NDEJEMBI AITAKA TUME YA UTUMISHI WA UMMA KUSHUGHULIKIA RUFAA KWA WAKATI KUWAWEZESHA WARUFANI KUPATA HAKI ZAO

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi ameitaka Tume ya Utumishi wa Umma kushughulikia kwa wakati rufaa zilizowasilishwa ili kuwawezesha warufani kupata haki zao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma leo wakati akizindua rasmi Tume ya Utumishi wa Umma, ambayo Makamishna wake wameteuliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni na kuapishwa tarehe 21 Mei, 2022 katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.
Naibu Waziri Ndejembi amesema Tume inazo rufaa na malalamiko mengi ambayo yanatakiwa kutolewa maamuzi hivyo haina budi kuyashughulikia ili kutenda haki na kuondoa sintofahamu kwa warufani wanaosubiri hatma ya rufaa zao.

“Wengi wenu hapa Makamisha ni wanasheria na katika sheria mnasema justice delayed is justice denied hivyo mkayashughulikie hayo mashauri kwa wakati,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Ameongeza kuwa, Tume ya Utumishi wa Umma isipofanya uamuzi sahihi na kwa wakati itaongeza malalamiko katika Utumishi wa Umma na kukwamisha shughuli za maendeleo na huduma muhimu ambazo zinazotolewa na waliowasilisha mashauri na rufaa zao.
Akizungumzia utatuzi wa changamoto ya baadhi ya waajiri na warufani kutowasilisha vielelezo vya rufaa kwa wakati, Mhe. Ndejembi amesema kuwa ofisi yake inafanya marekebisho ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003 ambayo yataipa Tume mamlaka ya kusikiliza na kutoa maamuzi ya rufaa kwa kutumia vielelezo vya upande mmoja vilivyopo.
“Kuna mashauri mengi Tume ya Utumishi wa Umma ambayo yanasababisha Tume kulalamikiwa kwa kutotolea maamuzi, wakati vielelezo vya mashauri hayo havijawasilishwa, hivyo tumeamua kurekebisha kanuni ili kuipa Tume mamlaka ya kufanya maamuzi ya rufaa kwa kutumia vielelezo vilivyopo,” Mhe. Ndejembi amefafanua.

Kwa niaba ya Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe. Jaji (Mst.) Hamisa Kalombola amesema kuwa anatambua jukumu kubwa linalowakabili ni kuhakikisha sheria zinazosimia Utumishi wa Umma zinatekelezwa ipasavyo.
“Tunaahidi kuwa tutatekeleza jukumu hilo la kuhakikisha sheria za Utumishi wa Umma zinasimamiwa ipasavyo kwa kuzingatia Haki, Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo ili kuhakikisha Watumishi wa Umma wanaendelea kutoa huduma bora kwa umma na kujenga imani ya wananchi kwa Serikali yao ya Awamu ya Sita,” Mhe. Jaji Kalombola amesisitiza.


Kwa upande wake Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama amesema Tume ni mamlaka ya kwanza ya rufaa katika Utumishi wa Umma hivyo ina wajibu wa kuhakikisha masuala ya nidhamu katika Utumishi wa Umma yanashughulikiwa kwa misingi ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.
Aidha Bw. Kirama ameongeza kuwa, Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma walioteuliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni watapewa mafunzo ya siku tatu ili kuwajengea uwezo kiutendaji.
Tume ya Utumishi wa Umma inalo jukumu kubwa la kuhakikisha usimamizi na uendeshaji wa rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma linatekelezwa kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali ya Utumishi wa Umma iliyopo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *