WAZIRI MKUU MAJALIWA AAGIZA USHIRIKIANO UTUNZAJI MAZINGIRA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa amesema kuwa kutokana na kuongezeka kwa uharibifu wa Mazingira, aagiza Wizara na Taasisi husika, pamoja na wananchi kwa ujumla, kuimarisha ushirikiano katika kukomesha uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu kote nchini.

Waziri Majaliwa, ameyasema hayo leo jijini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani yanayoadhimishwa Juni 5 ya Kila mwaka yakienda sambamba na kaulimbiu isemayo “Tanzania Moja tu, Tunza Mazingira” amesema Majaliwa. 

“Halmashauri za Miji, Serikali za vijiji na mitaa kote nchini wekeni mikakati ya kukomesha uchomaji moto ovyo. Nawasihi tutoe ushirikiano wa kutosha katika kuhakikisha tunarejesha misitu, ikolojia na uoto wa asili katika maeneo yenu, hususan maeneo ambayo miti ya asili iko kwenye tishio la kutoweka” alisema.

Aidha, amesema kutokana na mwenendo wa hali ya mazingira nchini ipo haja ya kuimarisha mipango na mikakati ya utekelezaji wa uhifadhi na usimamizi wa mazingira ambayo ni vema ikawa shirikishi ikijumuisha ufuatiliaji, usimamizi thabiti na kufanya tathmini ya mara kwa mara ya hali ya mazingira nchini. 

“Uhifadhi wa mazingira ni suala endelevu, linalopaswa kuwa shirikishi na kufanywa kila siku. Hivyo, basi, ni matarajio yangu kuwa, wakati wote shughuli za uhifadhi na usimamizi wa mazingira zitaendelea kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku.” amesisitiza Majaliwa. 

Katika hatua nyingine, Waziri Majaliwa ameitaka Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha Mpango Kabambe wa Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira unakuwa sehemu ya vipaumbele vya bajeti vya kila mwaka kwa kipindi chote cha utekelezaji wake wa miaka kumi (10). 

“Wizara za kisekta, Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira unajumuhishwa katika mipango na Bajeti zao, sambamba na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji Ofisi ya Makamu wa Rais” ameongeza Majaliwa. 

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Seleman Jafo amesema wameendelea kusimamia na kutaratibu ya ajenda ya mazingira ili kuhakikisha nchi inafanya vizuri katika utunzaji wa Mazingira.

“Nchi imeendelea kupanda miti ikienda sambamba na program ya mazingira. Tuna tekeleza ajenda ya upandaji miti Kwa lengo la kuilinda Tanzania. Tuyatunze Mazingira jukumu letu ni kuhakikisha kazi ya Mazingira inakwenda mbele” amesema Dkt. Jafo. 

Kwa upande wa Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Zlatan Milisic, amesema familia ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuunga mkono jitihada zinazohimiza utunzaji wa mazingira na teknolojia endelevu ambazo ni rafiki zaidi kwa mazingira. 

“Tutaendelea pia kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya mipango mikakati, sera na mikakati ya kitaifa ya mazingira na tabianchi.” amesema Zlatan. 

Hatahivyo, katika Maadhimisho hayo umezinduliwa Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira pamoja na kutoa tuzo kwa Mabalozi wa Mazingira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *