OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Innocent Bashungwa ameagiza Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kuhakikisha ujenzi wa miundombinu hiyo inakamilika kwa asilimia 100 ifikapo Juni 30 mwaka huu.
“Maelekezo niliyoyatoa ya Juni 30 lazima tukamilishe ujenzi, Wakuu wa mikoa na maRAS wahakikishe wanasimamia maelekezo haya.”
Bashungwa ameyasema hayo wilayani Chemba mara baada ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuzungumza viongozi wa Wilaya hiyo.
Alisema kabla ya kufikia muda huo anatarajia kufanya kikao na wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ambao watatakiwa kutoa taarifa ya hatua walizofikiwa.
Ofisi ya Rais-TAMISEMI imepanga kufika Juni 30 mwaka huu, kukamilisha miradi ambayo ilikuwa ikitekelezwa kabla ya operesheni maalumu ya Covid 19 ikiwa ni ujenzi wa hospitali 68 zilizojengwa mwaka 2018/19, ujenzi wa hospitali mpya 28, kuendeleza hospitali 31, vituo vya afya vipya 354, kuendeleza vituo vya afya 52 na kukamilisha zahanati 763.
Aidha, Bashungwa alisema Rais Samia ametoa kibali cha ajira kwa watumishi na fedha kwa ajili ya vifaa tiba na kuwa kwa sasa Ofisi ya Rais-TAMISEMI iko katika hatua za mwisho za manunuzi.
” Kuhusu vifaa tiba, Rais Samia Suluhu Hassan ameshatupatia fedha na tuko katika hatua za mwisho za manunuzi, pia kibali cha kuajiri watumishi wa afya ambao ni wauguzi na madaktari. Hivyo Chemba jitahidini mkamilishe hospitali hii kwa asilimia 100, mkimaliza mtakuwa wa kwanza kuletewa vifaa tiba na watumishi.”
Naye Mkuu wa Mkoa, Anthony Mtaka alisema pamoja na Waziri kutoa muda wa hadi Juni 30, ni vyema uongozi wa Wilaya wakajiwekea muda wa hadi Juni 20 kukamilisha kazi hiyo.
Alisema ili kufikia muda huo waangalie namna ya kutekeleza mradi huo kwa kujenga usiku na mchana hususani kwa kazi ambazo hazina hathiri umaliziajia wa majengo.





