
WAZIRI wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe leo Juni 3, ameiagiza Bodi ya Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kuanza mchakato Kutafuta mzabuni atakayejenga mfumo thabiti wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji katika shamba la ASA lililopo Ngaramtoni jijini Arusha.
Mhe. Bashe ametoa agizo hilo wakati alipotembelea shamba hilo la uzalishaji wa mbegu za arizeti, ngano na soya alilolikuta likiwa halina uzio na wala hakuna miundombinu ya umwagiliaji na huduma nyingine muhimu.
Aidha Mhe.Bashe amesema ili mashamba ya ASA yaendelee kuwa salama ni lazima yawe kwenye mfumo ambao unawazuia wananchi kuyavamia na kufanya shughuli mbalimbali za kibinadamu.

Amesisitiza kuwa ASA haitoweza kuzuia uvamizi wa wananchi kwenye mashamba yao kama wakishindwa kuyalinda ambapo alishauri kujengwa kwa nguzo za zege kisha kuunganishiwa senyenge kuzunguka mashamba yote ya ASA.
“Huwezi kumzuia mtu asivamie mashamba haya kama hujaweka uzio na tena mkubwa ambao unalenga kuimarisha usalama wa maeneo ya mashamba, hii itazuia hata wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba yenu ya kuzalisha mbegu” alisema Waziri Bashe.
Waziri Bashe amesema itakapofika Julai mosi mwaka huu anataka kuona wakandarasi waliopewa zabuni za ujenzi wa miradi ya umwagiliaji wameshaanza kazi na atakuwa akipita kukagua miradi hiyo na kuitaka Tume ya Umwagiliaji kusimamia kuanza kwa kandarasi za ujenzi.

