NAIBU WAZIRI MAVUNDE AZINDUA KITABU CHA MRADI WA VIJANA WENYE ATHARI CHANYA ZA MAENDELEO KWENYE SEKTA YA KILIMO


Naibu Waziri, Wizara ya Kilimo, Antony Mavunde leo tarehe 31 Mei, 2022 amezindua rasmi kitabu chenye hamasa kwa vijana kuhusu mafaniko yao binafsi kwenye Sekta ya Kilimo kupitia Mradi wa Kuwaendeleza Vijana kwenye Kilimo (Advancing Youth Impact) kupitia Mradi Mkubwa wa Feed the Future unaosimamiwa na Shirika la Maendeleo la Marekani USAID.

Naibu Waziri Mavunde amepongeza aina hiyo ya Mradi ambao Umelenga kuleta athari chanya za maendeleo kwa Vijana wa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani (Zanzibar).

“Ninaamini, Mradi huu umechangia katika kupunguza umaskini kwa Watanzania ambao wengi wao ni Vijana na kupitia kitabu hicho, Taarifa na shuhuda zenu za mafanikio zitakuwa hamasa na kichocheo kwa kila Kijana, kwamba kuna mafanikio kwenye Sekta ya Kilimo na kuwa Tanzania ya kesho ni njema kwa kila atakayeamua kuwekeza kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.

Naibu Waziri Mavunde ametumia mkutano kuwakumbusha Washiriki kuwa Sekta ya Kilimo imechangia katika kupunguza umaskini wa kipato na wakati huo huo kuzalisha ajira kwa Watu.

“Sekta ya Kilimo inachangia asilimia 26.9 ya GDP, asilimia 61.5 ya ajira na asilimia 65 ya malighafi za viwandani. Takwimu zinaonyesha Vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 hawajaajiriwa huku kiwango hicho kikiongezeka kutoka asilimia 12.1 mwaka 2014 hadi asilimia 12.6 za sasa”.“Hii inaonyesha Sekta za Kiuchumi kama Kilimo na Viwanda zinatakiwa kuchangia katika kuzalisha ajira kwa Vijana.” Amekaririwa Naibu Waziri Mavunde.

Naibu Waziri Mavunde amesema, mafanikio ya Mradi wa Kuwaendeleza Vijana kwenye Kilimo (Advancing Youth Impact) Yametokana na uwezeshaji mkubwa kutoka Serikali ya Marekani na kuongeza kuwa uwezeshaji huo umesaidia kuendeleza miradi mingi na ambayo imejikita katika kuwajengea uwezo wa Wakulima wa Tanzania, kujenga na kuendeleza miundombinu ya barabara za vijijini ili kusafirisha mazao na Pembejeo.

Naibu Waziri Mavunde ametaja miradi ya kilimo inayonufaika na uwezeshaji kutoka Serikali ya Marekani kuwa ni pamoja na Mradi wa Mboga na Matunda chini ya Taasisi ya TAHA.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *