
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amesema Wizara yake haitarajii kuwepo makazi holela nchini baada ya mwaka mmoja kwa kuwa serikali ilijiwekea malengo ya miaka kumi ya kurasimisha maeneo ya makazi holela.
Zoezi la urasimishaji makazi holela lilianza mwaka 2013 na linarajiwa kukamilika 2023.
Amesema, serikali inakusudia kupima kila kipande cha ardhi hivyo kuwataka Maafisa Ardhi kuhakikisha wanatangulia kupima ardhi tofauti na sasa ambapo wananchi wanawahi kufanya shughuli za ujenzi kabla mipango miji kufanyika.
Dkt. Mabula ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao cha siku moja kati ya Wadau wa Wizara ya Ardhi na Sekta binafsi ili kujadili changamoto mbalimbali zinazohusu sekta ya Ardhi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya upimaji ardhi imeshirikisha sekta binafsi na kulaani tabia ya wabia hao kushindwa kukamilisha kazi zao kwa wakati jambo alilolieleza linachangia suala zima la migogoro inayosikika kwa sasa.

‘’Serikali imetoa kazi kwa sekta binafsi lakini wametukwamisha na ndio kelele unazozisikia kwa sasa’’ Aliongeza Dkt Mabula Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi amesema, Wizara hiyo inatambua uhitaji mkubwa wa kuboresha mifumo ya utawala bora katika sekta ya ardhi kwenye kupanga, kupima, kutoa hati miliki na kutatua migogoro ya ardhi.

‘’Nia ya kuimarisha utawala bora kwenye sekta ya ardhi ni kulinda haki za umiliki za waendelezaji sekta ya ardhi kwa kuongeza uwazi uwajibikaji kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na kuhakikisha usawa kwenye kutoa maamuzi ya masuala ya ardhi pamoja na kuimarisha ushirikishwaji wa wadau katika kutoa maamuzi’’ amesema Dkt Allan Kijazi.
