TAMKO LA WAZIRI WA MAJI; KUHUSU USHIRIKI WA WIZARA YA MAJI KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI MJI WA SERIKALI MTUMBA TAREHE 02 JUNI, 2022

Ndugu Wafanyakazi na Waandishi wa habari: Kama mnavyofahamu, kila mwaka tarehe 5 Juni nchi yetu huungana na nchi nyingine kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho haya hutumia kaulimbiu inayoandaliwa na Shirika la Umoja wa Taifa linalosimamia Hifadhi ya Mazingira Duniani (UNEP) ili kuhamasisha jamii kuadhimisha Siku ya Mazingira kwa mwaka husika. Aidha, hapa nchini Maadhimisho ya Siku ya Mazingira yanaratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano.

Ndugu Wafanyakazi na Waandishi wa habari: Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo; “Only One Earth” kwa Kiswahili ni “Dunia ni Moja tu”. Kitaifa kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya ni “Tanzania ni Moja tu, Tunza Mazingira”, Kauli mbiu hii inahamasisha jamii “kuishi maisha endelevu pamoja na rasilimali inayotuzunguka” kwa Kingerea ni “Living Sustainably in Harmony with Nature”. Kutunza mazingira pamoja na rasilimali zinazotuzunguka kama rasilimali maji ni jukumu letu sote kwa kuwa Tanzani ni Moja tu, hakuna mbadala wa Tanzania.

Ndugu Wafanyakazi na Waandishi wa habari: Kama mnavyofahamu maji ni moja ya rasilimali adhimu, maji ni uhai, maji hayana mbadala, hivyo kauli mbiu ya mwaka huu inahimiza kutumia vema rasilimali tuliyonayo ili kuilinda Tanzania yetu. Hifadhi ya vyanzo vya maji ni muhimu ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Kauli hii inakwenda sambamba na tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alilolitoa tarehe 22 Machi, 2022 Jijini Dar es Salaam wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Maji kwamba “kwa Watanzania kutunza mazingira, hususan uoto wa asili kwa kuepuka kukata au kuchoma miti ovyo”.

Ndugu Wafanyakazi na Waandishi wa Habari: Katika maeneo ya vijijini, chemichemi nyingi za maji pamoja na baadhi ya mito imetoweka kutokana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli binadamu karibu na vyanzo vya maji. Kama inavyosema kaulimbiu ya mwaka huu, Tanzania ni Moja tu, Tutunze Mazingira, vyanzo vya maji vikikakauka vitahatarisha uwepo wa Mama Tanzania, hivyo hata uhai wetu utakuwa hatarini; ndio maana tunasema maji ni uhai, maji hayana mbadala. Unaweza ukakosa nishati ya umeme wa maji ukatumia nishati mbadala (jua, gas nk.), lakini maji hakuna uhai.

Ndugu Wafanyakazi na Waandishi wa habari: Ili kuhimiza umuhimu wa maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani, Wizara imetoa maelekezo kwa taasisi zake zote kushiriki ipasavyo katika maadhimisho haya katika ngazi ya Mkoa na Wilaya. Aidha, kwa kuwa Maadhimisho ya Kitaifa yanafanyika Jijini Dodoma yakiambatana na maonesho katika viwanja vya nje ya ukumbi wa Jakaya Kikwete, Wizara na Taasisi zake (DUWASA, RUWASA na Bodi ya Maji ya Wami-Ruvu) zinashiriki katika maonesho hayo. Hivyo, nitumie fursa hii kuwakaribisha wananchi wote kutembelea mabanda ya taasisi zetu ili kupata ufafanzi wa huduma zinazotolewa na Wizara.

Ndugu Wafanyakazi na Waandishi wa habari: Nitumie fursa hii pia kuwasihi Watumishi wote kushiriki katika matukio mbalimbali yanayokwenda sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Mazingira. Aidha, ninawasihi watumishi wa Wizara ya Maji kushiriki katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni, 2022 ambapo Mgeni rasmi atakuwa Mhe: Kassim Majaliwa Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma.

Ndugu Wafanyakazi na Waandishi wa habari: Aidha, ninatoa maelekezo kwa taasisi zetu zote kushirikiana na wadau mbalimbali katika kusimamia utunzaji wa rasilimali za maji. Kumekuwa na mtazamo wa kwamba Bodi za Maji pekee ndizo zenye jukumu la kusimamia na kutunza vyanzo vya maji, tutambue kwamba kutunza vyanzo vya maji ni wetu sote siyo Bodi za maji pekee.

Ndugu Wafanyakazi na Waandishi wa habari; Nitoe wito kwa Mamlaka za Maji nchini kuiga mfano wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga kwa namna wanavyoshirikiana na Bodi ya Maji Bonde la Pangani katika kuhifadhi chanzo cha maji cha Mto Zigi kupitia Umoja wa Wakulima Wahifadhi Mazingira Kihuhwi-Zigi (UWAMAKIZI). Leo hii wote tumeshuhudia maji yakiongezeka katika Bwawa la Mabayani ambalo ndio chanzo kikuu cha maji kwa Jiji la Tanga. Nimejulishwa pia hata gharama za uzalishaji wa maji zimepungua kutokana na kupungua kwa gharama za kununua madawa ya kutibu maji.

Ndugu Wafanyakazi na Waandishi wa habari: kwa msisitizo ninatoa maelekezo kwa Bodi za Maji za Mabonde nchini kutumia maadhimisho haya kuwaelimisha wananchi juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na Mamlaka za Maji kuwahimiza wananchi kutumia maji kwa uangalifu, kulipa ankra za maji na kulinda miundombinu ya maji.

Mwisho, kwa kuzingatia kuwa mwaka huu kutakua na tukio la Sensa ya watu na makazi, hivyo ni vema kila tukio la maadhimisho taasisi zetu likatoa ujumbe wa kuwakumbusha wananchi kuhusu sensa usemao; “Jiandae kuhesabiwa tarehe 23 Agosti, 2022, Tujenge Serikali ya Kidijitali” Kwa Wizara ya Maji Takwimu sahihi ni muhimu katika kuboresha usimamizi wa rasilimali ya maji na huduma ya majisafi na usafi wa mazingira.

ASANTENI

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *