
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga ametoa pongezi kwa Uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma kwa kutekeleza ajenda ya Mazingira kwa vitendo.
Bi. Maganga ametoa pongezi hizo leo tarehe 29 Mei, 2022 mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Hospitali ya Benjamin Mpaka kwa lengo la kujionea jitihada za wadau katika upandaji wa miti na usafi wa Mazingira.
Akiwa Hospitalini hapo Bi. Maganga amejionea matumizi ya nishati mbadala wa kuni na mkaa kwa matumizi ya kupikia na kutoa rai kwa taasisi zingine kuiga mfano huo ili kupunguza kiasi cha ukataji wa miti kwa matumizi ya kuni na mkaa.

“Tumeshuhudia hapa, matumizi ya gesi kama nishati ya kupikia, nawapongeza sana, ninyi ni mfano wa kuigwa,” alisisitiza Bi. Maganga.
Pia, Bi. Maganga ameuagiza uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kuhakikisha kuwa eneo lililotengwa na kutumika kwa ajili ya kutibu majitaka halivamiwi na kutumika kwa matumizi mengine.
“Eneo hili lihifadhiwe vizuri kusiwe na shughuli nyingine za kijamii,” alisema Bi. Maganga.
Katika hatua nyingine wakati akitembelea na kukagua mabwawa ya kutibu majitaka, Katibu Mkuu huyo aliipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa kusimamia vyema mradi huo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe amesema Wizara ya Afya ina Taasisi nyingi na Hospitali ya Benjamin Mkapa ni moja ya Taasisi za mfano wa kuigwa.
Katika kuadhimisha Siku ya Mazingira shughuli mbalimbali za hifadhi na usafi wa mazingira zinafanyika katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma zikihusisha wananchi, taasisi, shule, vyuo na viongozi mbalimbali.

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatafikia kilele chake tarehe 5 Juni, 2022, Katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, ambapo Mgeni Rasmi ni Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
