Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema ofisi yake inafanya kikao kazi cha siku mbili na Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma ili kutathmini utendaji kazi kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Jenista ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kufungua kikao kazi hicho kilichanza leo jijini Dodoma.
Mhe. Jenista amesema ofisi yake imeamua kufanya kikao kazi hicho na watendaji hao kwani ndio wenye dhamana ya kusimamia rasilimaliwatu katika sekta zote za umma nchini kwa ajili ya ustawi wa taifa.

“Tukiongozwa na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, nimeona nikutane na wasimamizi hao wa rasilimaliwatu kwa mara ya kwanza ili kuweka msingi wa kutathmni utendaji kazi katika utumishi wa umma ambao utatuwezesha kujitathmini kwa lengo la kuongeza ufanisi kiutendaji.” Mhe. Jenista ameongeza.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa, ofisi yake inatarajia kufanya tathmni ili kupima utekelezaji wa malengo yaliyowekwa katika kikao kazi cha mwaka jana na kuweka malengo mapya yatakayotekelezwa katika mwaka wa fedha ujao kwenye eneo la utumishi wa umma.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa, Mhe. Rais amefanya kazi kubwa ya kusimamia na kutoa haki na stahiki kwa watumishi wa umma, hivyo ofisi yangu inao wajibu wa kukutana na wasimamizi hao wa rasilimaliwatu ili kuweka mkakati endelevu wa kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa watumishi wa umma.

“Tumeshuhudia Mhe. Rais amefanya mambo mengi mazuri kwa Watumishi wa Umma ikiwemo upandishaji wa madaraja, ulipaji wa malimbikizo ya mishahara, kutoa ajira na kupandisha mishahara kwa asilimia 23.3 kwa kima cha chini, hivyo watumishi tumuunge mkono kwa kufanya kazi kwa bidii bila kushurutishwa, weledi, uzalendo kwa taifa na kutoa huduma bora kwa wananchi,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Kikao kazi hicho kinaongozwa na kaulimbiu isemayo “Utumishi wa Umma wenye Uadilifu, Nidhamu, Ubunifu, Weledi na Uwajibikaji wa Hiari kwa Ustawi wa Taifa”

