MATUMAINI MAPYA UPATIKANAJI HUDUMA YA MAJI MBOPO

Na Fredy Mshiu

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ipo mbioni kukata kiu ya wakazi wa mtaa Mbopo, kata ya Mabwepande wilaya ya Kinondoni kwa kufikisha huduma ya majisa kwa mara ya kwanza .

Hatua hij inafuatia utekelezaji wa mradi wa maji Makongo hadi Bagamoyo unaoendelea kutekelezwa na DAWASA chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo kwa eneo la Mbopo linalotarajiwa kuanza kupata huduma ya majisafi ifikapo Juni 2022, Mhandisi Juma Kalemera ameeleza kuwa kazi inayoendelea kwa sasa inatoa matumaini kwa wananchi wa Mbopo kupata huduma ndani ya muda uliopangwa.

“Kwa sasa mkandarasi anayetekeleza mradi huu CDEIC & HAINAN JOINT VENTURE anaendelea na kazi ya kufunga mita za maji kwa wateja ili tutakapo ruhusu maji kwenda kwa wananchi yawafikie miundombinu ikiwa imekamilika ili waweze kupata huduma kwa wakati,” ameeleza Mhandisi Kalemera.

Mhandisi Kalemera ameongeza kuwa hadi sasa zaidi ya mita 300 za maji zimefungwa huku zaidi ya wananchi 3,000 wakitarajia kunufaika na huduma ya majisafi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbopo Ndugu Mohammed Bushiri ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kutekeleza mradi mkubwa utakaoleta nafuu ya maisha kwa wananchi ambao awali walikuwa wanatumia maji kutoka kwa watu binafsi.

“Utekelezaji wa mradi huu unaonesha ni jinsi gani Serikali yetu ilivyo sikivu na kuwajali wananchi wake, leo Mbopo tuna matumaini makubwa hivi karibuni tunaenda kupata huduma ya majisafi, lakini zaidi mradi huu hautunufaishi wakazi wa Mbopo tu bali kuna maeneo mengine mengi ambayo hayakuwa na huduma” ameeleza Ndugu, Bushiri.

Ndugu Rashid Kawa, Mkazi wa Mbopo ameeleza kuwa kwa muda mrefu wamekua hawana huduma ya majisafi huku wakitumia gharama kubwa kupata maji kwa watoa huduma binafsi.

“Tumeishi kwa muda Sasa bila huduma ya majisafi huku Mbopo, gharama za maisha zimekua juu kwa kuwa maji tumekua tukinunua kwa bei ghali toka kwa watoa huduma binafsi, tutakapoanza kupata maji sasa maisha yataimarika sana,” ameeleza Ndugu Kawa.

Mradi wa maji kutoka Makongo hadi Bagamoyo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 65.4 na unatarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 450,000 katika maeneo ya Changanyikeni, Vikawe, Goba, Bunju, Wazo, Ocean Bay, Salasala na Mji wa Bagamoyo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *