli za kibinadamu zinazofanyika ndani ya mita sitini, bila kuzingatia sheria.