KISHINDO CHA MEMBE KUREJEA CCM,SHAKA AONGOZA MAPOKEZI

Aliyewahi kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Bernard Membe ameeleza sababu zilizomfanya arejee CCM ikiwemo kuondoka kwa sababu ambayo ilimfanya atimkie upinzani.

Aidha, amefungunguka jinsi alivyoumia kutokana na uamuzi wa kumwondolea uanachama wa CCM, Chama alichokulia huku akiahidi sasa atafia ndani ya CCM.

Akizungumza katika mkutano huo, katika Kijiji cha Rondo, alisema Machi 30 hadi Aprili 1, mwaka huu aliitwa Dodoma, kwenye kikao cha kamati ya Maadili ya CCM Taifa na Vikao vya kamati kuu ya CCM na Halmashauri Kuu ambapo kote alipewa nafasi na Mwenyekiti wa CCM Taifa kuzungumza na wajumbe wa vikao hivyo juu ya kurejeshewa uanachama wake.

“Mama yetu, Rais wetu na Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa Ndugu Samia Suluhu Hassan alinipa nafasi ya kuzungumza na wajumbe wa kamati kuu ya Chama Taifa. Nashukuru kwa kupewa nafasi ile na wajumbe waliliridhia kwa kauli moja nirejee CCM.

Nimerejea CCM kwa sababu kuu mbili, sababu ya kwanza nilishauriwa na viongozi wa dini zote, nilishauriwa na viongozi wa CCM ngazi ya Wilaya na Mkoa, nilishauriwa na marafiki zangu wote nirejee CCM, nilishauriwa na wana CCM.

Kutokana na ushauri wote huo sikuwa na namna nyingine zaidi ya kutii, nimekubaliana na ushauri wa wote waliosema nirudi CCM na sasa nimerudi CCM,” amesema Membe.

Amesema sababu ya pili ya kurudi kwenye Chama hicho inatokana na dhamira yake ya kukitumikia Chama Cha Mapinduzi hadi atakapokwenda kaburini. “Nilipoondolewa CCM nilisikitika sana, nilisononeka sana, na ninyi wananchi mlisikitika na mlisononeka sana.”

“Sababu ambazo zilinifanya niondoke CCM haziko tena, narudi sababu zilizoniondoa CCM haziko tena. Nimerudi, namshukuru Mwenyekiti wa CCM Mama yetu Samia Suluhu Hassan, wajumbe wa Kamati Kuu na halmashauri Kuu ya Taifa kwa kunirudisha. Nimerudi kwenye Chama ambacho nimezaliwa na kukulia, chama ambacho kimenisomesha na kunipa heshima ya kutumikia Nchi yangu.

Hivyo niahidi sitaondoka tena, nitabakia CCM hadi mwisho wa uhai wangu. Kurudi kwangu CCM nitaendelea kukitumikia Chama changu na sasa nitaendelea kushirikiana na Mbunge wangu Nape Nnauye. Mwaka 2015 nilisema nitawaletea Nape na kweli nilimleta, hivyo sasa Mtama mtakuwa na wabunge wawili, Mbunge wetu Nape na mimi mbunge wa chini chini.”

Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Mtama Mheshimiwa Nape Moses Nnauye amesema wanamshukuru sana Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan kupitia vikao mbalimbali vya chama hicho kwa kuwarejeshea matumaini, amani, furaha, mshikamano na kuwaondolea maumivu wana-CCM na wananchi wa mkoa wa Lindi na kusini kwa ujumla kwa kumrejeshea uanachama wa CCM ndugu yao Bernard Membe ambaye alionewa na kudhalilishwa.

Akizungumza katika mkutano huo, Shaka amesema Ndugu Membe amerejeshwa katika Chama baada ya kufuatwa kwa utaratibu ikiwemo kujadiliwa na tawi lake kupitia kamati ya siasa na kukubaliwa kurejeshewa kadi ya uanachama wa CCM.

Shaka amesema Membe na wanachama wengine zaidi ya 1,670 waliovuliwa uanachama ambao wamejadiliwa katika vikao na kurejeshewa uanachama, sasa wanaweza kukabidhiwa kadi zao katika matawi yao.

Shaka amesema kurejea kwa Ndugu Benard Membe ndani ya CCM kuendelee kuwa chachu ya kudumisha umoja na mshikamano hususani kwa wana-CCM wa Jimbo la Mtama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *