
Waziri wa Kilimo, Mhe.Hussein Bashe amesema Maonesho ya wakulima ya Nanenane yaliyokuwa yamesitishwa, sasa yanarudishwa rasmi kwa mfumo na utaratibu mpya tofauti na ilivyokuwa awali.
Waziri Bashe ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma leo wakati wa kipindi cha maswali na majibu alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Rita Kabati aliyetaka kujua mpango wa serikali kuhusu maonesho hayo.
Mhe.Bashe ameliambia Bunge kuwa maonesho ya mwaka huu yataadhimishwa kitaifa jijini Mbeya ambapo shughuli zote zitasimamiwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Sekretarieti za mikoa.
“Serikali ipo katika hatua za mwisho kuandaa mfumo wa Nanenane ambapo tumepanga kuwa na Maonesho ya Kimataifa ya Kibiashara ya Kilimo yajulikanayo kama Tanzania International Agricultural Trade Show ambayo yatakuwa yakifanyika kila mwaka katika eneo moja nchi nzima” Waziri Bashe aliliambia Bunge.
Aidha amefafanua kuwa taasisi ya TASO iliyokuwa imejimilikisha viwanja na maonesho hayo haitahusika tena na badala yake maonesho ya Nanenane yatasimamiwa na serikali kwa uratibu wa mikoa husika.