BASHUNGWA AAGIZA WAKURUGENZI KUWARUHUSU MAKATIBU MAHSUSI KUHUDHURIA SHUGHULI ZA KITAALUMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa amewaelekeza wakurugenzi wa mamlaka za Serikali za mitaa na watendaji ndani ya wizara hiyo kutowazuia makatibu mahsusi kote nchini kuhudhuria shughuli za Chama Cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA).

Bashungwa amesema hayo Juni 2, 2022 Jijini Dodoma wakati akizungumza katika Mkutano mkuu wa 9 wa Makatibu Mahsusi( TAPSEA) ambao uliofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan.

“Asilimia 70 ya Watumishi wa umma wanatoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, hivyo nawaagiza wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wote nchini na watendaji wote ndani ya wizara, ole wenu atakayemzuia katibu mahsusi wake kwenda kuhudhuria mikutano hii,” amesisitiza Bashungwa

Waziri Bashungwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia ameonyesha mapenzi makubwa na makatibu mahsusi, Hivyo Ofisi ya Rais –TAMISEMI haitakubali kuwa kikwazo katika upendo wake na imani waliyoishosha kwake.

Amesema TAMISEMI wanaandaa jambo lao na watamuomba Rais Samia ashiriki ili aweze kuzungumza na Watendaji wa kata na vijiji nchi nzima.

“Kata zilizopo nchini ni 3,956 na vijiji 12,319 kwa kuwa ni wengi tutakachofanya tutaandaa mkutano na watendaji Kata ili wawakilishe watendaji wa vijiji na wao wapate fursa ya kukaa na kuzungumza na wewe ili wapate ari na moyo wa kufanya zaidi katika majukumu yao, nikuombe tukileta barua rasmi utukubalie,”amesema.

Aidha, Waziri Bashungwa amempongeza Rais Samia kwa kuwajali watumishi wakiwemo makatibu mahsusi kwa kuwaongezea mishahara na posho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *