SEKTA YA MADINI KUTOA MABILIONEA NA MAMILIONEA WAPYA

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuonesha dhamira yake ya kutengeza mabilionea na mamilionea wapya kwa kuwapatia fursa ya kuchimba madini kwa kuwaongoza vyema kuelekea kwenye mafanikio.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko baada ya kufanya ziara katika mgodi Busolwa Mining Limited uliopo katika wilaya ya Misungwi jijini Mwanza yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya dhahabu katika mgodi huo.

Waziri Biteko amesema Soko Kuu la Mkoa wa Mwanza limeuza na kununua jumla ya Tani 9 za madini ya dhahabu kwa mwaka kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Aidha, Dkt. Biteko ameipongeza kampuni ya Busolwa Mining kwa uwekezaji mkubwa na wa kisasa ulioufanya mgodini hapo na kutoa fursa za ajira zaidi ya 127 kwa watanzania pamoja na kulipa kodi Serikalini ambapo kwa kipindi cha kuanzia mwishoni mwa mwaka jana hadi mwaka huu tayari imelipa zaidi ya shilingi bilioni mbili.

Sambamba na hayo, Dkt. Biteko amesema Kampuni ya Busolwa imenya uwekezaji unaopaswa kuigwa na wawekezaji wengine ambapo kampuni hiyo imeweka mfumo wa uwekezaji kwa kuwahusisha wananchi wa kawaida kupitia umoja wao wa Isihika ambapo wana asilimia 20 na mwekezaji kampuni ya Busolwa asilimia 80.

Pia, Dkt. Biteko amewataka watendaji na viongozi wa Serikali wanaosimamia Sekta ya Madini kuwasaidia na kuwawezesha wachimbaji madini na si kudhibiti tu wanaokosea ili wachimbaji hao waweze kufanya shughuli zao kwa amani na usalama.

Kuhusu uanzishwaji wa masoko ya madini, Dkt. Biteko amesema yamesaidia kurahisisha biashara na kupunguza changamoto ya utoroshaji madini ambapo amebainisha kuwa kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 hadi kufikia Mwezi Machi Mwaka huu kiasi cha tani tisa ya dhahabu imeuzwa katika Soko Kuu la Madini mkoani wa Mwanza na hivyo kuwapongeza wachimbaji kwa ushirikiano wao.

Naye, Mkurugenzi wa kampuni ya Busolwa Mining, Baraka Ezekiel amesema uwekezaji wa mradi huo ni zaidi ya Dola Milioni 20 ambapo mitambo yake inaweza kusaga mawe ya madini kiasi cha tani 1,200 kwa siku ingawa changamoto ya umeme na maji imekuwa ikisababisha uzalishaji kusuasua.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya Misungwi Veronica Kessy amewahakikishia wawekezaji katika mgodi wa Busolwa kutengeneza mazingira rafiki ya uwekezaji katika wilaya hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *