WAZIRI MKUU AKEMEA UTIRIRISHAJI MAJI MACHAFU, ATOA MAAGIZO 15

WAZIRI MKUU AKEMEA UTIRIRISHAJI MAJI MACHAFU
Atoa maagizo 15 ya uhifadhi wa mazingira nchini

Ataka Mpango Kabambe wa Mazingira utengewe bajeti
 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea tabia ya utiririshaji wa maji machafu na majitaka kutoka viwandani na kwenye migodi kwani inachangia kuhatarisha usalama wa afya ya binadamu na mazingira.
 
“Hivi karibuni tumeshuhudia kutoweka kwa baadhi ya viumbe hai, maeneo mengi ya vyanzo vya maji yameathirika kutokana na ukame wa mara kwa mara, uchafuzi wa mazingira unaotokana na majitaka na kemikali kutoka na shughuli za viwandani.  Uchafuzi huu umeendelea kuongezeka kwa kasi nchini na kuathari maji, hewa na ardhi. Hali hii inahatarisha usalama wa afya ya binadamu na mazingira,” amesema.
 
Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo (Jumapili, Juni 5, 2022) wakati akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kitaifa yamefanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. Kaulimbiu yake ni Tanzania ni moja tu, Tunza Mazingira.
 
Vilevile, amekemea tabia ya uchomaji miti, uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu, ukataji wa miti holela kwa ajili ya uchomaji wa mkaa, uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji pamoja na uchomaji moto misitu.
 
“Kutokana na kuongezeka kwa uharibifu wa mazingira, ninaagiza Wizara na taasisi husika, pamoja na wananchi kwa ujumla, kuimarisha ushirikiano katika kukomesha uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu kote nchini. Ninawasihi wananchi tutoe ushirikiano wa kutosha kuhakikisha tunarejesha misitu, ikolojia na uoto wa asili katika maeneo yetu, hususan maeneo ambayo miti ya asili iko kwenye tishio la kutoweka. Tuwe walinzi wazuri wa mazingira kwa faida ya kizazi hiki na kijacho,” amesisitiza.
 
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ametoa maagizo 15 kwa wizara, taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu uhifadhi wa mazingira nchini na kutaka yatekelezwe kikamilifu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *