
Timu ya Usimamizi Shirikishi kutoka Idara ya Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Seali za Mitaa(OR-TAMISEMI) imeridhishwa na utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya ya Kituo cha Afya Hoteli tatu kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.
Aidha timu hiyo imetoa rai kwa Kamati ya usimamizi wa shughuli za afya (CHMT) Halmashauri ya Kilwa kuendelea kuzingatia ubora wakati wa utekelezaji ili miundombinu hiyo idumu kwa muda mrefu lakini pia kuepusha adha na gharama ya kufanya ukarabati wa miundombinu mara kwa mara.
Hayo yamebainishwa Juni 2,2022 na Bw. Mathew Mganga Mkuu wa Kitengo cha huduma za dawa Ofisi ya Rais-TAMISEMI alipozungumza kwa niaba ya timu hiyo wakati wa ziara ya ukaguzi na utekelezaji wa shughuli za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.
“ ujenzi upo katika hatua nzuri, ubora na viwango unaridhisha lakini tuendelee kuzingatia ubora ili miundombinu hii idumu kwa muda mrefu lakini Pia kuondokana na adha ya kufanya ukarabati mara kwa mara” Bw. Mganga

Kwa upande mwingine timu hiyo imewataka wajumbe wa CHMT kuhahakikisha wanaimarisha usimamizi na ufatiliaji katika ujenzi wa Jengo la dharula linaloendea kujengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilwa (Kinyonga) ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati ifikapo tarehe 30 juni 2022.
Sambamba na hilo Bw. Mganga ametoa wito kwa wajumbe wa CHMT kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi pamoja na kushiriki kikamilifu katika zoezi la ukaguzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi ili kuleta uelewa wa pamoja lakini pia kuwa na taarifa sahihi za utekelezaji wa shughuli za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.



