WAKUU WA MIKOA SIMAMIENI UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO KWENYE HALMASHAURI

Angela Msimbira, OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Innocent Bashungwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa wote nchini kuhakikisha wanazisimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa ziweze kutumia fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama ilivyopangwa.

Akifungua kikao kazi cha Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa leo tarehe 24 MEI, 2022 Jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri, Naibu Waziri OR-TAMISEMI Mhe. David Silinde amesema Wakuu wa Mikoa wanawajibu wa kusimamia utekelezaji wa Miradi ya maendeleo katika Ngazi za Halmashauri na kuhakikisha Halmashauri zinatekeleza majukumu yao kikamilifu.

Mhe. Silinde amewataka viongozi hao kuhakikisha wanafanya uchambuzi wa mahitaji halisi ya mashine za kukusanyia mapato (POS) ili waweze kufahamu mapungufu yaliyopo na kuchukua hatua stahiki, lengo likiwa ni kuhakikisha mashine hizo zinatumika katika ukusanyaji wa mapato

Amewataka Wakuu wa Mikoa kuzisimamia Halmashauri pindi zinapoandaa makisio ya bajeti ya mapato ya ndani ili bajeti hiyo iendane na uhalisia na fursa zilizopo kwenye Halmashauri.

Mhe. Silinde pia amewataka Viongozi hao kuhakikisha wanazisimamia Halmashauri kujibu hoja zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kaguzi nyingine ili hoja hizo ziweze kufungwa.

Pia amewaagiza Wakuu wa Mikoa wote kufanya maamuzi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa maslahi ya Mkoa na Taifa kwa ujumla na kuwachukulia hatua watumishi wanaokiuka maadili ya utumishi kwa kuzingatia sharia, miongozo na taratibu za Utumishi wa Umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *