BASHUNGWA ATOA SIKU SABA KWA WAKURUGENZI WALIOCHELEWESHA MIRADI KUJIELEZA

OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa ametoa siku saba kwa wakurugenzi wa Halmashauri ambao wako nyuma katika ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya kujieleza kwa nini wasichukukiwe hatua.

Bashungwa ameyasema hayo wilayani Chemba mara baada ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuzungumza viongozi wa Wilaya hiyo.

Alisema ndani ya wiki moja, Katibu Mkuu, Profesa Riziki Shemdoe akutane na wakurugenzi hao ambao wako nyuma katika ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali za Wilaya.

” Namuagiza Katibu Mkuu ndani ya wiki moja zile halmashauri ambazo ziko nyuma kwenye ujenzi wa miundombinu awe ameshakaa na wakurugenzi hawa na aniambie ni kwa nini nisiwachukukie hatua kwa wale ambao wako nyuma kwenye ujenzi”.

Wakati huo huo Bashungwa ameagiza wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa kuhakikisha ujenzi wa miundombinu hiyo inakamilika kwa asilimia 100 ifikapo Juni 30 mwaka huu.

” Nitumie fursa hii kuwaelekeza wakuu wa mikoa maelekezo niliyoyatoa ya ukamilishaji wa miundombinu vituo vya afya, zahanati na hospitali za Wilaya tunayo deadline(mwisho) ya Juni 30.

” Maelekezo niliyoyatoa ya Juni 30 lazima tukamilishe ujenzi, Wakuu wa mikoa na maRAS wahakikishe wanasimamia maelekezo haya.”

Alisema kabla ya kufikia muda huo anatarajia kufanya kikao na wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ambao watatakiwa kutoa taarifa ya hatua walizofikiwa.

Ofisi ya Rais-TAMISEMI imepanga kufika Juni 30 mwaka huu, kukamilisha miradi ambayo ilikuwa ikitekelezwa kabla ya operesheni maalumu ya Covid 19 ikiwa ni ujenzi wa hospitali 68 zilizojengwa mwaka 2018/19, ujenzi wa hospitali mpya 28, kuendeleza hospitali 31, vituo vya afya vipya 354, kuendeleza vituo vya afya 52 na  kukamilisha  zahanati 763, 

Aidha, Bashungwa alisema Rais Samia ametoa kibali cha ajira kwa watumishi na fedha kwa ajili ya vifaa tiba na kuwa kwa sasa Ofisi ya Rais-TAMISEMI iko katika hatua za mwisho za manunuzi.

Kwa upande wa Wilaya ya Chemba, Bashungwa ameupa uongozi wa Wilaya hiyo mpaka Juni 30 kukamilisha kwa asilimia 100 na kuwahidi kazi hiyo ikifanyika atawaletea vifaa tiba na watumishi.

” Kuhusu vifaa tiba, Rais Samia Suluhu Hassan ameshatupatia fedha na tuko katika hatua za mwisho za manunuzi, pia kibali cha kuajiri watumishi wa afya ambao ni wauguzi na madaktari. Hivyo Chemba jitahidini mkamilishe hospitali hii kwa asilimia 100, mkimaliza mtakuwa wa kwanza kuletewa vifaa tiba na watumishi.”

Naye Mkuu wa Mkoa, Anthony Mtaka alisema pamoja na Waziri kutoa muda wa hadi Juni 30, ni vyema uongozi wa Wilaya wakajiwekea muda wa hadi Juni 20 kukamilisha kazi hiyo.

Alisema ili kufikia muda huo waangalie namna ya kutekeleza mradi huo kwa kujenga usiku na mchana hususani kwa kazi ambazo hazina hathiri umaliziajia wa majengo.

Mbunge wa Chemba, Mohamed Moni alisema ujenzi wa hospitali hiyo ambayo awali ulisimama kwa mwaka mmoja na miezi saba unaendelea vizuri huku baadhi ya huduma zikianza kutolewa.

Hata hivyo imebainishwa changamoto zilizopo ni uhaba wa watumishi ambao ni asilimia 83, vifaa tiba jambo ambalo linafanya wananchi kwenda kupata baadhi ya huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *