Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete amewataka wapangaji wa nyumba za NHC ambao wametelekeza nyumba hizo pamoja na kuwa wanazilipia kodi kuondolewa mara moja na kupangishwa watanzania wengine wanaohitaji.
Ridhiwani ameyasema hayo katika Hoteli ya Nashera jijini Dodoma wakati wa kuwaaga Wakurugenzi wa Bodi ya NHC waliomaliza muda wao wa miaka mitatu.
Amesema kuwa baadhi ya wapangaji wa NHC wamekuwa si waungwana kwa sababu wamepangishwa nyumba na wanazilipia kodi lakini hawaishi ndani ya nyumba hizo jambo ambalo ni kinyume na mkataba wa upangaji.
“Lengo la Serikali ya Awamu ya Sita ni kutaka watanzania kupata nyumba za kuishi kwa hiyo ni jambo la ajabu kama baadhi ya watanzania wanaopewa upangaji katika nyumba za NHC na baadaye kuzitelekeza huku wakizilipia kodi, “Hili siyo lengo la Serikali” sasa umefika wakati wapangaji wote wasiotumia nyumba za Shirika wanyang’anywe upangaji na kupangishwa watanzania wengine” Alisema Kikwete
Ameongeza kusema kuwa yeyote atakayebainika kuwa haishi katika nyumba aliyopangishwa sheria ichukue mkondo wake maana mtu huyo atakuwa anawanyima wengine fursa ya kupanga katika nyumba za Shirika.

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Kikwete amewataka Mameneja wa mikoa ya Shirika la Nyumba la Taifa – NHC kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu yao.
“Baadhi ya nyumba za NHC ziko tupu bila wapangaji na meneja anajua lakini akiulizwa anasema hakuna nyumba jambo ambalo halileti taswira nzuri kwa jamii, kwani nyumba zimejengwa ili zipangishwe. Lakini baadhi ya Mameneja wamekuwa hawataki kutoa taarifa za uwepo wa nyumba tupu na hata mteja akitoa taarifa hiyo hapati ushirikiano unaotakiwa’ Alisema Kikwete
Amesema kuwa baadhi ya Mameneja wa Mikoa wa NHC wanakosa uadilifu na kutokuwa na lugha nzuri kwa wateja. Amewataka Mameneja hao kusimamia nyumba za Shirika na kutoa huduma bora kwa wapangaji kama maadili ya utumishi wa Umma yanavyotaka.
Amebainisha kuwa NHC inatoa huduma kwa wananchi ni jukumu la kila meneja kuhakikisha anatoa huduma bora ili kuweza kulipa heshima Shirika na kuondoa sintofahamu kwa wananchi ambao wamekuwa wakilalamika juu ya huduma inayotolewa na baadhi ya Mameneja wa Mikoa.
Wakati huo huo Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa imeitaka Menejimenti ya NHC kuhakikisha inasimamia vyema na kuikamilisha miradi ya Serikali inayotekeleza katika mji wa Serikali Mtumba Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kutembelea miradi hiyo Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Sophia Kongela ameitaka Menejimenti ya NHC kuhakikisha miradi iliyopewa na Serikali ya kujenga majengo nane ya baadhi za Wizara inakamilika kwa wakati.
Dkt. Kongela amesema kuwa Serikali kupitia Wizara zake imeliamini Shirika la Nyumba la Taifa hivyo Menejimenti ihakikishe imani iliyotolewa kwao inatimia kwa kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
“Niwaombe Menejimenti, hakikisheni mnatoa ushirikiano mzuri kwa Wahandisi wanaosimamia miradi hii wanatimiza majukumu yao ipasavyo ikiwemo kuhakikisha vifaa vinavyohitajika vinapatikana kwa wakati na hata ikiwezekana viwepo vyote eneo la ujenzi ili waweze kukamilisha kazi yao vyema” Alisema Dkt. Kongela
Ameongeza kusema kuwa ili kazi hiyo iweze kukamilika kwa wakati ni wajibu wa Menejimenti kuwa karibu sana na wahandisi wanaosimamia miradi hiyo ili kujua mahitaji yao na kuweza kuyapata bila kuchelewa. Amesema kuwa kwa kufanya hivyo ana imani miradi hiyo itakamilika kwa muda uliopangwa bila mikwamo yoyote.
Akijibu hoja hiyo Mkurugenzi wa Ujenzi na Uhandisi NHC Mhandisi Haikamen Mlekio amesema kuwa idara yake imejipanga vyema kuhakikisha miradi hiyo inakamilika ndani ya mwaka mmoja tofauti na mkataba wa ujenzi unaotaka miradi hiyo ikamilike kwa kipindi cha miaka miwili.
“Wajumbe wa Bodi niwahakikishie tu kwamba timu yangu imejipanga vyema kuhakikisha miradi hii tunaitekeleza kwa ufanisi na weledi mkubwa ili kuliletea tija Shirika letu ambalo limepewa dhamana kubwa sana na Serikali ya kujenga Wizara zake tisa hapa Mtumba” Alisema Mhandisi Mlekio.
Kwa upande wake Msimamizi wa ujenzi wa jengo la Wizara ya Madini Mhandisi Peter Mwaisabula ameihakikishia Bodi hiyo kuwa jengo analolisimamia lenye ghorofa tano mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 24% na wako ghorofa ya pili, litakamilika mwezi Oktoba mwaka huu tofauti na mkataba unavyosema na kwamba jengo hilo linajengwa kwa viwango na ubora unaotakiwa.
Bodi ya Wakurugenzi NHC imefanya ziara leo ya kutembelea miradi inayotekelezwa na Shirika hilo katika jiji la Dodoma ukiwemo mradi wa nyumba za makazi Iyumbu, Chamwino, eneo la Njedengwa lenye ukubwa wa ekari 48 ambako zitajengwa nyumba za ghorofa na maduka makubwa ya biashara na mji wa Serikali Mtumba.


