Na: Jovine Machele

Manchester City imefanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu England, kufuatia ushindi wake wa leo wa mabao 3-2 dhidi ya Aston Villa.
Mpaka dakika 15 za mwisho City walikuwa nyuma kwa mabao ya Phillipe Coutinho na Matty Cash. Lakini wakatumia dakika 12 kupata mabao matatu muhimu kupitia kwa Ikay Gundogan aliyepachika mabao 2 akiingia dakika ya 69 na lingine la ushindi likiwekwa kimiani na Rodri.

Liverpool yenyewe licha ya kushinda 3-1 dhidi ya Wolves, imesalia nafasi ya pili kwa alama zake 92, City ikitwaa ubingwa kwa alama 93.
Mbio za kuwania nafasi ya nne, zimemalizika kwa Spurs kufikisha alama 71 baada ya kuibwaga Norwich kwa mabao 5-0. Arsenal imeshinda 5-1 dhidi ya Everton, ushindi ambao ni wakujifurahisha tu ikifikisha alama 69, na kushika nafasi ya 5 nyuma ya Spurs.
Burnley imeshuka daraja ikiungana na Watford na Norwich, baada ya kuchapwa 2-1 na Newcastle United. Leeds chupuchupu baada ya kushinda jioni kwa mabao 2-1 dhidi ya Brentford na kusalia kwenye EPL mwakani.

Manchester United imemaliza nafasi ya 6 baada ya kulala kwa bao 1-0 dhidi ya Crystal Palace, Chelsea imemaliza nafasi ya 3 ikiibwaga Watford 2-1.
Ma City, Liverpool, Chelsea na Spurs zimefuzu kucheza ligi ya mabingwa Ulaya mwakani, Arsenal na Manchester United zitacheza Europa League huku Westham iliyoshika nafasi ya 7 itacheza Conference League.
