
ADO SHAIBU: TUMUENZI MAALIM SEIF KWA VITENDO.
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Ado Shaibu amewahimiza Wanachama wa ACT Wazalendo kumuenzi aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad kwa kutekeleza kwa vitendo misingi ambayo aliwaachia.
Ndugu Maalim Seif alifariki tarehe 17 Februari 2021.

“Leo tumefanya ziara ya kuwatembelea na kuwajulia hali Wazee na Wagonjwa kwenye Kata ya Tuangoma. Huu ni urithi aliotuachia kipenzi chetu Maalim Seif Sharif Hamad. Maalim alitufunza kuwa Chama ni familia. Ni lazima tuishi kwa upendo na kujaliana wenyewe na jamii yetu kwa ujumla “-Alisisitiza Ndugu Ado Shaibu.
Ndugu Ado Shaibu aliongeza kuwa Maalim Seif alikuwa kiongozi mwenye kuona mbali, mpenda haki na aliyetanguliza mbele maslahi ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
“Leo Vyama vyote vinazungumza umuhimu wa maridhiano na meza ya mazungumzo. Sisi ACT Wazalendo, mapema baada ya Uchaguzi Mkuu 2020, Maalim alituongoza kwenye meza ya mazungumzo na maridhiano ili kuhakikisha yale yaliyojitokeza kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020 hayajirudii tena. Tunafurahi kuwa licha ya changamoto, kebehi na dhihaka tuliyopitia wakati huo, Sasa kila mmoja anaona umuhimu wa kuliponya Taifa ili kufungua ukurasa mpya wa kisiasa Nchini”- Alisisitiza Ndugu Ado.


