DUWASA: Utekelezaji miradi ya UVIKO-19 wafikia asilimia 81

Na Mwandishi Wetu

KAIMU Meneja Ufundi Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA), Mhandisi Emmanuel Mwakabole amesema utekelezaji wa Mradi wa UVIKO-19 mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 81.

Ameeleza kazi inaendelea vizuri na tayari wapo hatua za mwisho za kukamilisha mradi huo ili wananchi waweze kufaidi matunda ya Rais wao Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

“Sisi DUWASA tulipokea Shilingi Bilioni 1.1 kwa ajili Miradi ya UVIKO-19 na mpaka sasa tumefikia asilimia 81 ya kazi zote,” amesema Mhandisi Mwakabole

Amesema kazi zilizofanyika mpaka sasa, ni kazi ya uchimbaji wa visima, mitaro na ulazaji bomba na ujenzi wa tanki zimekamilika kwa Mji wa Bahi na Ntyuka isipokuwa maeneo machache yamebakia, kuingiza bomba kwenye tanki na eneo la kukata lami na katika mji wa Bahi kuna eneo la mawe.

“Kwa sasa ujenzi wa tenki la mji wa Bahi lenye ujazo wa lita 200,000 unaendelea na kwa upande wa Ntyuka ujenzi umekamilika. Katika eneo la Ntyuka ufuatiliaji wa route ya kutoa maji kisima kipya umekamilika na uchimbaji wa mtaro pia umeanza,” amesema Mhandisi Mwakabole

Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa Bahi, Khalifa Ismaily amesema kibanda cha kuwekea pampu kiko tayari na umeme tayari wameshalipia upo katika hatua za mwisho.

Katika fedha za UVIKO-19 Serikali ya Tanzania ilipata mkopo wa shilingi trilioni 1.3 kama mkopo wa masharti nafuu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambapo shilingi Bilioni 139.4 ziligaiwa kwa Wizara ya Maji kwa lengo la kuhakikisha zinatumika kuondoa changamoto ya maji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *