
HOTUBA YA WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM, MHE. DKT. DOROTHY GWAJIMA (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO
NA MATUMIZI YA FEDHA KWA
MWAKA 2022/23
A. UTANGULIZI
- Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ndani ya Bunge lako Tukufu, ambayo imechambua Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, ninaomba kutoa hoja kwamba sasa Bunge lako likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum (Fungu 53) kwa mwaka 2021/22 na Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2022/23. Aidha, ninaliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Kawaida pamoja na Miradi ya Maendeleo ya Wizara kwa mwaka 2022/23.
- Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili kuwasilisha hotuba yangu siku ya leo. Pia, nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri katika kuimarisha utoaji wa huduma za ustawi na maendeleo ya jamii kwa Watanzania. Kipekee ninamshukuru kwa kuunda Wizara mpya ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na kuniteua kuiongoza Wizara hii. Natambua kuwa matarajio ya Mheshimiwa Rais ni kuona hali ya usawa wa kijinsia hapa nchini inaimarika na utoaji wa huduma za maendeleo na ustawi wa jamii unafanyika kwa kasi kubwa na ufanisi. Ninamuahidi kwamba nitaendelea kutimiza majukumu yangu kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha kwamba matarajio yake yanafikiwa kikamilifu. Aidha, nampongeza kwa kuendelea kuongoza nchi yetu kwa mafanikio makubwa tangu aingie madarakani akiwa ni Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sote tumeshuhudia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali chini ya uongozi wake.
- Mheshimiwa Spika, pia, napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuboresha huduma za maendeleo na ustawi wa jamii, kuhimiza usawa wa jinsia, uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na kuzingatia haki za mtoto katika jamii. Wizara yangu itaendelea kutekeleza kikamilifu maelekezo na mikakati inayotolewa na Ofisi yake.
- Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Kassim Majaliwa
Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri uliowezesha kuleta tija na ufanisi katika utendaji na kuimarisha huduma zinazotolewa katika Sekta ya Maendeleo na Ustawi ya Jamii. Aidha, ninampongeza kwa hotuba yake aliyoiwasilisha kwenye Bunge lako Tukufu tarehe 6 Aprili, 2022 ambayo imetoa mwelekeo wa majukumu yatakayotekelezwa na Serikali katika mwaka 2022/23.
- Mheshimiwa Spika, ninapenda kukupongeza wewe binafsi kwa kuaminiwa na Waheshimiwa Wabunge na kuweza kuchaguliwa kwa kishindo kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, ninampongeza Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb) kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika. Ni imani yangu kuwa mtatekeleza majukumu yenu kwa weledi na ufanisi mkubwa katika kuliongoza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, nawapongeza sana Wenyeviti wa Bunge kwa kuendelea kusimamia vyema mijadala mbalimbali ndani ya Bunge hili Tukufu.
- Mheshimiwa Spika, vilevile, nitumie fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Emmanuel Lekishon Shangai kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro na Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha kwa kuteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naamini kuwa Bunge lako Tukufu litaendelea kushirikiana nao ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
- Mheshimiwa Spika, ninapenda kuwashukuru Mawaziri wenzangu kwa ushirikiano wanaonipatia ambao unaiwezesha Wizara yangu kuendelea kuimarisha na kuboresha utoaji wa huduma za maendeleo na ustawi wa jamii. Wizara itaendelea kushirikiana nao na kuhakikisha tunatimiza dhamira ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha kuwa Sekta ya Maendeleo na Ustawi wa Jamii inaratibiwa vyema kwa matokeo chanya.
- Mheshimiwa Spika, kipekee ninapenda kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo (Mb) na Makamu wake, Mheshimiwa Aloyce John Kamamba (Mb) kwa ushauri na maelekezo waliyoyatoa wakati wa maandalizi ya Bajeti hii. Aidha, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano mzuri wanaotupatia ikiwemo kutoa ushauri na maoni mbalimbali yenye lengo la kuboresha huduma za maendeleo na ustawi wa jamii. Ninawaahidi kwamba, Wizara ninayoiongoza itazingatia ushauri wao na kuendelea kuwapa ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya kuwatumikia wananchi kwa moyo wote ndani na nje ya Bunge.
- Mheshimiwa Spika, naomba kutoa pole kwako, Bunge lako Tukufu na wananchi wote kwa vifo vya wapendwa wetu Mheshimiwa Elias John Kwandikwa, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mbunge wa Jimbo la Ushetu; Mheshimiwa William Tate Olenasha, aliyekuwa Naibu Waziri wa Uwekezaji (Ofisi ya Waziri Mkuu) na Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro; Mheshimiwa Khatibu Said Haji, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Konde Zanzibar); na Mheshimiwa Irene Alex
Ndyamkama, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa (CCM). Aidha, nawapa pole Watanzania wenzetu waliopoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukatili. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahala pema peponi. Amen.
- Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo ya awali, ninapenda sasa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2021/22, Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi pamoja na Maombi ya Fedha kwa ajili ya kutekeleza Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2022/23.
B. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2021/22
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sera, Mpango Mkakati pamoja na Makubaliano ya Kitaifa na Kimataifa yenye lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za maendeleo na ustawi wa jamii nchini. Sera hizo ni pamoja na Sera ya Maendeleo ya Jamii (1996); Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000); Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2001);Sera ya Taifa ya Wazee (2003); na Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008). Vilevile, katika kuandaa mpango na bajeti, Wizara imezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025), Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26), Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020, Mpango Kazi wa Taifa wa
Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18 – 2021/22), Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs 2030) na Agenda ya Afrika Tuitakayo (2063). Aidha, Wizara inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Ahadi za Nchi katika Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa
(Generation Equality Forum – GEF, 2021 – 2026).
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/22, Wizara ilipanga kutekeleza afua mbalimbali zenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma za maendeleo na ustawi wa jamii katika maeneo yafuatayo: –
- Kukuza ari ya jamii, uzalendo na kujenga moyo wa kujitolea katika kujiletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kutumia nguvukazi na rasilimali
zinazowazunguka;
- Kutekeleza dhana ya uanagenzi, ubunifu na ushirikishwaji jamii kwenye Taasisi na Vyuo ili kuzalisha wanafunzi wanaoajirika na kujiajiri na kuwa chachu ya maendeleo;
- Kuratibu uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na uingizaji wa masuala ya jinsia katika Sheria, Sera, Mipango, Mikakati, Programu na Bajeti;
- Kuendelea kuimarisha huduma za ustawi wa jamii na haki kwa familia na watoto ikiwemo malezi ya kambo na kuasili, watu/walezi wa kuaminika, malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto, ulinzi na usalama kwa watoto dhidi ya vitendo vya ukatili pamoja na huduma za utengemao katika familia kwa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani;
- Kuimarisha huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia, Msaada wa Kisaikolojia na Kijamii kwa familia, jamii na makundi mbalimbali wakiwemo wazee, watoto walio katika mazingira hatarishi pamoja na manusura wa ukatili na majanga mbalimbali;
- Kuimarisha ufuatiliaji na uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili yaweze kutoa mchango chanya katika ujenzi wa
Taifa;
- Kuendelea kuratibu kampeni mbalimbali za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto;
- Kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ili kutoa mafunzo yanayokidhi mahitaji ya soko;
- Kusimamia, kufuatilia na kuimarisha uanzishaji na uendelezaji wa Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo na Vituo vya Kijamii vya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto katika ngazi ya jamii ili kuboresha malezi na makuzi ya kila mtoto;
- Kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za msingi katika Vituo vya Ustawi wa Jamii ikiwemo Makazi ya Wazee na Watu wenye Ulemavu, Mahabusu za Watoto, Makao ya Watoto na Shule ya Maadilisho;
- Kuimarisha mifumo ya kusimamia, kufuatilia na kutathmini viwango vya huduma za ustawi wa jamii zinazotolewa nchini;
- Kuanzisha na kuimarisha utendaji wa Mabaraza ya Watoto na Dawati la Ulinzi la Watoto Shuleni;
- Kuendelea kuratibu uundwaji wa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto pamoja na kuzijengea uwezo;
- Kuratibu uanzishwaji wa vikundi vya malezi katika ngazi ya jamii; na
- Kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika ngazi za uongozi na nafasi mbalimbali za maamuzi.
MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA (FUNGU 53)
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/22, Wizara ilipanga kukusanya kiasi cha Shilingi 6,000,000,000 kutokana na ada za wanafunzi katika Vyuo nane (8) vya Maendeleo ya Jamii, uuzaji wa Mitaala ya Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, usajili na ada za mwaka za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), uuzaji wa Mitaala ya Vyuo vya Ustawi wa Jamii, ada za mwaka, uuzaji wa Mitaala ya Vituo vya kulelea Watoto Wadogo Mchana na vyanzo vingine vya mapato. Hadi kufikia mwezi Aprili 2022, Wizara imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi 3,566,324,302 sawa na asilimia 59ya makadirio ya mapato. Ni matarajio yangu kuwa hadi kufikia mwezi Juni 2022, Wizara itafikia lengo la asilimia 100 ya makusanyo kama ilivyopangwa.
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/22, Wizara iliidhinishiwa na Bunge lako tukufu jumla ya matumizi ya Shilingi
45,966,248,430.83. Kati ya fedha hizo, Shilingi 31,066,248,430.83 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Shilingi 18,080,576,430.83 ni fedha za Matumizi Mengineyo (OC) na Shilingi 12,985,672,000 ni kwa ajili ya Mishahara. Aidha, kiasi cha Shilingi 14,900,000,000 kilikuwa nikwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 4,900,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 10,000,000,000 ni fedha za nje.
- Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Aprili 2022, Wizara imepokea jumla ya Shilingi 31,315,282,868.47 sawa na asilimia 68ya bajeti kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha zilizopokelewa, Matumizi ya Kawaida ni Shilingi 25,143,892,668.47 sawa na asilimia 81ambapo kati ya fedha hizo, Shilingi 14,294,778,313.27 ni Matumizi Mengineyo na Shilingi 10,849,114,355.20 ni kwa ajili ya Mishahara. Aidha, Shilingi 6,171,390,200 ni Fedhaza Maendeleo ambapo kati ya fedha hizo, Shilingi 4,900,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 1,271,390,200 ni fedha za nje.
Naipongeza sana Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuipatia Wizara kiasi hicho cha fedha kwa mtiririko mzuri unaowezesha utekelezaji wa majukumu.
C. UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA (FUNGU 53)
16. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/22, utekelezaji wa majukumu ya Wizara ulilenga kuimarisha ushiriki wa jamii katika shughuli za maendeleo, kuimarisha upatikanaji wa haki na maendeleo ya mtoto, kuboresha huduma za ustawi wa jamii, kuchochea maendeleo ya jinsia na uwezeshaji wa wanawake, kuratibu utekelezaji wenye ufanisi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA). Uratibu wa utekelezaji wa majukumu haya ulifanywa na Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zake pamoja na wadau mbalimbali.
ENEO LA 1: MAENDELEO YA JAMII
- Mheshimiwa Spika, Wizara ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Jamii ya Mwaka 1996, ambayo inasisitiza dhana ya ushiriki wa jamii katika kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizopo katika maeneo yao. Aidha, inasisitiza kuendeleza na kukidhi mahitaji ya makundi maalum wakiwemo wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) ambao wengi wao ni vijana. Katika utekelezaji wa jukumu hilo, yafuatayo yamefanyika: –
- Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, Wizara imeimarisha uratibu na usimamizi wa shughuli za wafanyabiashara ndogondogo wajulikanao kama Machinga, kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyotoa tarehe 25 Januari 2022 kwamba Serikali anayoiongoza inawatambua Machinga wote nchini kama kundi maalum ambalo litakuwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Hivyo, uongozi wa Wizara uliwapokea rasmi na kukutana na viongozi wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA) ngazi ya Taifa. Aidha, katika vipindi tofauti kuanzia mwezi Februari hadi Aprili 2022, Wizara imejadiliana nao na kubaini kuwa Shirikisho hilo lilikuwa linakabiliwa na changamoto za kiuongozi na kiusimamizi, kiuchumi, kimfumo (TEHAMA), kutokuwa na usajili, kutokuwa na mahali pa uhakika pa kufanyia kazi na kutokuwa na anwani.
- Mheshimiwa Spika, katika kutatua changamoto hizo, Wizara imewezesha usajili wa SHIUMA kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kupatiwa cheti chenye usajili Namba 21825. Pia, imewajengea uwezo viongozi 10 wa SHIUMA ngazi ya Taifa pamoja na washiriki 198 kutoka Mikoa 26 ya Tanzania Bara. Lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwajengea uwezo kuhusu uongozi bora, fursa za kifedha, ujasiriamali na utii wa sheria bila shuruti. Aidha, imewapatia sehemu ya kufanyia kazi ndani ya jengo lake. Vilevile, inaendelea kuimarisha mahusiano ya kiutendaji baina ya viongozi na wanachama wa shirikisho kuanzia ngazi ya Taifa hadi kwenye masoko. Wizara kupitia Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imeanza kutengeneza Mfumo wa Kieletroniki wa utambuzi wa wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) ujulikanao kama “Wajasiriamali Connect”. Mfumo huo utawawezesha wafanyabiashara hao kupata fursa mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mikopo nafuu kutoka katika taasisi za fedha.
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeratibu mafunzo kwa viongozi 803 wa SHIUMA kuanzia tarehe 16 – 19 Mei, 2022 Jijini Dodoma. Kaulimbiu ilikuwa “Machinga ni Fursa Sahihi ya Kukuza Uchumi wa Nchi Yetu’’. Katika mafunzo hayo, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alishiriki kwa njia ya simu ambapo aliweza kuahidi kutoa Shilingi Milioni 10 kwa kila Mkoa kuanzia mwaka 2022/23 ili kukabiliana na changamoto wanazopata Machinga katika uendeshaji wa shughuli zao. Mwelekeo zaidi kuhusu Machinga ni kuandaa Sheria moja ya Machinga pamoja na Mkakati wa Maendeleo ya Machinga hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa.
- Mheshimiwa Spika, Wizara inapenda kutambua mchango wa Wadau mbalimbali, Taasisi na Wizara za Kisekta ikiwemo: Ofisi ya Makamu wa Rais; Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu; Ofisi ya Rais – TAMISEMI; Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; Wizara ya Fedha na Mipango;
Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara; Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi; na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Wizara hizi kwa pamoja zimeweza kutekeleza majukumu yake katika kutatua changamoto za Machinga kama ifuatavyo: kuratibu zoezi la utambuzi wa Machinga kwa kuwapa vitambulisho na kuondoa kodi zilizokuwa zinakwamisha ukuaji wa biashara za Machinga; kutenga na kujenga miundombinu ya masoko katika Mikoa mbalimbali ili kurahisisha utendaji wa shughuli za Machinga; kuwapa elimu juu ya utambuzi wa bidhaa bandia; athari zinazotokana na bidhaa bandia kwa Machinga na katika uchumi wa nchi; na kuwapa elimu juu ya kuheshimu sheria za Nchi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
- Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri nchini na Wadau wengine kwa namna wanavyoshughulikia suala la ujenzi wa miundombinu na upangaji wa wafanyabiashara ndogondogo nchini. Aidha, shukrani zangu za dhati ziwafikie viongozi wa SHIUMA ngazi ya Taifa kwa kuendelea kushirikiana na Wizara yangu katika kuhakikisha kuwa changamoto za Machinga Nchini zinapatiwa ufumbuzi.
- Mheshimiwa Spika, Wataalam wa
Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na viongozi ngazi mbalimbali wamekuwa chachu ya kutekeleza kampeni mbalimbali za Kitaifa na wanaendelea kuamsha ari ya jamii kuboresha makazi yao. Kampeni hii inatumia mfumo wa asili wa kusaidiana katika maeneo yenye makazi duni ikiwemo Mikoa ya Lindi, Kagera, Tanga, Tabora, Pwani, Arusha, Kigoma, Singida, Mtwara na Katavi. Ujenzi wa nyumba hizo unatumia gharama nafuu kati ya Shilingi 7,000,000 hadi Shilingi 10,000,000 ambapo jamii au kikundi humsaidia mmoja wao anayejenga nyumba kufyatua tofali za kuchoma, kukusanya mawe, mchanga na kuchota maji ya kujengea ili kupunguza gharama za ujenzi. Fedha taslimu hutumika kununua vifaa vya dukani kama bati na saruji. Aidha, jamii hutumia vikundi vya kuweka na kukopa (VICOBA) au mtindo wa kupeana fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya dukani.
Vilevile, ili kurahisisha ujenzi wa nyumba bora,
Vyuo vya Maendeleo ya Jamii Ufundi vya Mabughai na Misungwi vimekuwa na utaratibu wa kuandaa ramani za makazi na kuzitoa kwa gharama nafuu. Katika kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, kampeni ya makazi bora imetekelezwa katika Mikoa 10. Nyumba zilizojengwa zimeongezeka kutoka nyumba 751 mwaka 2020/21 hadi nyumba 5,002 kufikia mwezi Aprili, 2022. Nyumba hizo zimejengwa katika Mikoa ya Arusha (683), Morogoro (2,397), Songwe (225), Shinyanga (698), Rukwa (22), Mwanza (273), Tanga (350), Ruvuma (2), Pwani (186) na Geita (166). Kampeni inalenga kufikia Mikoa 26 ifikapo mwaka 2025. Nitumie fursa hii kuishukuru Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa miongozo ya Kisera, OR-TAMISEMI kwa kusimamia utekelezaji wa kampeni na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hususan Shirika la Kivulini kwa kushiriki kuhamasisha jamii kuboresha makazi yao.
- Mheshimiwa Spika, katika kuamsha ari ya jamii kushiriki kikamilifu kwenye miradi ya kijamii kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na viongozi ngazi mbalimbali kuanzia Taifa, Mkoa, Halmashauri hadi Kata wameendelea kuhamasisha jamii kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye Mikoa 26 ya Tanzania Bara, ambapo jamii imeshiriki kikamilifu kwenye miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 963 katika Mikoa ya Singida, Morogoro, Arusha, Kilimanjaro, Rukwa, Katavi, Dodoma, Dar es Salaam, Geita, Kagera, Kigoma, Lindi, Mara, Mbeya, Mtwara, Pwani, Njombe, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Tanga, Iringa na Lindi. Aidha, jamii imeshiriki katika ujenzi wa vituo 294 vya kutolea huduma za afya katika Mikoa ya Iringa, Singida, Morogoro, Arusha, Katavi, Dar es Salaam, Geita, Kagera, Kigoma, Lindi, Mara, Mbeya, Mtwara, Njombe, Pwani, Ruvuma, Rukwa, Tanga, Tabora, Simiyu na Kilimanjaro. Juhudi za ujenzi wa madarasa hayo kupitia utaratibu huu zinachangia hesabu ya madarasa kama ilivyowasilishwa na Waziri wa Nchi, OR-TAMISEMI, Mhe. Innocent Lugha Bashungwa wakati akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2022/23 hivyo kuleta msukumo wa maendeleo ya jamii kwenye Sekta ya Elimu.
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha utoaji wa mafunzo ya Taaluma ya Maendeleo ya Jamii katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vya Buhare, Mlale, Misungwi, Rungemba, Mabughai, Ruaha, Uyole na Monduli kwa kusimamia ubora wa mafunzo na kuboresha miundombinu. Udahili wa wanafunzi umeongezeka kutoka wanafunzi4,753 (Me 1,871 na Ke 2,882) mwaka 2020/21 hadi wanafunzi 5,135 (Me 2,112 na Ke 3,023) kufikia mwaka 2021/22 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 382sawa na asilimia 8. Aidha, mwaka 2020/21, wanafunzi 2,759 walihitimu katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ikilinganishwa na wanafunzi 3,953 waliohitimu mwaka 2019/20 sawa na upungufu wa asilimia 30 ya wahitimu. Hii ni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuahirisha masomo na kushindwa kulipa ada.
- Mheshimiwa Spika, katika kutatua changamoto hizo, Wizara imefanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuwaunganisha wanafunzi na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayosaidia wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu yakiwemo; Compassion, CAMFED, Tumaini Fund, Black School Learning, SEMA Singida, King Lion na Ngorongoro Community-Based Organization. Aidha, wanafunzi wengine wamekuwa wakiunganishwa na Mikoa na Halmashauri ili kuwawezesha kuendelea na masomo kupitia mafungu ya kuwasaidia wanafunzi wasio na uwezo. Hadi Aprili 2022, jumla ya wanafunzi 29 wasio na uwezo wa kulipa ada wameunganishwa na Mashirika mbalimbali ambapo wamewezeshwa kuendelea na masomo yao.
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha utoaji wa mafunzo ya Taaluma ya Maendeleo ya Jamii katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) na Vyuo nane (8) vya Maendeleo ya Jamii (CDTIs) kwa kutekeleza dhana ya Uanagenzi ili kuzalisha wahitimu wenye weledi na umahiri unaoendana na soko la ajira. Uanagenzi (apprenticeship) ni programu ya kukuza ujuzi ambapo vyuo huwaunganisha wanafunzi/wahitimu wake na Kampuni, Mashirika na Taasisi mbalimbali ili waweze kupata ujuzi/kujengewa uwezo katika eneo fulani kulingana na mahitaji yao. Programu hii ilianzishwa rasmi mwaka 2019/20. Aidha, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi Ibara ya 22 (a) ukurasa wa 22 imehimiza kuongeza ujuzi wa mafunzo kwa vitendo kwa vijana ili kuwasaidia vijana kujiajiri, kuajiriwa na kuajiri wengine.
- Mheshimiwa Spika, jumla ya wanafunzi na wahitimu wa Vyuo 721 walijiunga na programu ya uanagenzi mwaka 2021/22 ambapo kati ya hao, vijana 114 sawa na asilimia 16 wamehitimu programu ya uanagenzi katika mwaka huu wa fedha na kupata ujuzi katika maeneo ya ujasiriamali, ujenzi wa barabara, usimamizi wa miradi, uandishi wa maandiko ya miradi, uelimishaji rika na ujenzi wa majengo. Aidha, kati ya hao, vijana 40 wamepata ajira (27 wamejiajiri na 13 wameajiriwa katika Kampuni na Mashirika mbalimbali) na wengine 607 bado wanaendelea na programu ya uanagenzi. Katika mwaka 2022/23, vyuo vinatarajia kupeleka wanafunzi 931 kujifunza mafunzo mbalimbali kwenye Kampuni, Mashirika na Taasisi 334. Kwa maelezo hayo, ni dhahiri kuwa Wizara imejielekeza kwenye mapinduzi ya mafunzo ili wahitimu waweze kujiajiri na kuajiri.
- Mheshimiwa Spika, Wizara inatekeleza programu ya ushirikishaji jamii zinazozunguka Taasisi na Vyuo nane vya Maendeleo ya Jamii kutatua changamoto zinazowakabili kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka kama ifuatavyo: elimu ya lishe imetolewa kwa wananchi 825 wanaozunguka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vya Rungemba na Ruaha; na hamasa ya kilimo cha parachichi imetolewa na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Rungemba katika Vijiji vya Kitelewasi, Itimbo na Rungemba ambapo jumla ya miche
6,120 imepandwa katika Vijiji hivyo. Pia, elimu ya ujasiriamali imetolewa kwa wananchi 376 wanaozunguka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vya Mlale na Monduli. Aidha, mafunzo ya ufundi ujenzi yametolewa na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Misungwi kwa mafundi 40.
Napenda kutoa wito kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii waliopo katika ngazi ya Mkoa, Halmashauri na Kata kushirikiana na wadau wengine wote na kuendelea kwa kasi zaidi kuelimisha na kushirikisha jamii kuimarika katika dhana nzima ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
- Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuipatia Wizara fedha za maendeleo kiasi cha Shilingi Bilioni 3.6 kwa ajili ya ukarabati wa majengo na miundombinu katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii. Hatua hii itaboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Vyuo hivyo.
- Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi zote za ushirikishaji jamii zinazofanywa na Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini, bado tunakabiliana na changamoto ya uhaba wa Maafisa hao. Jumla ya Maafisa Maendeleo ya Jamii 5,296 wanahitajika nchini. Hadi mwezi Aprili 2022, Maafisa waliopo katika ngazi ya Mkoa, Halmashauri na Kata ni 3,014 ambapo upungufu ni Maafisa 2,282 sawa na asilimia 43 kama inavyoonesha katika Jedwali Na. 1. Mahitaji makubwa zaidi ya wataalam hawa yapo ngazi ya Kata ambapo kuna changamoto nyingi za jamii zinazopaswa kushughulikiwa.
Jedwali Na. 1: Idadi ya Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Ngazi Mbalimbali
NA. | NGAZI | MAAFISA WANAOHITAJIKA | MAAFISA WALIOPO | UPUNGUFU / ZIADA | ||
IDADI | % | IDADI | % | |||
1. | Mkoa | 52 | 51 | 98 | -1 | -2 |
2. | Halmashauri | 1,288 | 1,329 | 103 | 41 | 3 |
3. | Kata | 3,956 | 1,634 | 41 | -2,322 | -59 |
JUMLA | 5,296 | 3,014 | 57 | -2,282 | -43 |
Chanzo: OR-TAMISEMI
- Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa Maafisa Maendeleo ya Jamii, Wizara itaendelea kuwasiliana na ORTAMISEMI pamoja na OR-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kutatua changamoto ya upungufu wa Maafisa hao katika ngazi ya Kata kwa kuwaajiri kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kadiri bajeti ya Serikali itakavyoruhusu kila mwaka.
Nitoe rai kwa Wadau wa Maendeleo yakiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoa ajira za muda kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii hususan katika ngazi ya Kata ambapo kuna upungufu mkubwa ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa afua za kutatua changamoto zinazoikabili jamii yetu. Pia, Wizara inatoa wito kwa wote wenye taaluma ya maendeleo ya jamii ambao wapo katika jamii baada ya kustaafu wajitokeze ili kuendelea kutoa mchango wao kwenye jamii kama ambavyo taaluma zingine zimekuwa zikifanya. Lengo ni kila mzalendo mwenye nafasi na nia ya kuchangia maendeleo ya jamii apewe nafasi.
- Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Vyuo nane vya Maendeleo ya Jamii vya Buhare, Monduli, Rungemba, Ruaha, Uyole, Mlale, Misungwi na Mabughai imeendelea kutekeleza programu mbalimbali zinazolenga kukuza ubunifu na maarifa. Ubunifu na Maarifa ni programu ambayo wanafunzi na jamii inayozunguka vyuo wanapewa fursa ya kutoa mawazo yao ya kibunifu ambayo yanalenga kutatua changamoto fulani katika jamii ambapo mawazo hayo hulelewa ili yafikie hatua ya kuwa huduma au bidhaa iliyokusudiwa.
Programu zinazotekelezwa katika Taasisi na Vyuo hivyo ni pamoja na: kutoa uelewa kwa wananchi kuhusu uwepo wa nafasi za kupokea na kulea mawazo ya kibunifu kwenye vituo na umuhimu wa ubunifu katika kuongeza kipato chao; kuwajengea uwezo wanafunzi na wananchi katika eneo la ubunifu kwa kuwaunganisha na wabunifu wakubwa pamoja na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali; na kuwaunganisha wabunifu na masoko kwa ajili ya kutangaza na kuuza bidhaa/huduma zinazotokana na ubunifu wao.
- Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, jumla ya mawazo ya kibunifu saba (7) yameibuliwa na hivyo kuwa na jumla ya mawazo ya kibunifu 61 tangu kuanzishwa kwa dhana ya ubunifu na maarifa mwaka 2019/20. Kati ya hayo, mawazo ya kibunifu 23 (sawa na asilimia 38) yamekamilika na yapo kwenye hatua za mwisho kuwa bidhaa au huduma. Huduma/bidhaa hizo ni pamoja na: kifaa cha kugundua madini ardhini katika Chuo cha Maendeleo Jamii Ufundi Misungwi ambapo mbunifu ametengeneza sampuli kifani na Chuo kimeshirikisha Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili kukamilisha wazo hilo kuwa bidhaa; mashine ya kuchakata viazi katika Chuo cha Maendeleo Jamii Ufundi Misungwi ambapo Chuo kimeshirikisha SIDO kukamilisha wazo hilo; na mashine ya kusukuma maji inayotumia nishati ya maji katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mlale ambapo mbunifu huyo amefanikiwa kutengeneza mashine tatu na kuziuza kwa kiasi cha Shilingi Milioni
2.2 kila moja. Aidha, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru imeanzisha huduma ya web application kwa ajili ya kusaidia uuzaji, utunzaji wa hesabu na kutangaza masoko ya bidhaa za wajasiriamali.
- Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani kwa COSTECH kwa kutoa mafunzo ya namna ya kuanzisha, kusimamia na kuviendesha vituo vya kidijitali vya ubunifu na maarifa katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii. Aidha, Wizara inaendelea kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhamasisha jamii kwenda kwenye vituo vya kidijitali vya ubunifu na maarifa kwa kuonesha vipaji vya kibunifu walivyonavyo na kufanya uhamasishaji kwa Taasisi za elimu ya juu, kati na Sekondari ili kuongeza mwitikio wa jamii kujiunga katika vituo hivyo. Wizara inaendelea kutafuta wadau kwa ajili ya kufadhili wabunifu kufikia malengo yao.
ENEO LA 2: HAKI NA MAENDELEO YA MTOTO
- Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike na wanawake vinatokomezwa, Wizara imeshirikiana na wadau kuandaa Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2020/21 – 2024/25. Mkakati unalenga kupunguza ukeketaji nchini kutoka asilimia 10 mwaka 2015/16 hadi asilimia 5 mwaka 2021/22 na hatimaye kutokomeza ukeketaji ifikapo mwaka 2024/25. Mkakati huo utafikia malengo yake iwapo: (i) Wasichana na wanawake watakataa vitendo vya ukeketaji; (ii) Msaada na huduma zitapatikana kwa waathirika wa ukeketaji kwa wakati; (iii) Familia zitakataa kuwatoa watoto wao wa kike kwa ajili ya kukeketwa; (iv) Jamii zitapinga na kukataa ukeketaji ikiwemo jamii ya wanaume wa rika zote; (v) Ngariba wengi watakataa na kuacha vitendo vya ukeketaji; na (vi) Uratibu wa wadau katika kushughulikia masuala ya ukeketaji utaimarishwa. Utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji utachangia katika utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008; Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000; Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na Sheria mbalimbali zikiwemo Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2019; na Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2018.
- Mheshimiwa Spika, ukeketaji una madhara makubwa katika maendeleo na ustawi wa jamii. Madhara hayo ni pamoja: maumivu makali kwa mtoto (ukatili wa kimwili); kutokwa damu nyingi kwa mtoto jambo linaloweza kusababisha kupoteza maisha; na kovu la kudumu linalosababisha maumivu wakati wa kujamiiana na hatimaye kupoteza hisia na kusababisha migogoro katika ndoa. Aidha, ukeketaji unaweza kusababisha kupata magonjwa kama Fistula (kutokwa na haja ndogo mara baada ya kujifungua) na maambukizi katika njia ya mkojo (UTI).
- Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa ukeketaji inaratibu utendaji wa Muungano (coalition) wa Taifa wa utekelezaji wa afua za Kutokomeza Ukeketaji Nchini. Muungano huo unajumuisha watendaji wa Wizara za Kisekta, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Wadau wengine wa masuala ya ukeketaji. Vilevile, Wizara inaratibu utekelezaji wa Maazimio na Mpango Kazi wa Kushughulikia Ukeketaji Mipakani mwa nchi za Afrika Mashariki. Mpango huo unalenga kuzuia vitendo vya ukeketaji wa kuvuka mipaka ambapo familia zinawavusha watoto kwenda nchi jirani kwa kuhofia vyombo vya dola kuwachukulia hatua. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2022 jumla ya Kamati tano (5) za Ulinzi na Usalama katika Wilaya za Tarime (Sirari), Longido (Namanga), Mkinga (Hororo), Rombo (Holili) na Serengeti zimejengewa uwezo ili kukabiliana na vitendo vya ukeketaji wa kuvuka mipaka. Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutekeleza afua za kutokomeza ukeketaji katika mikoa yenye takwimu za juu ambayo ni Manyara kwa asilimia 58; Dodoma asilimia 47; Arusha asilimia 41; Mara asilimia 32; na Singida asilimia 31. Afua hizo zimewezesha takribani ngariba 1,800 katika mikoa hiyo kusalimisha zana za ukeketaji na kuachana na vitendo hivyo kwa kipindi cha mwaka 2015/16 hadi kufikia Aprili, 2022.
- Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na aina mpya ya Ukatili dhidi ya Watoto Mitandaoni unaosababishwa na kukua kwa maendeleo ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA), Serikali imeunda kikosi kazi cha Taifa cha Ulinzi na Usalama wa Mtoto mtandaoni chenye lengo la kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa dhidi ya ukatili wa mtandaoni na kuwasaidia kutumia vifaa vya kieletroniki kwa usahihi na usalama. Pia, Kikosi Kazi kina jukumu la kuratibu wadau katika Serikali na Sekta Binafsi kuhuisha masuala ya ukatili dhidi ya watoto mtandaoni na utekelezaji wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009. Aidha, Serikali imeandaa machapisho/majarida ya kufundishia watoto, wazazi na walimu kuhusu ukatili wa watoto mtandaoni.
- Mheshimiwa Spika, katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 na Kanuni zake, Wizara imebaini kuwa kuna uhitaji wa kuifanyia marekebisho Sheria hiyo ili iweze kuakisi mazingira ya sasa ikiwa ni pamoja na ukatili wa watoto mtandaoni (online child abuse). Ili kutekeleza hilo, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Mwandishi Mkuu wa Sheria) imeshaandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria na kuyawasilisha kwa wadau ili kutoa maoni ambapo tayari Wizara imeanza kupokea maoni. Mchakato wa marekebisho ya Sheria hiyo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba, 2022. Pia, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inayosimamia Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 inafanya mapitio ya Sera ya hali ya usalama katika mitandao ili kubaini maeneo ya kuboresha. Aidha, ifikapo mwezi Oktoba, 2022 zoezi la tathmini litakuwa limekamilika na litatoa mwelekeo wa kuandaa Sera na Sheria mpya ya Makosa ya Mtandao.
- Mheshimiwa Spika, mwezi Machi 2022, Wizara ilizindua Taarifa ya Utafiti kuhusu Hali ya Ukatili wa Watoto Mtandaoni nchini (Disrupting Harm Report in Tanzania). Utafiti huo ulifanywa mwaka 2021 kwa ushirikiano wa Mashirika yafuatayo: Shirika la kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF – Tanzania), Shirika la ECPAT International na INTERPOL kwa uratibu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya usimamizi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Aidha, nchi nyingine 12 za Afrika zilifanya utafiti kama huu kutoka Barani Afrika (Nchi 6 kutoka Mashariki na Kusini mwa Afrika na 6 Kusini Mashariki mwa Bara la Asia). Taarifa hiyo inaeleza tathmini ya kina ya hali ya ukatili nchini, athari za ukatili wa kingono, mitazamo ya watoto juu ya ukatili wa kingono mtandaoni na mwitikio wa kitaifa wa namna ya kupambana na aina hii ya ukatili. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa: –
- Asilimia 4 ya watumiaji wa mtandao wenye umri wa miaka 12 – 17 nchini Tanzania ni manusura wa ukatili wa mtandaoni;
- Watoto wengi hufanyiwa vitendo vya ukatili kupitia mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp, Instagram, Facebook, Tik Tok;
- Wanaofanya vitendo vya ukatili ni watu wanaofahamika na watoto wakiwemo ndugu wa karibu na marafiki; na
- Watoto wanaofanyiwa ukatili hawajui namna na sehemu ya kutoa taarifa ili wapate msaada.
- Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha Malezi na Makuzi Jumuishi ya Watoto wa umri wa miaka 0 – 8 ambao ndio umri muhimu sana katika ukuaji wa ubongo wa binadamu, Wizara imezindua Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJTMMMAM) itakayotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (2021/22 – 2025/26). Programu hii inalenga kutatua changamoto za ukuaji na maendeleo ya watoto wenye umri wa miaka 0-8 na kuhakikisha watoto wote Tanzania wapo kwenye mwelekeo sahihi wa kufikia ukuaji timilifu. Pia, Programu ya MMMAM inalenga kuharakisha upatikanaji wa matokeo chanya kwenye malezi na makuzi ya watoto kwa kuhimiza ushiriki wa Sekta mbalimbali katika kutoa huduma za malezi jumuishi kwa watoto kwenye maeneo makuu matano (5) ambayo ni: Afya bora kwa Mtoto na Mama/Mlezi; Lishe ya kutosha kuanzia Ujauzito; Malezi yenye Mwitikio; Fursa za Ujifunzaji wa Awali; na Ulinzi na Usalama. Aidha, ili kuhakikisha programu hiyo inaleta matokeo chanya kwa watoto wadogo, itatekeleza mambo makuu manne ambayo ni: kuboresha mazingira wezeshi ili kuwezesha uratibu wenye ufanisi na utoaji wa huduma za malezi jumuishi; kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma jumuishi za MMMAM na uthibiti ubora; kuongeza upatikanaji wa huduma bora na zilizoratibiwa za malezi jumuishi kwa watoto wenye umri wa miaka 0-8 na walezi wao; na kuwawezesha wazazi, walezi, familia na jamii kutoa huduma za malezi jumuishi.
- Mheshimiwa Spika, katika hatua za awali za utekelezaji wa Programu ya MMMAM, mwezi Desemba 2021, mafunzo ya uelewa kuhusu Programu hiyo yalitolewa kwa Watendaji wa Sekretarieti za Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara ambapo kila Mkoa uliwakilishwa na watendaji watano (5) wakiwemo Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii, Waganga Wakuu, Maafisa Elimu na Maafisa Lishe wa Mikoa. Pia, mafunzo hayo yalitolewa kwa wanahabari vinara wa Programu hiyo ili kuwajengea uwezo wa kutoa taarifa za utekelezaji wake. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na wadau ilijenga hamasa kwa Waheshimiwa Wabunge ambao wameanzisha Kikundi cha Wabunge Vinara (champions) wapatao 30 kuwa Mabalozi katika kusukuma Ajenda ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ndani na nje ya Bunge. Kikundi hicho kinaongozwa na Mhe. Dkt. Pius Chaya (Mwenyekiti), Mhe. Esther Matiko (Makamu Mwenyekiti) na Mhe. Justine Nyamoga (Katibu).
Aidha, kikundi hicho kimeandaa Katiba na Mpango Mkakati wa Miaka Mitatu (3) utakaowaongoza katika kutekeleza majukumu yao. Nitumie fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge hawa kwa kujitolea kusukuma Ajenda hii muhimu katika Nchi yetu inayolenga kuimarisha malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya Mtoto.
- Mheshimiwa Spika, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la BRAC Maendeleo imeratibu ujenzi wa Vituo 30 vya mfano vya Kijamii vya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (Community-Based Early Childhood Development Centers) katika Mikoa ya Dar es Salaam (10) na Dodoma (20). Vituo hivyo vina lengo la kutoa huduma jumuishi za Malezi na Makuzi kwa Watoto walio na umri kuanzia miaka miwili (2) hadi chini ya miaka mitano (5) kwa kuwapatia huduma jumuishi za afya, lishe, ulinzi, ujifunzaji na uchangamshi wa awali kabla ya kujiunga na darasa la awali. Katika kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, jumla ya Vituo vya mfano 15 kati ya 30 vimeanza kufanya kazi na jumla ya watoto 883 (Wavulana 426 na Wasichana 457) wamesajiliwa na kupatiwa huduma katika Vituo hivyo kama inavyoonesha katika Kiambatisho Na. 1. Aidha, vituo hivyo vitatumika kama mfano katika ujenzi wa vituo vingine vitakavyojengwa katika
Vijiji/Mitaa yote ya Tanzania Bara.
- Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Programu hii ina mfumo madhubuti wa kukusanya na kutunza taarifa za utekelezaji, Wizara kwa kushirikiana na UNICEF na Wataalam wa Mifumo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imetengeneza Dashbodi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECD Dashboard) ambayo itawezesha ukusanyaji na utunzaji wa taarifa mbalimbali zinazohusu masuala ya Lishe, Afya, Fursa za Ujifunzaji wa Awali, Malezi yenye Mwitikio, Ulinzi na Usalama kwa Watoto wenye umri kati ya miaka 0-8. Aidha, Dashbodi hii imeunganishwa na mifumo mbalimbali inayotoa taarifa zinazohusu watoto wadogo.
- Mheshimiwa Spika, katika kushughulikia changamoto zinazowakabili vijana balehe wenye umri wa kati ya miaka 10 – 19, Wizara imeandaa na inatekeleza Ajenda ya Kitaifa ya Kuwekeza katika Afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe nchini (2021/22-2024/25). Ajenda imeandaliwa kwa ajili ya kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma rafiki za afya na kuondoa vikwazo vya maendeleo kwa vijana balehe nchini ambapo makadirio ya idadi ya vijana balehe kwa mwaka 2020 ni milioni 13 sawa na asilimia 23 ya watu wote nchini. Ajenda hii imejikita katika nguzo kuu sita (6) ambazo ni: Kuzuia Maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI; Kutokomeza Mimba za Utotoni; Kuzuia Ukatili wa Kimwili, Kisaikolojia na Kingono; Kuboresha Lishe, Kuhakikisha Watoto wa Kike na Kiume Wanabaki Shule; na Kuwajengea Vijana Balehe Ujuzi na Uwezo wa Kufikia Fursa za Kiuchumi.
Ajenda imejikita katika kutekeleza afua za kipaumbele zitakazoleta matokeo makubwa katika kipindi cha muda mfupi na muda wa kati. Pia, afua saidizi na afua nyinginezo zitakazoibuka zitatekelezwa katika muda wa kati na muda mrefu. Afua zinazohitajika katika kuboresha afya na maendeleo ya vijana balehe zinagusa maeneo mahsusi ya Mahitaji, Usambazaji na Mazingira Wezeshi. Kwenye eneo la Mahitaji, afua zinalenga kuboresha elimu, kupunguza kiwango cha umaskini, kupunguza athari zitokanazo na mila na desturi zenye viashiria vya kibaguzi katika jamii. Kwa upande wa Usambazaji, afua zinalenga kuongeza wigo wa huduma bora na rafiki za afya kwa vijana balehe. Aidha, Mazingira Wezeshi yanalenga kutoa elimu na ujuzi kwa vijana ili kuondokana na vikwazo vinavyosababisha vijana balehe kushindwa kushiriki katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
Katika kuratibu na kutekeleza Ajenda hii, Wizara kwa hisani ya Shirika la UNICEF imeajiri Mtaalam Mshauri (Individual Consultant) kwa kipindi cha mwaka mmoja (Mei, 2022 – Aprili, 2023) ili kwa kushirikiana na Wataalam wa Wizara kuratibu na kusimamia utekelezaji wa ajenda hiyo. Vilevile, Mtaalam huyo atawajengea uwezo wataalam wetu katika uratibu na utekelezaji wa Ajenda hii baada ya kumaliza muda wake.
Uratibu na utekelezaji wa Ajenda utakuwa jumuishi na utahusisha wajumbe kutoka Wizara za Kiseka, Idara za Serikali, Vijana balehe na Sekta Binafsi ikiongozwa na Wizara mtambuka na yenye dhamana ya watoto na vijana balehe Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Uratibu utakuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kupitia kamati elekezi ya Taifa ambayo itawahusisha Makatibu Wakuu wa Taasisi za
Serikali.
- Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha
Elimu ya Malezi Chanya kwa Wazazi na Walezi, Wizara kupitia Kitini cha Elimu ya Malezi katika Familia imetoa elimu ya malezi chanya katika mikoa nane (8) ya Kigoma, Kilimanjaro, Songwe, Iringa, Mwanza, Tanga, Mtwara na Mbeya ambapo jumla ya wazazi/walezi 800,000 walifikiwa. Vilevile, Wizara imeandaa Ajenda ya Taifa ya Wajibu wa Wazazi na Walezi katika Matunzo ya Watoto na Familia. Kupitia Ajenda hiyo Wizara imeandaa jumbe mahsusi za kuelimisha wazazi wote wawili kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto. Ajenda imeandaliwa katika nguzo tatu ambazo ni: (i) Mjali Mtoto kwa kumpatia huduma zote za msingi; (ii) Mlinde Mtoto dhidi ya Ukatili; na (iii) Wasiliana na Mtoto mara kwa mara ili kuwa huru kueleza changamoto za makuzi yake na maendeleo kwa ujumla.
- Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha jumbe hizo zinafika kwa wazazi na walezi wengi na kwa ubora, Wizara kwa kushirikiana na Shirika la PACT Tanzania na NIMR Mwanza imetambulisha na kufanya utafiti wa mbinu mpya ya utoaji elimu ya malezi kwa njia ya kidijitali kupitia simu zenye programu tumizi (apps) katika Mikoa ya majaribio ya Mwanza na Shinyanga. Programu tumizi itawezesha wazazi na walezi kupata ujuzi wa malezi bora na kubadilishana taarifa za malezi, makuzi na ulinzi wa watoto katika ngazi ya familia na jamii. Programu hiyo imezinduliwa mwezi Mei 2022 na itasambazwa katika mikoa yote nchini kuanzia mwezi Julai, 2022.
- Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha watoto wanapata haki ya kushiriki na kushirikishwa kwenye masuala yanayowahusu, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeanzisha Mabaraza ya Watoto kuanzia ngazi ya Mtaa/Kijiji, Mkoa na Taifa. Mabaraza ya Watoto ni jukwaa la watoto lililoanzishwa kwa lengo la kuwashirikisha watoto katika masuala yanayowahusu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa na Kikanda ambayo nchi yetu ilisaini na kuridhia. Aidha, ni utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008, inayobainisha Haki ya Kushiriki kuwa ni moja ya haki za msingi za Watoto.
- Mheshimiwa Spika, Mabaraza ya Watoto ni jukwaa linalotumika katika kuwaelimisha watoto masuala mbalimbali yanayohusu maisha yao ya sasa na baadaye nje ya mfumo rasmi wa elimu, ikiwa ni pamoja na uongozi, uadilifu, uzalendo kwa Taifa lao na masuala mengine mtambuka ikiwa pamoja na VVU na UKIMWI, mazingira, stadi za kazi na usawa wa Kijinsia. Mabaraza ya Watoto yameimarisha uwezo wa watoto katika kujitambua, kujiamini, kujieleza na kujilinda dhidi ya ukatili wa aina mbalimbali. Wizara imeanzisha Mabaraza ya Watoto katika ngazi ya Mtaa/Kijiji, Mkoa na Taifa. Hadi Aprili 2022, jumla ya Mabaraza ya Watoto 2,669 yameanzishwa nchini ikiwa pamoja na Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baraza hilo linalojumuisha wajumbe wawili (2) kutoka katika kila mkoa kwenye Mikoa 26 ya Tanzania Bara na wajumbe 10 kutoka Tanzania Visiwani kwa kuzingatia uwiano wa jinsi zote.
- Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto za uundaji wa Mabaraza ya Watoto, Serikali imefanya mapitio ya Mwongozo wa uundaji na uimarishaji wa Mabaraza ya Watoto wa mwaka 2010 ili kuboresha maeneo yaliyokuwa na changamoto. Moja ya eneo lililoboreshwa ni muundo wa mabaraza hayo kupelekwa katika ngazi za shule badala ya kuwa ni jukumu la Kijiji/Mtaa ambapo ufanisi wake umekuwa mdogo. Hivyo, Baraza la Watoto katika ngazi ya chini litakuwa katika shule za msingi na sekondari zilizopo katika Kijiji/Mtaa husika sambamba na uanzishwaji wa Klabu za Watoto shuleni. Uratibu na usimamizi wa Mabaraza ya Watoto utafanywa na Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Afisa Elimu Wilaya na Kata kwa usaidizi wa Mkuu wa Shule au Mwalimu Mkuu. Kupitia Mabaraza hayo, watoto wamepata fursa ya kushiriki kwenye majukwaa mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa na kutoa maoni kwenye nyaraka mbalimbali kama vile maandalizi ya Ajenda ya Wajibu wa Wazazi na Walezi katika Malezi Bora ya Familia na Watoto ya mwaka 2021. Aidha, mwezi Februari, 2022 wajumbe wa Baraza la Watoto la Taifa walipata fursa ya kipekee ya kushiriki katika kutoa maoni ya maboresho ya Mtaala wa Elimu kwa Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vya Ufundi Nchini unaoratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Wizara kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta imedhamiria kuhakikisha watoto wa Taifa hili wanakuwa na ufahamu wa kutosha wa mambo yanayowahusu na hakuna anayekatisha ndoto zao kwa kutumia mwanya wa watoto kutofahamu haki zao.
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeratibu uandaaji wa Mwongozo wa Dawati la Ulinzi na Usalama wa Mtoto ndani na nje ya shule. Dawati hilo linaundwa na Watoto Vinara wanaochaguliwa na Watoto wenzao chini ya usimamizi wa Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Mkuu wa Shule kwa lengo la kuwezesha watoto kutoa taarifa za vitendo vya ukatili na kuweza kubainisha viashiria vya ukatili ili wapate huduma stahiki kwa wakati. Mwongozo huo umefanyiwa majaribio kwa kuanzisha Madawati 185 katika Halmashauri tatu (3) za Mkoa wa Rukwa (Nkasi, Sumbawanga na Mlele). Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia tumekubaliana kuendelea kuanzisha Madawati ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto kwenye Shule za Msingi na Sekondari nchini kuanzia mwezi Julai, 2022. Utekelezaji wa Mwongozo huu unaenda sambamba na Mwongozo wa Malezi, Unasihi na Ulinzi wa Mtoto Shuleni na kwenye Vyuo vya Ualimu ulioandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuanza kutumika Mwaka 2020.
ENEO LA 3: HUDUMA ZA USTAWI WA JAMII
53. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha huduma za ustawi wa jamii kwa watoto, Wizara imeendelea kutoa huduma kwa watoto waliokinzana na sheria katika Halmashauri zote hapa nchini. Kwa kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, jumla ya watoto 2,109 (Me 1,715 na Ke 394) walipatiwa huduma mbalimbali ikiwemo marekebisho ya tabia, unasihi, chakula, malazi, mavazi, huduma za matibabu, msaada wa kisaikolojia na wa kisheria na wengine kuwekwa chini ya uangalizi wa Maafisa Ustawi wa Jamii. Hadi kufikia mwezi Aprili 2022, jumla ya watoto 127 (Me 115 na Ke 12) walifuzu programu za marekebisho ya tabia ikilinganishwa na watoto 82 (Me 77 na Ke 5) kwa mwaka 2020/21. Aidha, Wizara imetoa huduma kwa watoto 257 (Me 232 na Ke 25) katika Mahabusu za Watoto tano (5) za Mbeya, Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Dar es Salaam ikilinganishwa na watoto 413 (Me 380 na Ke 33) mwaka 2020/21 kama inavyoonekana katika
Jedwali Na. 2.
Jedwali Na. 2: Mwenendo wa Watoto walio katika Mahabusu za Watoto.
MWAKA | WASICHANA | WAVULANA | JUMLA |
2015/16 | 37 | 349 | 386 |
2016/17 | 18 | 237 | 255 |
2017/18 | 13 | 278 | 291 |
2018/19 | 34 | 320 | 354 |
2019/20 | 18 | 120 | 138 |
2020/21 | 33 | 380 | 413 |
Aprili, 2022 | 25 | 232 | 257 |
Chanzo: WMJJWM
Kupungua kwa idadi ya watoto katika Mahabusu za Watoto kunatokana na kuanzishwa kwa Programu za Kijamii za marekebisho ya tabia kwa watoto wanaokinzana na sheria ambayo inawachepusha watoto waliofanya makosa ya jinai kwa kutowashtaki Mahakamani na kuwaunganisha na huduma ya marekebisho ya tabia.
- Mheshimiwa Spika, Wizara pia imeendelea kusimamia huduma ya marekebisho ya tabia kwa watoto waliobainika kufanya makosa ya jinai kupitia Shule ya Maadilisho Irambo Mbeya. Hadi kufikia mwezi Aprili 2022, watoto tisa (9) kutoka Shule hiyo wameunganishwa na familia zao katika Mikoa ya Njombe, Shinyanga, Iringa na Arusha baada ya kukamilisha hukumu za marekebisho ya tabia. Watoto hao ni miongoni mwa watoto 296 (Me 280 na Ke 16) waliopewa hukumu ya marekebisho ya tabia kupitia Mahakama mbalimbali za Watoto nchini baada ya kupatikana na hatia kwa makosa ya jinai ikilinganishwa na watoto 219 (Me 210 na Ke 9) waliopatiwa huduma hiyo mwaka 2020/21. Shule hii inatoa marekebisho ya tabia kwa watoto na kuwapatia ujuzi ili wanapokamilisha hukumu zao waweze kujitegemea na kuwa raia wema. Ninapenda kuwapongeza watumishi kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha kwamba watoto waliokinzana na sheria wanarejea kuwa na maadili mema na kuwa raia wema.
- Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha upatikanaji wa haki kwa watoto wanaokinzana na sheria, Wizara imefanya ufuatiliaji katika Magereza yaliyopo Mikoa ya Rukwa, Katavi, Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma. Ufuatiliaji huu umewezesha watoto 16 kuachiwa huru kutoka Gereza Kuu la Segerea na kuwekwa chini ya uangalizi wa Maafisa Ustawi wa Jamii, Jijini Dar es Salaam. Watoto hao kesi zao zimekamilika ambapo baadhi yao wamepewa adhabu kulingana na kesi zao na kutozwa faini na wengine walipewa adhabu ya huduma kwa jamii. Mtoto mmoja (1) kati yao amepata ufadhili kutoka Kanisa la Assemblies of God Dar es Salaam kwa ajili ya kusoma masomo ya uchungaji ambapo ameshajiunga Chuo cha Uchungaji Mtama – Lindi.
- Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuratibu huduma kwa Watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi hapa nchini ambapo jumla ya watoto 218,369 (Me 85,699 na Ke 132,670) walitambuliwa na kupewa huduma mbalimbali zikiwemo msaada wa Bima za Afya, Ada, Lishe, vifaa vya shule, kuunganishwa na familia pamoja na msaada wa kisaikolojia na matibabu. Huduma hizo zimetolewa kwa kushirikiana na Halmashauri na wadau mbalimbali. Hata hivyo, bado nchi yetu inakabiliwa na uwepo wa watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.
- Mheshimiwa Spika, utafiti uliofanyika mwezi Julai 2021 katika mikoa sita (6) ya Dodoma, Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na Iringa ulibaini uwepo wa watoto 5,732 (Me 4,583 na Ke 1,149) wanaoishi na kufanya kazi mitaani. Sababu kuu za uwepo wa watoto hao ni pamoja na kuvunjika kwa ndoa, malezi hafifu kwa familia, msongo rika kati ya watoto wenyewe na umaskini wa kaya. Wengi wa watoto hao hukimbilia maeneo ya mijini na kufanya kazi mbalimbali zikiwemo kuosha magari, kuombaomba, kuuza bidhaa ndogondogo na wengine kuajiriwa katika kazi hatarishi ambazo zinadumaza maendeleo yao na kuwakosesha haki za msingi ikiwemo shule, malezi na afya bora.
- Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na wadau mbalimbali iliandaa hafla ya kihistoria ya chakula cha hisani kwa ajili ya kula pamoja na watoto waishio na kufanya kazi mtaani katika Jiji la Dar es Salaam. Lengo la hafla hiyo iliyofanyika mwezi Machi 2022 lilikuwa ni kuwaonesha watoto hao kuwa Serikali ipo pamoja nao licha ya changamoto wanazokumbana nazo.
Pia, hafla hiyo ililenga kuwasilikiza na kupokea maoni na mapendekezo yao kupitia umoja wao pamoja na kutambua vipawa na vipaji vyao kupitia burudani, michezo na nyimbo mbalimbali zenye ujumbe mahsusi walizoimba wakati wa hafla na mwisho kupata mapendekezo ya pamoja ya namna bora ya kumaliza tatizo hilo.
Kupitia hafla hiyo, Wizara iliunda kikosi kazi chenye wajumbe kutoka Serikalini na Asasi za Kiraia kwa lengo la kutoa ushauri wa kitalaam wa namna ya kutatua tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani. Kikosi kazi hicho kimeanza kazi na Wizara imekipatia Hadidu za Rejea ili kuja na ushauri wa namna bora zaidi ya kutokomeza tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani hapa nchini. Kikosi kazi hicho kipo chini ya Mwenyekiti Bw. David Mulongo, Mkurugenzi wa Shirika la SOS Tanzania. Vilevile, namshukuru sana Mhe. Amos Makalla, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambapo Mkoa huo utakuwa wa mfano katika kukabiliana na changamoto ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.
- Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 kama ilivyofanyiwa urekebu mwaka 2019, Kifungu cha 9 (3) kimetoa wajibu kwa mzazi na mlezi kumlinda na kumtunza mtoto katika maisha yake ya kila siku. Aidha, Kifungu cha 14 cha Sheria hiyo kimetoa adhabu kwa mtu yoyote atakayekiuka au kuvunja Sheria. Wizara imejipanga kuongeza kasi ya kuwafikia wazazi ambao hawakuwajibika ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wengi zaidi hivyo, natoa wito kwa kila mzazi kuhakikisha anatekeleza wajibu wake au kwa namna yoyote ile anahakikisha havunji sheria ya mtoto kwa kuweka mazingira mazuri ya mtoto husika. Aidha, natoa wito kwa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto zilizopo ngazi zote kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kuhakikisha wananchi wanazijua na kuzitumia. Lengo ni kila mtoto aishi maisha ya stahiki yake.
- Mheshimiwa Spika, huduma za malezi ya kambo na kuasili zimeendelea kutolewa kwa watoto wasio na wazazi, walezi au ndugu. Huduma hii inalenga kuhakikisha kuwa watoto wanalelewa katika mazingira endelevu ya familia. Katika kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, jumla ya watoto 46 (wavulana 27 na wasichana 19) walipata huduma ya malezi ya kambo na watoto 45 (wavulana 28 na wasichana 17) waliasiliwa. Natoa rai kwa wananchi wenye mapenzi mema kuwasilisha maombi ya kulea watoto wenye uhitaji wa malezi ya familia.
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu huduma ya uendeshaji wa makao ya watoto hapa nchini. Katika kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, jumla ya Makao 118 yamesajiliwa yakiwa na jumla ya watoto 1,524 (Me 668 na Ke 856). Idadi hii imewezesha kuwa na jumla ya Makao ya Watoto 301 yaliyosajiliwa nchini yakihudumia jumla ya watoto 11,341 (Me 5,713 na Ke 5,628). Aidha, Wizara imeendelea kusimamia Makao ya Watoto yanayomilikiwa na Serikali ambayo ni Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo (Dodoma) yenye uwezo wa kuwahudumia watoto 250 na Kurasini Dar es Salaam yenye uwezo wa kuhudumia watoto 100 walio katika mazingira hatarishi. Makao ya Taifa Kikombo ni ya mfano kwa ukanda wa Afrika Mashariki. Ndani ya makao hayo kuna kituo cha kulelea watoto wadogo mchana ambacho kinahudumia watoto wanaozunguka eneo la makao. Pia makao yana maktaba, ukumbi wa mikutano, viwanja vya michezo mbalimbali, karakana, eneo la shamba lenye ukubwa wa hekari 15 na zahanati inayohudumia watoto na wananchi. Ninachukua fursa hii kuwapongeza Taasisi ya Abbott Fund Tanzania kwa msaada wao mkubwa wa kifedha katika kujenga makao haya ya Kikombo na ununuzi wa vifaa.
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika vituo vya kulelea watoto wadogo mchana (Day Care Centers). Katika kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi Aprili 2022, Wizara imetoa leseni za uendeshaji kwa vituo 362 vikiwa na jumla ya watoto 9,638 (Wavulana 4,083 na Wasichana 5,555) wanaopata huduma ya malezi. Idadi hiyo imewezesha kuwa na jumla ya vituo 2,512 vilivyosajiliwa nchini ambavyo vinahudumia jumla ya watoto 173,032 (Wavulana 82,302 na Wasichana 90,730) kama inavyoonesha katika Jedwali Na. 3.
Jedwali Na. 3: Mwenendo wa Uandikishaji Watoto kwenye Vituo vya
Kulelea Watoto Wadogo Mchana
MWAKA | WASICHANA | WAVULANA | JUMLA |
2015/16 | 34,981 | 33,016 | 67,997 |
2016/17 | 39,790 | 33,791 | 73,581 |
2017/18 | 51,711 | 49,312 | 101,023 |
2018/19 | 76,094 | 72,999 | 149,093 |
2019/20 | 82,539 | 76,940 | 159,479 |
2020/21 | 85,175 | 78,219 | 163,394 |
Aprili, 2022 | 90,730 | 82,302 | 173,032 |
Chanzo: WMJJWM
Aidha, Wizara imeendelea kuboresha utoaji wa huduma katika vituo vya kulelea watoto wadogo mchana kwa kutoa mafunzo kazini kwa Wamiliki wa Vituo na Walezi wa Watoto 1,566 (Me 431 na Ke 1,135) katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Tabora, Shinyanga, Pwani, Shinyanga na Iringa ili kuimarisha stadi za uchangamshi wa awali na makuzi ya watoto wadogo pamoja na kutoa ulinzi wa uhakika kwa watoto wakiwa vituoni.
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia vyuo 33 vinavyotoa Mafunzo ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto vilivyotambuliwa na kupewa vibali vya kuendesha mafunzo hayo. Kati ya vyuo hivyo, chuo kimoja ni cha Serikali kilichopo Kisangara mkoani Kilimanjaro kinachotoa taaluma ya malezi na makuzi ya awali ya mtoto katika ngazi ya stashahada na vyuo 32 ni vya Watu Binafsi.
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na matunzo kwa watoto walio kwenye ndoa zenye migogoro na waliozaliwa nje ya ndoa kupitia Mabaraza ya Usuluhishi wa Ndoa nchini. Kwa kutambua hili, Serikali imeendelea kufanyia kazi mashauri ya migogoro ya ndoa kupitia Mabaraza ya Usuluhishi ambapo kwa kipindi cha mwezi Julai2021 hadi mwezi Aprili 2022, jumla ya mashauri ya migogoro ya ndoa 39,571 yalipokelewa. Kati ya mashauri hayo, mashauri ya migogoro 4,576 yalifikishwa mahakamani, mashauri ya migogoro 19,262 yalisuluhishwa na kuwawezesha wanandoa kupata haki zao na mashauri 15,718 yanaendelea. Natoa wito kwa wanandoa kuzingatia kujifunza maadili ya ndoa kabla ya kupanga harusi kwani itaepusha migongano na migogoro ambayo mwisho wake inaumiza watoto wasio na hatia.
- Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeendelea kuratibu uimarishaji wa utoaji wa Huduma za Ushauri na Msaada wa Kisaikolojia kwa familia na jamii. Huduma hii hutolewa kwa watu wenye misongo ya mawazo, manusura wa vitendo vya ukatili pamoja na migogoro ya ndoa na familia. Kwa kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, jumla ya wahudumiwa 545,501 katika Makazi ya Wazee, Nyumba Salama, Mahabusu za Watoto, Makao ya Watoto, Vituo vya Mkono kwa Mkono, waathirika wa majanga mbalimbali ikiwa ni pamoja na UVIKO19, Janga la moto katika Soko la Karume, manusura wa vita vya Ukraine waliorejea nchini na wazazi wao, wanandoa na wanajamii mmoja mmoja aliyehitaji huduma hii. Aidha, Taasisi ya Ustawi wa Jamii – Dar es Salaam imeanzisha Kituo cha Msaada wa Kisaikolojia na Kijamii kwa lengo la kutoa huduma kwa wanafunzi, wafanyakazi na jamii kwa ujumla. Huduma hizi za Msaada wa Kisaikolojia zinatolewa na Maafisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri na vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Wizara imeweka wazi simu za wataalam wake ngazi zote kuanzia Wizarani, Mikoani hadi Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya kusogeza wataalam hao karibu na jamii kwa njia ya teknolojia ya mawasiliano ya simu. Wananchi wengi wameendelea kuwasiliana na wataalam hawa na kupata msaada wa huduma za unasihi hata wakiwa mbali. Hii ni sambamba na Simu Namba 116 bila malipo ambapo mamilioni ya wananchi wanaoona au kuhisi mazingira ya ukatili hutoa taarifa na kupata msaada na huduma ya unasihi.
- Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuratibu uendeshaji wa Makazi ya Wazee hapa nchini. Kupitia huduma hii Wizara inaratibu makazi 14 yanayoendeshwa na Serikali ambapo hadi kufikia mwezi Aprili 2022, wazee wasiojiweza 271 (Me 160 na Ke 111) wamehudumiwa katika makazi hayo kama inavyoonesha katika Kiambatisho Na. 2. Aidha, Wizara imeendelea kuratibu Makazi ya Wazee yanayoendeshwa na watu binafsi na wakala wa hiari 20 yanayohudumia wazee wasiojiweza 451 (Me 216 na Ke 235). Wazee wasiojiweza wamekuwa wakiongezeka na kupungua kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya wazee kuunganishwa na familia zao pamoja na vifo. Hata hivyo, pamoja na huduma zinazotolewa, baadhi ya Makazi ya Wazee ya Serikali yanakabiliwa na uchakavu wa majengo na miundombinu. Wizara inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea kuboresha majengo na miundombinu kwenye Makazi ya Wazee Misufini yaliyopo Wilaya ya Muheza mkoani Tanga. Makazi haya yakijengwa na kukarabatiwa yatakuwa ya mfano hapa nchini.
- Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuboresha huduma kwa wazee, Serikali ina mpango wa kuanzisha Makazi ya Wazee Kikanda. Lengo ni kuhakikisha tunaboresha zaidi huduma kwa Wazee na kuwezesha kuwa na Makazi ya Wazee kwa uwiano wa kikanda. Awali huduma zilikuwa zinatolewa kwenye Makazi ya Wazee yaliyopo katika Mikoa mbalimbali bila kuzingatia uwiano wa Kikanda. Aidha, baadhi ya Mikoa ina Makazi zaidi ya moja, uwepo wa Wazee wachache kwenye Makazi na kukosekana wahudumu wa kutosha. Wizara inaendelea kutoa elimu kwa jamii ili familia ziweze kuwalea wazee wao na wale wachache watakaokosa huduma katika familia kupata matunzo katika makazi hayo. Vilevile, Serikali ipo katika mchakato wa kuanzisha miradi katika Makazi ya Wazee ili yaweze kupunguza utegemezi kwa Serikali.
- Mheshimiwa Spika, Wizara inaratibu uanzishaji na uendeshaji wa Mabaraza ya Wazee nchini. Kwa kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, Wizara imeratibu uundwaji wa Baraza la Taifa la Ushauri la Wazee lenye wajumbe 31 ambapo watano (5) ni viongozi wa kitaifa na 26 ni wajumbe/wawakilishi kutoka kila Mkoa. Uzinduzi wa Baraza hilo ulifanyika rasmi tarehe 11 Machi, 2022 Jijini Dodoma. Vilevile, Wizara imekamilisha uundwaji wa Mabaraza ya Wazee katika mikoa ya Geita, Pwani, Rukwa na Njombe na hivyo kufikia lengo la kuwa na jumla ya Mabaraza 20,749 katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara. Mabaraza hayo hutumika kama majukwaa ya wazee kwa ajili ya kujadili masuala yanayohusu haki zao pamoja na ushirikishwaji katika masuala yanayohusu maendeleo. Tarehe 17 – 19 Mei 2022, Wizara yangu kwa kushirikiana na Shirika la HelpAge International tuliwezesha Baraza la Wazee la Taifa kufanya kikao jijini Dodoma kwa lengo la kukusanya maoni ya mapitio ya Rasimu ya Sera ya Wazee pamoja na rasimu ya Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji wa Mabaraza ya Wazee nchini. Aidha, jumla ya Wazee 1,547,038 wametambuliwa katika Mikoa 26 na kati yao wazee 937,266 wamepatiwa vitambulisho/ Bima ya Afya kwa ajili ya matibabu. Sambamba na hilo jumla ya madirisha 2,335 ya kutolea huduma kwa wazee yametengwa katika hospitali na vituo vya umma vya kutolea huduma za afya kote nchini.
Pia, Wizara imeendelea kuratibu maadhimisho ya
Siku ya Kimataifa ya Wazee Duniani yanayofanyika tarehe 1 Oktoba kila mwaka ambapo kwa mwaka 2021 maadhimisho hayo
Kitaifa yalifanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma. Jumla ya Wazee 291 kutoka katika Halmashauri nane (8) za Mkoa wa Dodoma walishiriki maadhimisho hayo ambapo Wazee 135 walipatiwa huduma za afya. Natoa shukrani za pekee kwa wadau wa masuala ya wazee wakiwemo HelpAge International na REDESO kwa ushiriki wao mkubwa katika kuwezesha shughuli mbalimbali za wazee. Aidha, naishukuru Wizara ya Afya kuendelea kusimamia upatikanaji wa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
- Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi zote za utoaji wa huduma za ustawi jamii zinazofanywa na Maafisa Ustawi wa Jamii nchini, bado tunakabiliana na changamoto ya upungufu wa Maafisa 22,395 ambayo ni sawa na asilimia 97% ya Maafisa wanaotakiwa kama inavyoonesha katika Jedwali Na. 4.
Jedwali Na. 4: Idadi ya Maafisa Ustawi wa Jamii katika Ngazi Mbalimbali
NA. | NGAZI | MAAFISA WANAOHITAJIKA | MAAFISA WALIOPO | UPUNGUFU | ||
IDADI | % | IDADI | % | |||
1. | Mkoa | 26 | 26 | 100 | 0 | – |
2. | Hospitali za Rufaa za Mikoa | 168 | 35 | 20.8 | -133 | – 79 |
3. | Halmashauri | 1,472 | 490 | 33.3 | -982 | – 67 |
4. | Hospitali za Wilaya | 549 | 65 | 11.8 | -484 | – 88 |
5. | Kata/Vituo vya Afya | 4,494 | 115 | 2.56 | -4,379 | – 97 |
6. | Kijiji/Mtaa / Zahanati | 16,426 | 9 | 0.05 | -16,417 | – 100 |
JUMLA | 23,135 | 740 | 3.2 | -22,395 | – 97 |
Chanzo: OR-TAMISEMI
- Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa Maafisa Ustawi wa Jamii, Wizara itaendelea kuwasiliana na ORTAMISEMI pamoja na OR-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kutatua changamoto ya upungufu wa Maafisa hao hususan katika ngazi ya Kata kwa kuwaajiri kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kadiri bajeti ya Serikali itakavyoruhusu kila mwaka.
Nitoe rai tena kwa Wadau wa Maendeleo yakiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoa ajira za muda kwa Maafisa Ustawi wa Jamii hususan katika ngazi ya Halmashauri, Kata na Kijiji/Mtaa ambapo kuna upungufu mkubwa ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa afua za kutatua changamoto za ustawi wa jamii nchini.
ENEO LA 4. MAENDELEO YA JINSIA NA UWEZESHAJI WANAWAKE
- Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza ajenda ya usawa wa kijinsia, Wizara ilifanya uzinduzi wa Kamati ya Ushauri ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Ahadi za Nchi kuhusu Kizazi Chenye Usawa (Generation Equality Forum – GEF) tarehe 16 Desemba, 2021 Jijini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kamati hiyo ina wajumbe 25 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. Pia, Sekretarieti ya GEF imeanzishwa kwa ajili ya kuratibu shughuli za kila siku za Jukwaa hilo. Katika kutekeleza malengo ya Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa, Tanzania imechagua kuwa kinara wa utekelezaji wa eneo la Haki na Usawa wa Kiuchumi. Aidha, Wizara inaendelea kuratibu ukamilishaji wa Andiko la Programu ya Utekelezaji wa Ahadi za Nchi kuhusu Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa ili iweze kuzinduliwa mwishoni mwa mwezi Juni, 2022. Sambamba na hilo, Wizara inaratibu maandalizi ya Mwongozo wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi utakaowezesha uundaji na uhuishaji wa Majukwaa hayo kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa hadi Taifa ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Juni, 2022. Mwongozo huo utakapokamilika na kuanza kutumika utachochea ufanisi wa utendaji kazi wa Majukwaa hayo na hivyo kuongeza kasi ya jitihada za Serikali katika kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi na kiuongozi. Vilevile, Jukwaa la Kitaifa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi linatarajiwa kuundwa na kuzinduliwa ifikapo tarehe 30 Juni, 2022 baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhuisha majukwaa katika ngazi za mikoa.
- Mheshimiwa Spika, Wizara imekamilisha Kanzidata inayolenga kuwezesha ukusanyaji na utunzaji wa taarifa zinazohusu wasifu, ujuzi na utaalam wa Wanawake katika nyanja mbalimbali hapa nchini ambapo uzinduzi wake ulifanyika tarehe 8 Machi, 2022 katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. Kanzidata hii itawezesha utambuzi wa wanawake wenye sifa za kushika nafasi za uongozi na maamuzi ndani na nje ya nchi. Hadi kufikia mwezi Aprili 2022, jumla ya wanawake 978 walikuwa wamejisajili kwenye kanzidata hiyo kupitia https://twl.jamii.go.tz. Kanzidata hii inahusisha utunzaji wa taarifa za wanawake wenye wasifu mbalimbali kutoka Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.
- Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inalo jukumu la kuratibu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 8 Machi. Kwa mwaka 2022, Tanzania iliadhimisha Siku hii ambapo maadhimisho ya kimkoa yalifanyika katika Mikoa yote 26 Tanzania Bara. Wizara ilishiriki maadhimisho hayo katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga na Arusha. Kaulimbiu ya maadhimisho kwa mwaka 2022 ilikuwa “Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu: Tujitokeze Kuhesabiwa”. Kaulimbiu hii ililenga kuhamasisha uwajibikaji kwa wote katika kuleta usawa wa kijinsia pamoja na kukumbushana umuhimu wa usawa wa kijinsia katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo jumuishi. Kaulimbiu ilitoa fursa ya kutathmini utekelezaji wa Maazimio na Mikataba ya Kimataifa, Kikanda na Kitaifa yenye lengo la kuimarisha jitihada za kuleta amani, usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi. Vilevile, kaulimbiu ililenga kutoa wito kwa wananchi kuona umuhimu wa kujitokeza kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika mwezi Agosti, 2022. Halikadhalika maadhimisho yalilenga kutathmini mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa Maazimio ya Ulingo wa Beijing; Malengo ya Maendeleo Endelevu (2030) hususan Lengo Namba 5 linalohusu Usawa wa Jinsia; na Ajenda ya Afrika Tuitakayo (2063) pamoja na kujenga hamasa na ushiriki wa wananchi katika kuchangia na kuleta usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake. Aidha, maadhimisho haya hutoa fursa ya masoko kwa wanawake wajasiriamali ambapo katika wiki ya kuelekea kilele cha maadhimisho kuanzia tarehe 1 hadi 7 huwa ni wiki ya maonesho ya bidhaa zinazozalishwa na wanawake wajasiriamali.
- Mheshimiwa Spika, Wizara ilishiriki kwenye Mkutano wa Sita (6) wa Kamati Maalum ya Mawaziri wa Umoja wa Afrika wanaoshughulikia masuala ya Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia tarehe 1 Machi 2022. Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa ni kuweka mashauriano ya nchi za Afrika kuhusu Mkutano wa 66 wa
Kamisheni ya Wanawake Duniani(Africa-Wide Consultation for the 66th Session of the Commission on the Status for Women – CSW66). Mkutano huo ulikuwa ni sehemu ya maandalizi ya nchi za Afrika kushiriki Mkutano wa 66 wa Kamisheni ya Wanawake Dunianiuliofanyika New York, Marekani kuanzia tarehe 14-25 Machi 2022. Kaulimbiu ya mkutano wa 66 wa Kamisheni ya
Wanawake Duniani ni Kufanikisha Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake na Wasichana kwenye Sera na Programu za Kukabiliana na Maafa Yanayosababishwa na Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira. Katika mkutano huo, ilikubaliwa kuwa nchi za Afrika ziweke mipango ya kitaifa ambayo inashirikisha kikamilifu wanawake kwenye juhudi za kukabiliana na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na mazingira, kuwezesha ushiriki wa Wanawake na Wasichana kwenye nafasi za uongozi, kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na wasichana, kuongeza ufadhili na uwekezaji kwenye miradi ambayo inazingatia usawa wa kijinsia. Pia, nchi za Afrika zimekubaliana kuimarisha uwezo wa Taasisi za Takwimu za Kitaifa katika kukusanya takwimu na kuzitumia kutambua changamoto na fursa za wanawake na wasichana kushiriki katika kazi za uzalishaji kwenye sekta za kilimo na uchumi wa bluu.
Sambamba na mkutano huo, Wizara kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia za LANDESA na OXFAM zilifanya Mkutano wa Pembeni (Side Event) unaohusu Promoting Women’s Participation and Decision Making in Addressing Climate Change: Tanzania’s Village Land Use Planning Framework ambao ulifanyika tarehe 16 – 17 Machi, 2022 katika ukumbi wa Morena, Jijini Dodoma kwa njia ya mtandao ambapo jumla ya wadau 150 walishiriki mkutano huo.
- Mheshimiwa Spika, Tanzania kupitia Wizara ninayoiongoza ilipokea mwaliko kutoka Ubalozi wa Ujerumani kushiriki Mkutano wa G7 uliofanyika Berlin, Ujerumani kuanzia tarehe 6 – 8 Aprili, 2022. Mkutano huo ulilenga kujadili masuala mbalimbali kuhusu Uzingatiaji wa Usawa wa Kijinsia na Uthaminishaji Mchango wa Wanawake Wanaofanya Kazi Zisizo na Ujira katika Uchumi wa Familia na Taifa.Mkutano huo uliratibiwa na Shirika la UN Women kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO). Aidha, katika mkutano huo Tanzania ilipongezwa kwa juhudi kubwa inayoifanya katika utekelezaji wa lengo namba 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu linalohimiza kukuza ushiriki wa wanawake katika uongozi na nafasi za maamuzi na uwezeshaji wanawake kiuchumi na kuweza kuliweka suala la kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi kuwa moja ya vipaumbele vya Taifa.
- Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, Wizara imeendelea kuwajengea uwezo wanawake wajasiriamali ili kuwa na stadi za kufanya biashara. Katika kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, jumla ya wanawake wajasiriamali 1,167 wamejengewa uwezo kupitia mafunzo yaliyotolewa katika Mikoa ya Shinyanga, Geita, Katavi na Tanga. Katika mafunzo hayo, wanawake walijengewa uwezo kwa kupatiwa elimu kwenye baadhi ya maeneo kama vile kodi, urasimishaji wa biashara, elimu ya hifadhi ya jamii na elimu ya viwango na ubora wa bidhaa. Pia, mbinu mbalimbali za kukuza mitaji pamoja na kupata masoko ya uhakika ya bidhaa zao zilitolewa kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Taasisi za Fedha na Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA). Mafunzo hayo yataendelea kutolewa kwa wanawake katika mikoa yote Tanzania Bara. Aidha, katika kuwezesha wanawake wajasiriamali kupata mitaji ya biashara, Dirisha la Wanawake katika Benki ya Biashara Tanzania (Tanzania Commercial Bank) limewezesha mikopo yenye thamani ya Shilingi
16,138,750,000 kwa wanawake 3,421 wa
Tanzania Bara hadi kufikia mwezi Aprili, 2022.
- Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia katika Taasisi za Elimu ya Juu na Elimu ya Kati, Wizara imewezesha kuandaliwa na kuzinduliwa kwa Mwongozo wa Uanzishaji, Uendeshaji na Ufuatiliaji wa Dawati la Jinsia katika Taasisi za Elimu ya Juu na Elimu ya Kati. Mwongozo huo ulizinduliwa na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 25 Novemba 2021 ikiwa ni jitihada za Serikali za kuweka mfumo wa kushughulikia matukio ya unyanyasaji wa kingono na vitendo vya ukatili katika maeneo ya Taasisi za Elimu ya Juu na Elimu ya Kati. Hadi mwezi Aprili 2022, jumla ya Madawati 13 yameanzishwa katika Vyuo 13 kati ya Vyuo 50 vilivyokusudiwa kufikiwa ifikapo Juni 2022. Vyuo hivyo ni; Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Iringa, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha, Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare, Chuo Kikuu cha St. Augustine (SAUT) Mwanza, Chuo cha Mipango (IRDP) Dodoma na Chuo Kikuu cha Ushirika
Moshi.
- Mheshimiwa Spika, miongoni mwa jitihada zinazofanywa na Wizara katika kuhakikisha Madawati yanaanzishwa kwenye Taasisi za Elimu ya Juu na Elimu ya Kati ni pamoja na: –
- Kuvielekeza Vyuo kuhakikisha kuwa vinateua waratibu, wajumbe na kutenga sehemu maalum kwa ajili ya kutekeleza shughuli za Dawati;
- Kuwajengea uwezo menejimenti za Vyuo na Waratibu wa Madawati ya Jinsia kuhusu namna bora ya uanzishwaji wa madawati hayo; na
- Kufuatilia uanzishaji wa Madawati ya Jinsia katika Vyuo vya Elimu ya Juu na Elimu ya Kati ili kufikia lengo tarajiwa.
Aidha, Wizara imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa ifikapo Juni 2022, Vyuo 50 viwe vimeanzisha Madawati ya Jinsia na kuhakikisha yanafanya kazi. Katika kuwezesha hilo, Wizara inaratibu na kufuatilia matumizi ya Daftari lililoandaliwa mahsusi kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za taarifa za vitendo vya ukatili katika Taasisi za Elimu ya Juu na Kati. Vilevile, Wizara imeandaa Kitini cha Mafunzo kwa ajili ya kuwafundisha Waratibu na Wajumbe juu ya namna ya kuendesha Dawati hili.
ENEO LA 5: URATIBU WA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia usajili, uratibu na ufuatiliaji wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili yachangie katika kuleta maendeleo ya Taifa. Katika kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi Aprili 2022, Wizara imesajili jumla ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 1,217 kati ya Mashirika 500 yaliyopangwa kusajiliwa kwa mwaka 2021/22. Ongezeko la idadi ya Mashirika yaliyosajiliwa linatokana na uboreshaji wa mfumo wa usajili unaowezesha wadau kufanya usajili wa Mashirika kwa njia ya kielektroniki. Aidha, elimu inayoendelea kutolewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na mchango wake katika maendeleo ya nchi imechangia kuongezeka kwa usajili.
- Mheshimiwa Spika, Wizara ilifanya zoezi la uhakiki wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa lengo la kupata idadi sahihi ya Mashirika yaliyo hai na yanayotekeleza shughuli zao kwa kuzingatia Sheria Na. 24/2002 ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kuhuisha kanzidata ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Jumla ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 2,479 yalihakikiwa na kutangazwa kwenye tovuti ya Wizara. Aidha, kutokana na Mashirika kuwa mengi na kusambaa nchi nzima, Wizara iliongeza muda wa uhakiki hadi kufikia tarehe 30 Machi, 2022. Katika kipindi hicho cha nyongeza, jumla ya Mashirika 2,385 yalijitokeza kuhakiki na kufikia jumla ya Mashirika 4,864 yaliyohakiki. Hii imewezesha kanzidata ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwa na Mashirika 7,533 yaliyo hai kati ya Mashirika 12,442 yaliyopo kwenye kanzidata ya Mashirika.
- Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanaratibiwa vizuri nchini, Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali imeanzisha Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ikiwa ni moja ya chombo cha uratibu wa Mashirika hayo. Chombo hiki ni asasi mwamvuli wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Uanzishwaji wa Baraza hilo umerahisisha uratibu wa Mashirika katika ngazi za Mikoa na Halmashauri kwa kuanzisha mitandao katika ngazi hizo, kuwepo kwa Kanuni za Maadili za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali zenye kuimarisha uwazi na uwajibikaji na kuwezesha uwepo wa uwakilishi wa Sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Aidha, Baraza kwa kushirikiana na Serikali limewezesha kufanyika kwa Mkutano wa kwanza wa mwaka wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini mwaka 2021. Lengo la Mkutano huo ni kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kutambua mchango wa mashirika katika maendeleo ya nchi ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2001) na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 Ibara ya 127 (a) na (d). Mkutano huo ulizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 30 Septemba, 2021 Jijini Dodoma ambapo jumla ya Mashirika na Wadau 1,448 walishiriki.
- Mheshimiwa Spika, wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Rais aliielekeza Wizara yangu kushirikiana na wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kama hatua ya kupunguza utegemezi na kuyawezesha kuwa himilivu. Katika kutekeleza agizo hilo, Kamati ya kitaalam inayohusisha wajumbe 20 kutoka Serikalini na kwenye Mashirika hayo iliundwa mwezi Novemba 2021 ambapo mpaka sasa Kamati hiyo imefanikiwa kuandaa andiko la majadiliano na ushirikishaji wa wadau wa Sekta mbalimbali zikiwemo sekta binafsi na wadau wa maendeleo. Kupitia andiko hilo, nyenzo za kukusanyia taarifa zimeandaliwa na zimeanza kutumika kupokea maoni ya wadau nchi nzima katika Kanda tano (5) ambazo ni; Kanda ya Mashariki, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kati. Pia, Kamati imefanikiwa kuajiri Mtaalam Mwelekezi ili kukusanya na kuchakata taarifa na takwimu kisayansi ambapo jumla ya wadau 1,089 wamefikiwa kutoka katika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 1,015 sawa na asilimia 13.7 ya Mashirika 7,533 yaliyo hai. Hata hivyo, zoezi la ukusanyaji wa maoni ya wadau linaendelea kwa njia ya dodoso mtandao (KoboCollect). Aidha, Kikosi Kazi kinatarajia kuendelea kukusanya maoni ya wadau kutoka Sekta Binafsi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo (DPGs). Vilevile, mchakato wa uandaaji wa andiko la Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Julai, 2022.
- Mheshimiwa Spika, Sambamba na uzinduzi wa Mkutano huo, Taarifa ya Mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2020 ilizinduliwa ambayo ilibainisha kuwa Shilingi Trilioni 1.1 zilitumika katika utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, hifadhi ya jamii, uwezeshaji kiuchumi, utawala bora, mazingira, maji, jinsia na haki za binadamu ambapo jumla ya wanufaika 49,697,214 walifikiwa pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania 8,918.
- Mheshimiwa Spika, katika kuboresha uratibu, usajili na usimamizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Wizara imekamilisha ujenzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa asilimia 100 ambapo umeshaanza kutumika. Aidha, Wizara inaendelea kupitia mfumo huo na kufanya maboresho kwa kila hatua iliyokamilika ili kuwezesha utendaji mzuri wa mfumo huo.
- Mheshimiwa Spika, Wizara imetoa mafunzo kuhusu Sheria, Kanuni na Miongozo inayosimamia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kupitia mikutano ya wadau na vyombo vya habari. Jumla ya wadau 970 wamefikiwa kati wadau 1,000 waliyopangwa kufikiwa kwa kipindi cha mwaka 2021/22 katika mikoa ya Arusha (150), Pwani (125), Songwe (50), Mbeya (50), Mtwara (50), Kinondoni (60), Morogoro (25), Geita (52), Shinyanga (70), Tanga (100), Mwanza (123) Tabora (65) na Simiyu (50). Lengo la mafunzo hayo ni kuyawezesha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo ili kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa Taifa.
Aidha, katika kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa Sera ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini, Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali imeanzisha Bodi ya uratibu wa Mashirika hayo. Kwa mwaka 2021/22, Bodi ya nne (4) imewezesha kufanyika kwa zoezi la uhakiki wa Mashirika Tanzania Bara lililoendeshwa kuanzia mwezi Machi 2021 hadi mwezi Machi 2022 na Mkutano wa mwaka wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali uliofanyika kwa mara ya kwanza Septemba, 2021. Vilevile, Bodi imewezesha na kuboresha mazingira ya uwajibikaji na utendaji kazi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ikiwemo ujenzi wa Mfumo wa
Kielektroniki wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
- Mheshimiwa Spika, katika kuboresha ushirikiano baina ya Tanzania Bara na Zanzibar juu ya Masuala ya Muungano na Yasiyo ya Muungano, Idara ilishiriki vikao viwili (2) vilivyofanyika tarehe 18 Novemba, 2021 na tarehe
10 Desemba, 2021 ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mashirikiano baina ya Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara na Ofisi ya Mrajis wa Asasi za Kiraia Zanzibar. Kupitia vikao hivyo, uratibu na usimamizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa pande zote mbili (2) za Muungano umeboreshwa hususan katika masuala ya usajili na kuweka utaratibu wa kutoa barua za utambulisho kwa Mashirika yanayotaka kufanya kazi upande wa Tanzania Bara au Zanzibar.
ENEO LA 6: URATIBU WA UTEKELEZAJI WA MTAKUWWA
87. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kupitia maeneo nane (8) ya utekelezaji (Thematic Areas). Utekelezaji wa MTAKUWWA ulianza mwezi Julai, 2017 na utafikia ukomo mwezi Juni, 2022 na umekuwa ukitekelezwa kwa ushirikiano wa Wizara za Kisekta na Wadau mbalimbali. Baadhi ya mafanikio ya utekelezaji wa Mpango Kazi huu ni kama ifuatavyo: –
- Matukio ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa katika Dawati la Jinsia na Watoto la Polisi yamepungua kwa asilimia
31 kutoka matukio 42,414 mwaka 2020 hadi matukio 29,373 mwaka 2021
(Kielelezo Na. 1). Aidha, matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto yaliyoripotiwa kwenye Dawati hilo yamepungua kwa asilimia 28 kutoka matukio 15,870 mwaka 2020 hadi matukio 11,499 mwaka 2021 kama inavyoonesha katika Kielelezo Na. 2;
- Jumla ya Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 18,186 kati ya 20,750 (sawa na asilimia 88) zimeanzishwa katika ngazi ya Taifa, Mkoa, Halmashauri, Kata na Kijiji/Mtaa mwaka 2021/22 kutoka Kamati 16,343 zilizoanzishwa mwaka 2019/20 sawa na ongezeko la Kamati 1,843. Kamati hizi zinawezesha kubaini na kushughulikia vitendo vya ukatili nchini kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa hadi Taifa. Serikali inaendelea kufanya ufuatiliaji ili kuziimarisha na kuziwezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo;
- Hadi mwezi Februari 2022, Serikali kupitia
OR-TAMISEMI imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 35.55 kupitia asilimia 10 ya Mapato ya ndani ya Halmashauri. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 19.36 zimetolewa kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali 2,881. Fedha hizo zimeendelea kuwawezesha wanawake kujiimarisha kiuchumi na kuboresha uchumi wa kaya;
- Hadi mwezi Aprili 2022, jumla ya Vituo 21 vya Mkono kwa Mkono (One Stop Centers) vimeanzishwa katika Hospitali mbalimbali za Serikali kwenye Mikoa 12 ikilinganishwa na Vituo 14 vilivyoanzishwa hadi kufikia mwaka 2020/21. Jumla ya manusura wa vitendo vya ukatili 1,857 walipatiwa huduma jumuishi ikiwemo huduma za kitabibu, polisi, msaada wa kisheria, ustawi wa jamii kupitia Vituo hivyo. Lengo ni kuwezesha utoaji wa huduma hizo katika eneo moja ili kuepusha usumbufu, ucheleweshaji wa huduma, kuharibu au kupoteza ushahidi. Serikali kwa kushirikiana na Wadau itaendelea kuratibu uanzishwaji wa Vituo vya Mkono kwa Mkono katika Mikoa ambayo haijaanzisha Vituo hivyo ikiwemo Mikoa ya Dodoma, Singida, Tanga, Geita, Katavi, Rukwa, Mtwara, Lindi, Ruvuma, Mara, Kagera, Njombe, Songwe na Manyara. Vituo hivi vinarahisisha huduma kwa kumpa fursa manusura kufika katika kituo na kupata huduma za unasihi, utoaji taarifa kwa Afisa wa Polisi na kupata matibabu. Aidha, vinarahisisha upatikanaji wa haraka wa ushahidi unaotokana na vipimo vya
kitabibu unaowasilishwa katika Mahakama;
- Kuanzishwa kwa Nyumba Salama 10 katika mikoa ya Arusha (3), Iringa (1), Kigoma (1), Mara (2), Manyara (1), Morogoro (1) na Mwanza (1). Nyumba hizi zinatumika kutoa huduma za msingi na hifadhi ya dharura kwa manusura wa ukatili nchini. Kwa kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, jumla ya manusura 493 walihudumiwa kupitia Nyumba hizo. Serikali kwa kushirikiana na Wadau itaendelea kuratibu uanzishwaji wa Nyumba Salama katika maeneo mbalimbali kulingana na uhitaji wake. Napenda kuishukuru Serikali ya Uingereza kupitia Taasisi ya British Council kwa kutupatia msaada wa majengo kwa ajili ya kuanzisha kitengo cha kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu huduma ambayo uratibu wake utashirikisha sekta mbalimbali;
- Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma iliratibu kikao kilichowakutanisha wajumbe wa Kamati ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto ngazi ya Mkoa ili kujadili utekelezaji wa MTAKUWWA, kukumbushana majukumu ya Kamati ngazi ya Mkoa na kuweka mikakati ya kutokomeza ukatili. Kikao hicho kilifanyika tarehe 15 Februari, 2022 ambapo kilihudhuriwa na washiriki 67. Aidha, Wizara iliratibu kikao cha Wadau wanaotekeleza afua mbalimbali za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kilichofanyika tarehe 26 Februari, 2022 Jijini Dodoma kwa lengo la kuweka Mkakati wa pamoja wa kukabiliana na vitendo vya ukatili katika jamii ambapo Wadau zaidi ya 200 waliweza kushiriki. Maazimio ya kikao hicho yalikuwa ni pamoja na: Kuimarisha Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto ngazi zote ili zitekeleze majukumu yao ipasavyo katika kutokomeza vitendo vya ukatili na kuwezesha upatikanaji wa taarifa na takwimu za matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto; Kuelimisha jamii kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo redio za kijamii, sanaa, vyombo vya habari na wadau ili kuijengea jamii uelewa wa masuala ya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto; na kuwe na mabalozi wa MTAKUWWA; na
- Wizara iliwezesha kuzinduliwa kwa Kampeni ya “Twende Pamoja, Ukatili Tanzania Sasa Basi” katika Mkoa wa Mwanza lengo lilikuwa ni kuimarisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ambapo hadi kufikia mwezi Aprili 2022, Kampeni hii ilitekelezwa katika mikoa mitano (5) ya Dar es Salaam, Mara, Mwanza, Katavi na Kigoma. Mikoa hii imefanikiwa kuzindua mpango wa Kampeni hii kati ya mikoa 12 iliyopangwa kufikia 2021. Kutofikiwa kwa idadi hii kulitokana na athari za UVIKO-19.
- Mheshimiwa Spika, pamoja na Takwimu za Jeshi la Polisi kuhusu Hali ya Uhalifu na Matukio ya Usalama Barabarani kuonesha kupungua kwa matukio ya ukatili yaliyoripotiwa mwaka 2021 ikilinganishwa na miaka iliyopita, bado tumeendelea kushuhudia matukio ya vitendo vya ukatili mara kwa mara kwenye vyombo vya habari hususan kupitia mitandao ya kijamii. Pamoja na hatua za kila siku za Serikali na wadau mbalimbali kupambana na ukatili kupitia MTAKUWWA, Wizara inaratibu utekelezaji wa kampeni kubwa ya kupambana na ukatili sambamba na kuimarisha mifumo ya kubaini viashiria vya ukatili na kuchukua hatua za kuzuia.
- Mheshimiwa Spika, kwa kuwa utekelezaji wa MTAKUWWA unafikia ukomo mwezi Juni 2022, Wizara imeanza mchakato wa kufanya tathmini ya Mpango huo kwa lengo la kubaini mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji kwa kipindi cha miaka mitano, changamoto na upungufu wa kimuundo na kiutendaji ulioathiri kufikiwa kwa malengo ya Mpango. Aidha, tathmini inatarajiwa kubainisha masuala ya kuigwa (best practices) na kutoa mapendekezo ya namna bora zaidi ya kukabiliana na changamoto na upungufu uliobainika. Matokeo au mapendekezo yatakayobainishwa katika taarifa ya Tathmini ya Mpango yatawezesha kuanza kwa maandalizi ya MTAKUWWA awamu ya pili itakayotoa mikakati mahsusi ya kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa miaka mitano ijayo.
Katika hatua ya sasa, Wizara imesaini Mkataba na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kutoa huduma ya Ushauri Elekezi katika zoezi la Tathmini ya MTAKUWWA sambamba na kuandaa MTAKUWWA II. Hatua za awali ikiwemo kukamilika kwa wasilisho la kwanza yaani “Inception Report” zimekwishafanyika na hivyo maandalizi kwa ajili ya zoezi la kukusanya na kuchakata taarifa kutoka kwa Wadau mbalimbali linaendelea. Tathmini na Maandalizi ya MTAKUWWA II yanatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Septemba, 2022.
D. UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA
- Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza awali, Wizara imekuwa ikisimamia utekelezaji wa majukumu yake kupitia Taasisi zilizo chini yake ambazo ni Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Taasisi ya Ustawi wa Jamii.
- Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru imeendelea kutoa mafunzo ya taaluma ya maendeleo ya jamii katika ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada na
Stashahada ya Uzamili. Pia, Taasisi imeendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ili kuboresha shughuli za utoaji mafunzo. Katika mwaka 2021/22, Taasisi ilipanga kukusanya kiasi cha Shilingi 3,560,574,000 kutoka vyanzo mbalimbali. Hadi mwezi Aprili 2022, Taasisi imefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi 2,669,377,825 sawa na asilimia 75 ya makadirio.
- Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa masomo 2021/22, Taasisi ilidahili wanafunzi 2,800 katika ngazi zote (Ke 1,857 na Me 943) ikilinganisha na wanafunzi 2,492 waliodahiliwa mwaka 2020/21. Aidha, kwa mwaka 2021/22, jumla ya wanafunzi 1,464 (Ke 1,006 na Me 458) walihitimu katika fani na ngazi mbalimbali ikilinganishwa na wanafunzi 1,003 (Me 262 na Ke 741) waliohitimu mwaka 2020/21.
- Mheshimiwa Spika, Taasisi iliandaa Kongamano kubwa la wanawake tarehe 7 Machi 2022 kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani. Jumla ya washiriki 306 walihudhuria wakiwemo Mabalozi, Mashirika ya Kimataifa, Taasisi za Serikali, Maafisa kutoka Wizara mbalimbali, Wakurugenzi na Maafisa kutoka WMJJWM, Maafisa kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na wawakilishi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Aidha, Taasisi ilifanikiwa kuandika maandiko na kupata ufadhili wa kiasi cha Shilingi Milioni 70 kutoka kwa wadau.
- Mheshimiwa Spika, Taasisi imeandaa programu sita mpya za kitaaluma ambapo programu moja ya kitaaluma ilibadilishana na Taasisi ya Mafunzo ya Serikali za Mitaa (LGTI) – Hombolo. Ushirikiano huu umeongeza idadi ya watumishi wa kitaaluma na wasaidizi wanaofadhiliwa na Taasisi kwa kozi ndefu na fupi. Hadi kufikia mwezi Desemba 2021, wafanyakazi 20 wameanza programu za PhD katika Vyuo Vikuu mbalimbali. Vilevile, wafanyakazi 11 wanaendelea na masomo ya shahada ya uzamili. Pia, watumishi watatu (3) wanahudhuria kozi ya Mhasibu wa Umma Aliyeidhinishwa (CPA) na mmoja anahudhuria kozi ya taaluma ya ununuzi na ugavi. Ili kuongeza umahiri na maarifa ya wafanyakazi kitaaluma, mafunzo ya ndani kuhusu mbinu za utoaji na tafsiri ya mtaala yalifanyika kwa wiki moja Desemba 2021. Aidha, mafunzo kuhusu udhibiti wa msongo wa mawazo yalifanyika kwa wafanyakazi wote ili kuwa na wafanyakazi wenye afya bora wanaofanya kazi. chini ya udhibiti na udumishaji wa utamaduni thabiti, wenye afya mahali pa kazi ambao unafaa kwa ubunifu na tija.
- Mheshimiwa Spika, Taasisi imeendelea kutekeleza programu ya kuchochea na kuendeleza ubunifu (innovation) miongoni mwa wanafunzi kupitia Kituo cha Huduma Tandaa na Ubunifu wa
Kidijitali (Jamii Outreach Digital Innovation Center – JODIC). Kituo hiki kinatumika kuratibu utekelezaji wa programu za ubunifu wa kidijitali, ushirikishaji jamii na uanagenzi katika kazi pana za Taasisi. Kupitia kituo hicho, Taasisi
imetekeleza kazi zifuatazo: –
- Taasisi iliandaa Wiki ya Maendeleo ya Jamii kuanzia tarehe 6-11 Desemba 2021. Katika maadhimisho hayo, maonesho yaliandaliwa katika viwanja vya TICD ambapo wadau wakuu walishiriki na kuonesha bidhaa na huduma zao. Pia, vikundi mbalimbali vya wanafunzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru walionesha bidhaa zao. Maonesho hayo yaliongeza mwonekano wa bidhaa zao, pia kujenga mitandao/muunganisho na kuboresha ujuzi wa masoko, uuzaji na uwekaji chapa kwa wanafunzi;
- Kuhamasisha na kutoa mafunzo kwa vikundi 17 vya wanawake, vijana na walemavu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kuhusu stadi za ujasiriamali;
- Kuanzisha ushirikiano na Kampuni ya Gongali Model ambapo Kituo kiliwasilisha andiko la kufadhili shughuli za Kituo (JODIC);
- Kuendesha mafunzo kuhusu uundaji wa vikundi, taratibu za usajili, fursa za mikopo, uuzaji wa kidijitali, unyanyasaji wa kijinsia na ulinzi wa haki za binadamu kwa wanafunzi 49 na viongozi wa vikundi vya kijamii;
- Kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo shughuli mbalimbali zilifanyika ikiwemo mijadala kuhusu migogoro ya kifamilia inavyochangia unyanyasaji wa kijinsia miongoni mwa wanandoa. Mojawapo ya mambo muhimu yaliyochukuliwa kutoka kwenye mazungumzo hayo ni kutambua kuwa wanaume pia ni waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia. Aidha, mafunzo kuhusu unyanyasaji wa kijinsia yaliendeshwa kwa wanawake 500 kutoka Kata za Akheri, Kikwe na Kiutu Wilayani Arumeru. Pia, ilifanyika kampeni ya uhamasishaji juu ya mambo yanayoendeleza unyanyasaji wa kijinsia na hatua za kukabiliana nayo kwa wanafunzi 200 na 300 wa shule za msingi na sekondari mtawalia; na
- Kutoa mafunzo kwa wanafunzi 289 na wafanyakazi wa taaluma 53 kuhusu uanagenzi na stadi za kuajiriwa kwa ajili ya utekelezaji bora wa programu ya uanagenzi. Aidha, Kituo (JODIC) kilifanya uchanganuzi wa upungufu wa ujuzi kwa wanafunzi 289 ili kubaini maeneo yanayofaa kwa programu ya uanagenzi.
Vilevile, Kituo kiliendesha zoezi la ufuatiliaji na tathmini kwa wanagenzi 274 waliokuwa waandaaji katika mashirika mbalimbali nchini Tanzania.
96. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
Taasisi ya Ustawi wa Jamii ambayo nayo ipo chini ya Wizara ninayoiongoza ni kwamba Taasisi hii imeendelea kutoa mafunzo katika ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada, Stashahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamili katika fani ya
Ustawi wa Jamii na fani nyinginezo zinazoshabihiana nayo. Aidha, Taasisi imeendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye vyanzo vikubwa vya mapato ambavyo ni; ada za wanafunzi, tafiti, ushauri elekezi na vyanzo vingine. Katika mwaka 2021/22, Taasisi ilipanga kukusanya kiasi cha Shilingi 6,356,968,500. Hadi kufikia mwezi
Aprili 2022, Taasisi imekusanya Shilingi
4,877,734,052 sawa na asilimia 77 ya makadirio.
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa masomo 2021/22, Taasisi imedahili wanafunzi 3,234 (Ke 2,104 na Me 1,130) ikilinganishwa na wanafunzi 2,542 (Ke 1,680 na Me 862) waliodahiliwa mwaka 2020/21 sawa na ongezeko la asilimia 27. Kati ya wanafunzi waliodahiliwa mwaka 2021/22, wanafunzi 879 walidahiliwa katika ngazi za Astashahada, wanafunzi 674 ngazi ya Stashahada, wanafunzi 1,586 ngazi ya Shahada na wanafunzi 95 ngazi ya Shahada ya Uzamili. Aidha, katika mwaka 2020/21, Taasisi iliwezesha wanafunzi 2,493 (Ke 1,645 na Me 848) kuhitimu katika fani na ngazi mbalimbali ikilinganishwa na wanafunzi 1,246 (Ke 928 na Me 318) waliohitimu mwaka 2019/20. Kati yao, wanafunzi 938 walihitimu katika ngazi ya Astashahada, wanafunzi 687 ngazi ya
Stashahada, wanafunzi 692 ngazi ya Shahada na wanafunzi 176 walihitimu katika ngazi ya Shahada ya Uzamili.
- Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Ustawi wa Jamii imeendelea kutoa huduma ya msaada wa kisaikolojia kwa wanafunzi na jamii kupitia Kituo chake cha Elimu, Ushauri na Msaada wa Kisaikolojia kilichokarabatiwa kwa ufadhili wa
Shirika la Korea International Cooperation Agency (KOICA). Taasisi ilitoa huduma za kisaikolojia na ushauri kwa manusura 345 wa janga la moto katika Soko la Karume ikiwemo watu wenye mahitaji maalum 150. Kupitia Kituo hiki Taasisi pia imeweza kutembelea shule nne (4) za Wilaya ya Kinondoni na shule moja (1) katika Wilaya ya Mwanga ili kuelimisha wanafunzi kuhusiana na nidhamu, ufaulu na mahusiano. Vilevile, elimu ilitolewa juu ya viashiria vya ukatili wa kijinsia, stadi za kuepukana na makundi mabaya na matumizi ya dawa za kulevya. Kupitia afua hizo, Taasisi iliweza kuwafikia jumla ya wanafunzi 853 na kutoa huduma za ushauri, unasihi na kisaikolojia kwa wanajamii 1,034 wanaoizunguka Taasisi. Yote haya yamelenga katika kuhakikisha malezi na makuzi yanaimarishwa ili kukuza ustawi wa mtu mmoja mmoja, familia na Taifa kwa ujumla.
- Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Ustawi wa Jamii pia imekuwa ikiendesha programu za kushirikisha jamii (community engagement), uanagenzi (apprenticeship) na ubunifu (innovation). Kupitia kituo chake cha ubunifu, Taasisi imeweza kuwajengea ujuzi na uwezo wanafunzi 180 katika muda wa wiki nane (8) ili waweze kutumia teknolojia ya kidijitali kama nyenzo ya kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Kupitia programu yake ya uanagenzi, Taasisi imeweza kuwaunganisha wanafunzi 11 kupata ajira na kuwezesha wanafunzi wengine 56 kupata nafasi mbalimbali za kujifunza stadi za kazi katika mashirika mbalimbali kwa kipindi cha mwaka 2021/22. Pia, Taasisi kupitia porgramu yake ya kushirikisha jamii imewapatia vijana 428 wa Manispaa ya Kinondoni elimu na ushauri juu ya namna ya kukabiliana na changamoto za maisha, afya, mahusiano na namna ya kujikwamua na umaskini.
- Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Ustawi wa Jamii iliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ustawi wa Jamii duniani tarehe 15/3/2022 kwa kutoa huduma za ustawi wa jamii bure kwa wananchi. Huduma zilizotolewa ni pamoja na; ushauri wa masuala ya ndoa na mahusiano, masuala ya watoto waliotelekezwa na ushauri wa kisaikolojia. Vilevile, Taasisi iliadhimisha siku hiyo kwa kufanya vipindi vya luninga kuelimisha jamii juu ya Ustawi wa Jamii na wataalam wa ustawi wa jamii wanavyoweza kusaidia kupunguza changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika jamii.
- Mheshimiwa Spika, Taasisi imeendelea kufanya tafiti zinazohusu changamoto mbalimbali za kijamii ikiwemo utafiti kuhusu utumiaji wa taasisi za kimila na kijamii kukabiliana na ukatili wa kijinsia na jinsi ya kuondoa unyanyasaji wa kijinsia katika Taasisi za Elimu ya Juu. Aidha, Taasisi imejielekeza katika kuimarisha elimu ya malezi na makuzi ya watoto kwa kutoa kozi za awali za makuzi kwa walezi wanaolea watoto katika vituo vya SOS vya Arusha, Dar es Salaam na Mwanza. Katika kutambua umuhimu wa elimu ya awali ya malezi na makuzi, Taasisi imeanza maandalizi wa Mtaala wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Watoto (Early Childhood Care and Development) ambao utatumika kuwajengea uwezo na uelewa walezi hususan walio katika vituo vya kulelea watoto.
- Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 Ibara ya 80, Taasisi imefanya maboresho mbalimbali katika miundombinu yake ya kujifunzia na kufundishia kama ifuatavyo: –
- Taasisi imeendelea kutekeleza mradi wa kujenga maktaba ya kisasa hatua ya nane (phase VIII) na ya mwisho ambapo kazi zilizofanyika ni pamoja na kufunga mfumo wa mawasiliano ya TEHAMA, mfumo wa umeme, kuweka mfumo wa mabomba ya maji, kufunga kiinua (lift), ujenzi wa kuta za ndani na kupaka rangi;
- Katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA, Taasisi imenunua vifaa mbalimbali pamoja na kujiunga na mtandao wa Serikali (Government Network). Pia, Taasisi imefunga seva ya kompyuta yenye uwezo wa kuruhusu hadi wanafunzi 10,000 kutumia mifumo ya TEHAMA iliyopo kwa wakati mmoja na kuongeza wigo wa upatikanaji wa mtandao (Internet BandWidth) kutoka 12MbPs hadi kufikia 22MbPs; na
- Taasisi imekamilisha ujenzi wa madarasa mawili (2) pamoja na ofisi mbili za wafanyakazi katika Kampasi yake ya Kisangara iliyopo Mwanga Kilimanjaro. Madarasa hayo yana uwezo wa kuhudumia wanafunzi 500 kwa wakati mmoja na Ofisi hizo zina uwezo wa kuhudumia watumishi sita (6).
103. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha utendaji kazi na kutoa elimu yenye tija itakayoweza kukuza Ustawi wa Jamii nchini, Taasisi imewafadhili watumishi 32 wanaoendelea na masomo yao katika Shahada ya Uzamivu (PhD), Watumishi sita (6) katika Shahada ya Uzamili (Master’s) na watumishi 48 katika mafunzo ya muda mfupi (Short Courses).
F. UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO
- Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi, Wizara imeendelea kutekeleza afua mbalimbali za miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi na ukarabati wa majengo na miundombinu katika Taasisi na Vyuo vilivyo chini yake. Kwa kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, Wizara iliweza kupokea kiasi chote cha fedha za ndani za maendeleo kiasi cha Shilingi Bilioni 4.9 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Mradi wa Huduma za Ustawi wa Jamii.
Kati ya fedha za ndani zilizopokelewa, Shilingi Bilioni 3.6 ni kwa ajili ya Mradi wa Ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ambapo fedha hizo zimeanza kutumika kwa ajili ya kujenga mabweni mawili, maktaba na ukumbi wa mihadhara katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha, kujenga bweni lenye ghorofa mbili katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Rungemba na kujenga bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 600 katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole. Aidha, fedha hizo zimeanza kutumika kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala na darasa moja katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mlale, kukarabati kumbi mbili za mihadhara (zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 500 kila ukumbi kwa wakati mmoja) pamoja na kujenga ukumbi wa mihadhara (wenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 450 kwa wakati mmoja) katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli. Ujenzi wa miradi hiyo umeanza na upo katika hatua za awali za utekelezaji.
Aidha, kiasi cha Shilingi Bilioni 1.3 kimeelekezwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo na miundombinu katika Taasisi na Vituo vya Ustawi wa Jamii ikiwemo: ujenzi na ukarabati wa majengo na miundombinu katika Shule ya Maadilisho Irambo, Mahabusu za Watoto za Mbeya, Tanga na Arusha; na ujenzi wa hosteli ya wanafunzi katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii (Kampasi ya Kisangara) yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 kwa wakati mmoja. Ujenzi na ukarabati katika Taasisi na Vituo hivyo unaendelea.
- Mheshimiwa Spika, hata hivyo, katika kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara kupitia Vyuo vya Maendeleo ya Jamii inaandaa miradi ya maendeleo ambapo kupitia miradi hiyo ifikapo mwaka 2024/25 inatarajia kukusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 2.1.Aidha, kiasi hicho cha fedha kitaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa Vyuo hivyo kwa Serikali katika uendeshaji wake. Mchanganuo wa miradi hiyo na makadirio ya makusanyo umeoneshwa katika Kiambatisho Na. 3.
G. VIPAUMBELE VYA WIZARA NA BAJETI YA MAPATO, MATUMIZI YA KAWAIDA NA MIRADI YA MAENDELEO KWA MWAKA 2022/23
106. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2022/23, Wizara kupitia Idara na Taasisi zilizo chini yake itatekeleza vipaumbele nane (8) ili kuboresha utoaji wa huduma za maendeleo na ustawi wa jamii: –
- Kuratibu afua za kukuza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake kiuchumi na kiuongozi na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, watoto na wazee;
- Kukuza ari ya jamii kushiriki katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo iliyoibuliwa ngazi ya jamii;
- Kutambua na kuratibu makundi maalum wakiwemo wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) ili kuboresha mazingira ya biashara zao;
- Kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii
Tengeru na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii;
- Kuratibu utoaji wa huduma za msingi kwa watu wenye mahitaji maalum, huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia na huduma ya msaada wa kisaikolojia kwa manusura wa majanga mbalimbali na
makundi mengine yenye uhitaji katika jamii;
- Kuratibu na kuwezesha upatikanaji wa huduma za ustawi wa jamii kwa wazee;
- Kuratibu na kusimamia afua za upatikanaji wa haki za mtoto, ulinzi na malezi chanya ya watoto; na
- Kuimarisha ushiriki na mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika maendeleo ya Taifa.
107. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa hapo juu, Wizara kwa mwaka 2022/23 imekadiria kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 43.4 zitakazotumika kutekeleza majukumu ya Wizara ikiwa ni pamoja na kuwezesha uendeshaji wa ofisi na utekelezaji wa miradi wa maendeleo. Baadhi ya maeneo yaliyotengewa fedha kwa mwaka 2022/23 ni pamoja na: –
- Katika eneo la ukatili na masuala ya usawa wa kijinsia, kiasi cha Shilingi Bilioni 2.65 kimetengwa kwa ajili ya kuratibu utekelezaji wa afua za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikiwemo Kampeni ya
“Twende Pamoja, Ukatili Tanzania Sasa Basi“. Pia, fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kusambaza Mwongozo wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, kuwezesha utekelezaji wa Ahadi za Nchi kuhusu Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa na kuwezesha ushiriki wa wanawake katika Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa;
- Kwenye eneo la watoto, kiasi cha Shilingi Bilioni 2.36 kimetengwa kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na marekebisho ya tabia kwa watoto waliokinzana na sheria, kukarabati Mahabusu za Watoto katika Mikoa ya Mbeya na Arusha, kujenga Mahabusu ya Watoto mpya katika Mkoa wa Mwanza, kuratibu utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto (2021/22 – 2025/26) na kuanzisha vituo vya kijamii vya malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto;
- Katika eneo la wazee, Shilingi Bilioni 1.45 zimetengwa kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa huduma za ustawi kwa wazee wasiojiweza katika Makazi ya Wazee 14 na ukarabati wa majengo na miundombinu katika Makazi ya Wazee ya Ipuli na Njoro;
- Kwenye eneo la Taasisi na Vyuo, kiasi cha Shilingi Bilioni 5.6 kimetengwa. Fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo na miundombinu katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Taasisi ya Ustawi wa Jamii (Kampasi ya Kisangara) na
Vyuo nane (8) vya Maendeleo ya Jamii;
- Eneo la uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali limetengewa kiasi cha Shilingi Milioni 642.3 kwa ajili ya ufuatiliaji wa Mashirika 1,000 katika Kanda tano (5), kuendesha Mfumo wa Kielekroniki wa Usajili wa Mashirika, kuwezesha vikao vya Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, kusajili Mashirika na kuratibu Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali;
- Eneo la maendeleo ya jamii limetengewa kiasi cha Shilingi Milioni 160.2 kwa ajili ya kutekeleza Kampeni ya Kitaifa ya Kuamsha Ari ya Jamii kuhusu ujenzi wa nyumba bora za gharama nafuu kwa kutumia teknolojia rahisi katika mikoa 26 ya Tanzania Bara; na
- Katika eneo la ufuatiliaji na tathmini, kiasi cha Shilingi Milioni 200 kimetengwa.
Fedha hizo ni kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa mipango, programu na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Taasisi, Vyuo na Vituo vya Ustawi vilivyo chini ya Wizara.
H. SHUKRANI
- Mheshimiwa Spika, Wizara imekuwa ikipata ushirikiano mkubwa kutoka nchi rafiki, Mashirika ya Kimataifa na Sekta mbalimbali zinazosaidia na kuchangia katika huduma za maendeleo na ustawi wa jamii.
- Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii ya kipekee kuzishukuru Serikali za nchi za Marekani, Ujerumani, Ubelgiji, Ufaransa na nchi nyingine ambazo zimeendelea kuisaidia Wizara kwa njia mbalimbali. Aidha, naishukuru Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la Misaada la FCDO ambalo limefadhili kazi ya kupokea maoni ya wadau katika maandalizi ya Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini.
- Mheshimiwa Spika, nayashukuru pia Mashirika ya Kimataifa kwa ushirikiano wao waliotoa kwa Wizara. Mashirika hayo ni pamoja na: Mashirika yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa (UNICEF, UN-Women, UNFPA, WHO, IOM na UNESCO); Umoja wa Nchi za Ulaya (EU); Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB); USAID; Abbott Fund; na Global Fund (for HIV, TB na Malaria). Aidha, nazishukuru Taasisi za Kifedha zinazoshirikiana na Wizara ambazo ni pamoja na NMB, CRDB, Stanbic Bank na Benki ya Biashara Tanzania (TCB).
- Mheshimiwa Spika, nayashukuru Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya ndani ya nchi na Mashirika ya Dini kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia uimarishaji wa huduma za maendeleo na ustawi wa jamii. Mashirika hayo ni pamoja na; WiLDAF, TCRF, TAMWA, TAWLA, TGNP, TAYOA, LSF, Plan International – Tanzania, Kivulini, FSDT, The Aga Khan Foundation, CBM International, Segal Foundation, HelpAge International, Save the Children, World Vision,
PACT Tanzania, TradeMark East Africa (TMEA), Equality for Growth (EfG), Landesa, TAWIA, CAMFED, SOS Children’s Village Tanzania, CSEMA; Railway Children Africa, REPPSI, Amani Girls Home, Pelum Tanzania, LHRC, ECPAT, INTERPOL, Haki Elimu, SOS Children Tanzania, TWCC, Compassion International, Care International Tanzania, TECDEN, Pact Tanzania, BAKWATA na CCT.
- Mheshimiwa Spika, nazishukuru Taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo SIDO, BRELA, NIMR, TBS, Shirika la Posta Tanzania, NSSF, TFS, TASAC, TPA, NHIF, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), TASAF, Jeshi la Polisi Tanzania, Jeshi la Magereza Tanzania Bara na TAKUKURU kwa kuendelea kushirikiana na Wizara yangu. Pia, navishukuru Vyuo vilivyo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia uimarishaji wa huduma za maendeleo na ustawi wa jamii. Aidha, nawashukuru wadau wengine waliotoa huduma ya elimu kwa njia za redio, luninga, magazeti na mitandao ya kijamii kuhusu masuala ya maendeleo na ustawi wa jamii. Wadau hao ni pamoja na; Joyce Kiria (kupitia kipindi cha Wanawake Live), Mhe. Vicky Kamata (kupitia kipindi cha Wanawake na Maendeleo) na wadau wengine. Vilevile, navishukuru Vyama mbalimbali vya kitaaluma ikiwemo; CODEPATA, TASWO na Tanzania Bankers Association.
- Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha utekelezaji wa majukumu yangu nikiwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, nimepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi na wafanyakazi wa Wizara. Napenda kumshukuru Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis (Mb), Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa ushirikiano anaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Pia, naomba kuwashukuru Dkt. Zainab Abdi Seraphin Chaula, Katibu Mkuu na Bw. Amon Anastaz Mpanju, Naibu Katibu kwa mchango na ushirikiano wao katika kuwezesha utekelezaji wa majukumu yangu. Aidha, nawashukuru Makamishna, Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo na Wataalam wote wa Wizara kwa utendaji wao mzuri uliowezesha kukamilisha maandalizi ya Hotuba yangu kwa wakati muafaka. Vilevile, kupitia OR-TAMISEMI nawashukuru sana Wakuu wa Mikoa yote, Makatibu Tawala, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa
Halmashauri zote na wataalam wote chini ya ofisi zao na pia wadau wote wa sekta mbalimbali wanaohudumia katika maeneo yao.
- Mheshimiwa Spika, kipekee naomba kuwashukuru Wakuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru.
Pia, nawashukuru Wakuu wa Vyuo nane (8) vya Maendeleo ya Jamii kwa ushirikiano wao mzuri unaonirahisishia utekelezaji wa majukumu yangu. Natoa shukrani kwa sekta zote ambazo tunashirikiana nazo katika kutoa huduma za maendeleo na ustawi wa jamii pamoja na wananchi wote kwa ushirikiano wao. Nawaasa waendelee kuzingatia misingi ya huduma bora na kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya Taifa letu. Aidha, naishukuru Kamati ya Ushauri ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Ahadi za Nchi kuhusu Kizazi Chenye Usawa (Generation Equality Forum – GEF) chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Anjellah Kairuki ambaye niMwenyekiti wa Kamati hiyo.
- Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kuishukuru familia yangu, hususan mume wangu Advocate Metusela Gwajima na watoto wetu pamoja na wote ambao wamekuwa sehemu ya familia yetu kwa uvumilivu wao na kipekee kwa kunitia moyo katika kutekeleza majukumu yangu ya Kitaifa. Aidha, nawashukuru wananchi wote wa Tanzania kwa kuipatia ushirikiano Wizara ninayoisimamia wakati wote wa kutekeleza majukumu yangu na pia kwa wao binafsi kuendelea kupambana kuhakikisha maendeleo na ustawi wa jamii kwa usawa wa jinsia huku wakitumia Simu Namba 116 bila malipo kwa ajili ya kuripoti matukio au viashiria vya ukatili saa 24 kila siku. Aidha, nawahimiza kuendelea kutumia simu zote za wataalam waliopo Wizarani na katika Mikoa na Halmashauri nchi nzima pamoja na namba yangu 0734124191 kwa ajili ya kutoa taarifa za viashiria vya ukatili kama tulivyotangaza kwenye vyombo vya habari na kuziweka kwenye tovuti yetu ya Wizara ambayo ni www.jamii.go.tz.
I. MAOMBI YA FEDHA KWA KAZI ZILIZOPANGWA KUTEKELEZWA KATIKA MWAKA 2022/23
Makadirio ya Makusanyo ya Maduhuli kwa Mwaka 2022/23
116. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23, Wizara imekadiria kukusanya
Shilingi 8,500,000,000 kutokana na ada na tozo mbalimbali za usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, mapato ya ada za mitihani na uuzaji wa mitaala ya Mafunzo ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii na mapato mengine.
Matumizi ya Kawaida
117. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23, Wizara inakadiria kutumia kiasi cha
Shilingi 32,310,981,000 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Kati ya fedha hizo, Shilingi 18,169,057,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyona Shilingi 14,141,924,000 ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi.
Miradi ya Maendeleo
- Mheshimiwa Spika, kwa upande wa shughuli za maendeleo, Wizara inakadiria kutumia Shilingi 11,092,080,000 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi 6,900,000,000 ni Fedha za Ndani na Shilingi 4,192,080,000 ni Fedha za Nje.
- Mheshimiwa Spika, kwa mwaka
2022/23, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum (Fungu 53) inaomba jumla ya Shilingi 43,403,061,000 ili kutekeleza majukumu yake kwa maendeleo na ustawi wa jamii.
- Mheshimiwa Spika, Hotuba hii inapatikana pia katika tovuti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum www.jamii.go.tz.
- Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
VIAMBATISHO
Kiambatisho Na. 1: Idadi ya Watoto Waliosajiliwa na Kupatiwa Huduma katika Vituo 15 vya Mfano vya Kijamii vya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto
NA. | JINA LA KITUO | HALMASHAURI | WAVULANA | WASICHANA | JUMLA |
1. | Kongwa | Kongwa | 31 | 44 | 75 |
2. | Mbande | Kongwa | 28 | 32 | 60 |
3. | Chamwino | Chamwino | 37 | 30 | 67 |
4. | Bahi Sokoni | Bahi | 35 | 31 | 66 |
5. | Mayamaya | Kondoa | 26 | 23 | 49 |
6. | Kidulo | Kondoa | 38 | 32 | 70 |
7. | Soro | Kondoa | 23 | 27 | 50 |
8. | Chibelela | Bahi | 22 | 30 | 52 |
9. | Ngh’ombolola | Bahi | 25 | 27 | 52 |
10. | Mundemu | Bahi | 28 | 29 | 57 |
11. | Saku | Kondoa | 33 | 29 | 62 |
12. | Mlowa Barabarani | Chamwino | 22 | 39 | 61 |
13. | Mbagala Kuu | Temeke | 44 | 35 | 79 |
14. | Mbutu | Kigamboni | 26 | 32 | 58 |
15. | Kimbiji | Kigamboni | 08 | 17 | 25 |
JUMLA | 426 | 457 | 883 |
Chanzo: WMJJWM
Kiambatisho Na. 2: Wazee Wasiojiweza walio katika Makazi ya Wazee ya Serikali
MWAKA | WANAWAKE | WANAUME | JUMLA |
2010 | 239 | 375 | 614 |
2011 | 254 | 324 | 578 |
2012 | 242 | 330 | 572 |
2013 | 257 | 334 | 591 |
2014 | 250 | 332 | 582 |
2015 | 394 | 333 | 727 |
2016 | 238 | 207 | 445 |
2017 | 267 | 247 | 514 |
2018 | 209 | 240 | 449 |
2019 | 179 | 204 | 383 |
2020 | 110 | 179 | 289 |
2021 | 100 | 167 | 267 |
Aprili, 2022 | 111 | 160 | 271 |
Chanzo:WMJJWM
Kiambatisho Na. 3: Miradi ya Maendeleo katika Vyuo vya Maendeleo
Na. | Jina la Chuo | Aina ya Mradi | Hali Halisi ya Mradi Mwaka 2021/22 | Kiasi Kinachotaraji wa Kukusanywa Mwaka 2022/23 | Matarajio ya Mradi Ifikapo Mwaka 2024/25 | Kiasi Kinachotaraji wa Kukusanywa Ifikapo Mwaka 2024/25 |
1. | Rungemba CDTI | Kilimo cha Parachichi | Chuo kina ekari 25 zenye miti 1,500 iliyopandwa mwaka 2019/20 yenye uwezo wa kuzalisha kilo 150,000 za parachichi ifikapo Desemba 2022. Kila kilo ya parachichi itauzwa Shilingi 2,000/= | 300,000,000 | Kupanda ekari 70 zitakazokuwa na jumla ya miti 4,200 ya parachichi yenye uwezo wa kuzalisha kilo 420,000 na kilo moja itauzwa Shilingi 2,000/= | 840,000,000 |
Ufugaji wa Samaki | Chuo kina bwawa la asili lenye ukubwa wa mita za mraba 12,269 lenye uwezo wa kuchukua samaki 245,920 kwa mwaka. Kwa mwaka 2021/22, chuo kimepanda samaki 5,000 aina ya sato ambao watakuwa na kilo 1,250 na kila kilo itauzwa Shilingi 7,000/= | 8,750,000 | Kufuga samaki 245,920 aina ya sato ambao watakuwa na uzito wa kilo 61,480 na kila kilo itauzwa Shilingi 7,000/= | 430,360,000 | ||
Ufugaji wa Nyuki | Chuo kimejenga banda la kufugia chuki lenye uwezo wa kuchukua mizinga 1,000. Kwa mwaka 2021/22 chuo kimeweka mizinga 51 ambapo kila mzinga unatarajiwa kutoa lita 15 za asali na kila lita itauzwa Shilingi 12,000/= | 9,180,000 | Kuweka mizinga 1,000 kwenye banda la kufugia nyuki. Kila mzinga unatarajiwa kutoa lita 15 kwa mwaka na kila lita itauzwa Shilingi 12,000/= | 180,000,000 | ||
2. | Ruaha CDTI | Ufugaji wa Samaki | Chuo kina mabwawa mawili yenye ukubwa wa mita za mraba 534 yenye samaki 3,600 aina ya sato ambao watakuwa na kilo 900 na kila kilo itauzwa Shilingi 7,000/= | 6,300,000 | Kujenga mabwawa sita (6) yenye mita za mraba 2,034 yenye uwezo wa kuchukua samaki 55,800 kwa mwaka ambao watakuwa na uzito wa kilo 13,950 na kila kilo itauzwa Shilingi 7,000/= | 97,650,000 |
Kuzalisha vifaranga vya samaki 3,000,000 kwa mwaka na kila kifaranga kitauzwa Shilingi 150. | 450,000,000 | |||||
3. | Monduli CDTI | Kilimo cha Kahawa | Chuo kina ekari 36 zenye miti 5,650 iliyopandwa mwaka 2019/20 yenye uwezo wa kuzalisha kilo 16,950 za kahawa baada ya miaka mitatu na kila kilo itauzwa Shilingi | 33,900,000 | Kuongeza miti ya kahawa kutoka miti 5,650 hadi kufikia miti 11,300 ambayo itakuwa na uwezo wa kuzalisha kilo 33,900 na kila | 67,800,000 |
Na. | Jina la Chuo | Aina ya Mradi | Hali Halisi ya Mradi Mwaka 2021/22 | Kiasi Kinachotaraji wa Kukusanywa Mwaka 2022/23 | Matarajio ya Mradi Ifikapo Mwaka 2024/25 | Kiasi Kinachotaraji wa Kukusanywa Ifikapo Mwaka 2024/25 |
2,000/=. | kilo itauzwa Shilingi 2,000/=. | |||||
Kilimo cha Migomba | Chuo kina migomba 500 kwenye eneo la ekari tatu (3) yenye uwezo wa kuzalisha mikungu ya ndizi 500 baada ya mwaka mmoja. Kila mkungu utauzwa Shilingi 10,000/=. | 5,000,000 | Kuongeza migomba 3,000 kwenye eneo la ekari 36 yenye uwezo wa kuzalisha mikungu ya ndizi 7,000 na kila mkungu utauzwa Shilingi 10,000/=. | 70,000,000 | ||
JUMLA | 363,130,000 | 2,135,810,000 |
Kielelezo Na. 1: Idadi ya Watu Waliofanyiwa Ukatili wa Kijinsia na Unyanyasaji kwa kipindi cha mwaka 2017 – 2021
Kielelezo Na. 2: Idadi ya Watoto Waliofanyiwa Ukatili wa Kijinsia kwa kipindi cha mwaka 2017 – 2021

