VIONGOZI NA WADAU WAANDAMIZI WA SKAUTI WAKUTANA NA WAZIRI MKENDA

Na Mathias Canal, WEST-Dar es salaam

Mkutano Mkuu wa SKAUTI umepangwa kufanyika tarehe 2 Julai 2022 Jijini Dodoma ukiwa na agenda kubwa ya uchaguzi Mkuu wa Viongozi wa kuendelea kuhudumu katika nafasi mbalimbali.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amyeyasema hayo tarehe 3 Juni 2022 Jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wa pamoja wa mashauriano wa Viongozi na wadau waandamizi wa Skauti nchini.

Mkutano huo kwa kauli moja umekubaliana kuundwa kamati ya pande zote mbili za muungano ili ili kuwa na mapendekezo yatakayoweza kuboresha uratibu na shughuli za Skauti ikiwa ni pamoja na kamati hiyo kutoa mapendekezo kwenye Bodi itakayochaguliwa kwenye uchaguzi mkuu baada ya Bodi iliyokuwepo kumaliza muda wake.

Waziri Mkenda ameeleza kuwa Bodi hiyo itakapochaguliwa itakuwa na jukumu la kushauri namna bora ya kuratibu na kuendesha shughuli za Skauti.

Kuhusu changamoto za kikatibu kuhusu Zanzibar kwenye uendeshaji wa Skauti, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amesema kuwa atashauriana na Waziri wa Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar.

Naye Waziri wa Elimu na mafunzo ya Amali Mhe Lela Mohamed Mussa amempongeza Waziri Mkenda kwa kupanga kikao hicho cha mashauriano ambacho kimetoa muelekeo.

Amewasihi wajumbe na wanachama wote wa SKAUTI Tanzania kujitayarisha kwa ajili ya mkutano huo wa uchaguzi.

AMesema kuwa miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na nafasi ya Zanzibar katika masuala ya SKAUTI.

Mhe Lela amewasihi wanachama wote kusimama imara na kuendeleza ukakamavu kwani SKAUTI ni chama chenye heshima kubwa na kioo cha jamii nchini kuwalea watoto kuanzia utotoni ili kuwa katika malezi bora ya uzalendo na uwajibikaji.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Ali Abdullgulam Hussen, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndg Ali Khamis Juma, Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Elimu, Saynsi na Teknolojia Dkt Lyabwene Mtahabwa, Skauti Mkuu Tanzania Mhe Mwantumu Mahiza na Askofu Mkuu wa Jimbo la Mbeya na Mjumbe wa Bodi ya Udhamini ya Skauti Mhashamu Baba Askofu Gervas Nyaisonga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *