WIZARA YA MAJI YAINGIA MKATABA WA SH.BILIONI 1.4

Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) imeingia mkataba wa thamani ya Sh. bilioni 1.4 na Kampuni ya CityTaps ya Ufaransa wenye lengo la kukabiliana na changamoto ya upotevu wa maji katika eneo la Mwisenge lililopo Manispaa ya Musoma, mkoani Mara.

Akishuhudia utiaji saini wa mkataba huo uliofanyika makao makuu ya Wizara ya Maji jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Sanga amesema mkataba huo ni muendelezo wa hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara ya Maji kukabiliana na changamoto kubwa ya upotevu wa maji mijini na vijijini.

Mhandisi Sanga amesema kuwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) na Kampuni ya CityTaps ya Ufaransa waliandaa andiko linalohusu mkakati wa kupunguza kiwango cha upotevu wa maji kwa kutumia teknolojia mpya ya “Smart Meters” inayotumia mawimbi ya satelaiti kubaini mivujo ya maji ardhini lililopata kibali wizarani na kufanikiwa kupata ufadhili wa kiasi cha Shilingi 1,425,000,000 kutoka kwa Serikali ya Ufaransa.

“Lengo letu ni kukabiliana changamoto ya upotevu wa maji mijini na vijijini ili kiwango kikubwa cha maji yanayozalishwa kiwafikie wanufaika pamoja na kuwezesha mamlaka kupata makusanyo ya kutosha yatakayowawezesha kuboresha huduma na shughuli zake za uendeshaji”, Mhandisi Sanga amefafanua.

“Natarajia ufanisi na matokeo mazuri katika utekelezaji wa mradi huu, ambao utadhibiti kiwango cha upotevu wa maji lakini pia kubaini sababu zinazosababisha upotevu wa maji na kuja mkakati bora wa kukabiliana na changamoto hiyo katika maeneo mengine nchi nzima”, amesisitiza Mhandisi Sanga.

Aidha, Katibu Mkuu Sanga ametoa shukrani kwa Serikali ya Ufaransa kwa ushirikiano inayoutoa kwa Serikali ya Tanzania hususani kwenye Sekta ya Maji na kusema kuwa pamoja na mradi huo, Serikali ya Ufaransa imefadhili miradi mbalimbali katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera na Morogoro.

Mkataba huo umesainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), Mhandisi Nicas Mugisha na Meneja Biashara wa Kampuni ya CityTaps, Aurelie Guibert.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *